MASOMO
1.
1Sam 3:3-10,19
2.
1Kor6:13-15,17-20
3.
Yn 1:35-42
Tafakari “ Njoo nanyi
mtaona”
Tunavyoadhimisha
jumapili ya 2 ya mwaka B wa Kanisa tunaongozwa na tafakari isemayo “ njoo nanyi
mtaona” hii ni tafakari inayotutafakarisha juu ya maisha ya kumfuasa Kristu
anawaambia wafuasi wake kuwa waende nyumbani kwake wakaone.
Katika kuenenda na
kukaa katika nyumba ya Bwana ni lazima tutambue na tujiulize swali moja kuwa kwa nini
Kristu anawaambia wanafunzi wake ya kuwa nao waende wataona? Anawaambia hivyo
kusudi wapate kuona, kusikia na kujifunza anawaambia waone ili wapate kuwa si
ili mradi wafuasi bali wapate kuwa wafuasi wazuri.
Tunaambiwa kuwa katika
maisha ya ufuasi wa Kristu lazima pawepo mwongozo na kiongozi, pawepo mtu wa
kuelekeza namna ya kufanya, katika maisha ya kiroho lazima pawepo mwongozaji na
zaidi ya hapo ni lazima pawepo mpatanishi. Hivyo ni mwaliko na wajibu wetu kuwa
kabla ya kufanya utume wetu, kumtangaza Kristu, na kuwa tayari kutumwa na yeye,
ni lazima ni lazima kwanza kuona kristu anavyofanya, kujifunza na kufundishwa
namna ya kufanya. Bwana aliwaita wanafunzi wake waone , wajifunze na
wafundishwe. Hivyo Kristu anavyowaambia wanafunzi wake kuwa “ njoo nanyi mtaona”
alitaka waone kuwa nyumba aliyokuwa anakaa lilikuwa siyo jengo bali ilikuwa
nyumba ya roho, ilikuwa siyo nyumba iliyojengwa kwa mawe, matofari na mbao bali
ilikuwa nyumba iliyojengwa kwa mikono ya mioyo safi na myeupe. Hivyo twaweza
sema kuwa ni kwa msing huu Nazareti nyumbani kwa Yesu ni shule inayofundisha
ukimya, na namna ya kutengeneza maisha ya pamoja, ikiwemo maisha ya familia.
Kristu anawaita wanafunzi wake wajifunze shule ya upendo, uvumilivu, ukimya,
ukarimu, na fadhila nyinginezo. Maisha kuanzia katika familia ni pale ambapo
tunaona na kugundua karama na vipaji mbalimbali. Ili kuweza kufanikisha hilo ni
lazima kuwa katika umoja, kuwa na roho ya ushirikiano katika kuhakikisha kazi
na neno la Mungu linaenda duniani kote.
Tunavyosikia Kristu
akiwaita wafuasi wake waende waone nyumbani mwake, hapa yatubidi tutofautishe
nyumba na jengo. Nyumba imejengwa kwa upendo, heshima, upole, na utii, wakati
jengo limetengenezwa kwa matofali na mawe. Katika nyumba ya Kristu wanafunzi wake
walijifunza shule ya utii na hili andiko limedhihirishwa katika maandiko
matakatifu kama yasemavyo “ akashuka pamoja nao akafika Nazareti na aliwatii”(Lk2:51).
Yesu alipowaambia wanafunzi wake “ njoo
muone waliona pia utii wake kwa mama yake Bikira Maria, waliona upendo wake na
pia wakaona upole wake. Katika nyumba kuna upole sauti kubwa haimlei mtoto (
Fr. F.Kamugisha). Jengo ni kwa ajili ya watu na nyumba ni kwa ajili ya
binadamu. Binadamu ni wachache lakini watu ni wengi, kuwa mwanadamu maana yake
ni kuishi fadhila za kiutu, yaani kuwa na fadhila ya upendo kama wa Kristu,
fadhila ya shukurani, fadhila ya uvumilivu, na fadhila ya upole kama
ilivyosemwa hapo awali.
Kuna mhubiri mmoja
katika mahubiri yake alipata kusema “ Familia ya Yesu, Maria na Yosefu ilikuwa
ni Nyumba na si jengo, ilikuwa familia ya binadamu, jengo wanapokaa wezi
wanyanganyi wa kutumia silaha, makahaba, wachonganishi, waongo, wafanya mipango
mibaya hilo ni jengo siyo nyumba.” Jengo hutoa ulinzi wa namna moja, lakini
nyumba hutoa ulinzi wa kimaadili, kisaikolojia, kimwili , kiroho na kidini.
Haya maneno yamethibitishwa na kudhihirishwa na maandiko matakatifu kama
yasemavyo “ Bwana asipoijenga nyumba waijengao wanafanya kazi bure. Bwana
asipoulinda mji waulindao hufanya kazi bure ( Zab127:1)
Tunafundishwa somo la
kuwasikiliza walezi ( wazazi, ndugu, jamaa na walimu wetu) kwa kuwa kupitia
kwao Mungu hujifunua kutuonyesha njia ya
kwenda, mfano kutoka somo la kwanza kutoka kitabu cha Samweli tunaona Samweli
alikua na kulelewa na Eli ambaye alikuwa kuhani, na Samweli alikuzwa katika
malezi ya kiroho na huyu kuhani Eli hivyo Samuel alikuwa amejaa ufahamu mwingi
juu ya mambo ya dini na mambo ya Kiroho. Cha kushangaza ni kuwa na mbali ya kuwa na ujuzi na ufahamu
juu ya mambo ya Kiroho, tunaona Samweli bado anashindwa kuitambua sauti ya
Mungu kuwa ndiye aliyekuwa akimuita na baadala yake anafikiri kuwa Eli ndiye
aliyekuwa akimwita. Hivyo kwa msingi huu tunapata mwaliko kuwa kuitambua sauti
ya Mungu ni lazima kuhitaji msaada na usaidizi kutoka kwa watu tunaoishi nao
nyumbani mwetu. Vivyo hivyo katika injili ya leo tunaona jambo la namna hiyo
kwamba Yesu anawaita mitume wajifunze kutoka kwa Yesu kama tulivyosikia hapo kabla. Wanafunzi wa
Yesu walikuwa na mwito wa kumtumikia Mungu ila walihitaji maelekezo ili kufikia
lengo lao la kumtumika Mungu na ni kwa msingi huu tunaona Kristu anawaita ili
waone na wakajifunze kutoka kwake namna ya kumtumikia Mungu na kutimiza mapenzi
yake.
Ni mwaliko kwa kila
mmoja wetu, kuwa tayari kujifunza, kupata maelekezo ya kiroho kutoka kwa
viongozi wa kiroho, hasa kuishi maisha ya Sakramenti, kufuata amri za Mungu na
amri za Kanisa.
0 Response to "MAHUBIRI YA JUMAPILI YA PILI YA MWAKA B"
Chapisha Maoni