MAHUBIRI YA
KRISMAS
MASOMO
I.Isa.52:7-10
II.Heb.1:1-6
III.Jn.1:1-18
TAFAKARI:
UPENDO WA MUNGU KWETU UNAJIDHIHIRISHA WAKATI WA KUZALIWA KWA YESU KRISTU.
Tunavyotafakari
kuzaliwa kwa mwokozi wetu Yesu Kristu, kadiri ya masomo jinsi yanavyotuongoza, tunapata
picha kwamba Kristu anazaliwa katika mazingira ya kawaida tena mazingira
hafifu, Katika kuzaliwa kwake Kristu anakosa hata nafasi katika nyumba ya
wageni, na baadala yake anazaliwa katika holi la kulishia ngombe. Katika somo
la kwanza, Isa52:7-10, tunasikia ujumbe na habari njema juu ya utabiri wa nabii
ambapo nabii anasema kuzaliwa kwa Kristu kunaleta amani miongoni mwa wana wa
Israel ambao walikuwa kwenye miangaiko na mifadhaiko. Amani iletwayo na Kristu
ni ile amani ya ndani kwanza. Kuzaliwa kwa Kristu kwa wakati ule, kulibadili
taswira, ya wakati ule ambapo chini ya utawala wa dola ya warumi, maovu , kama
vile uzinzi, ndoa za jinsia moja, rushwa, ukosefu wa amani, upendo, mshikamano
na haki vilishamiri sana. Na Kristu kwa
makusudi anazaliwa katika mazingira duni ambayo hata hayatamaniki kuzaliwa
binadamu. Kristu katika kuzaliwa hivyo ilikuwa ishara kuonesha kwamba alizaliwa
ili ashikamane na mazingira duni ya binadamu, ambapo pia kuzaliwa kwake katika
mazingira duni ya namna hiyo ilikuwa ni pia kielelezo na taswira ya mazingira
ya jamii ya utawala wa warumi ambao ulishamiri maovu mengi kama tulivyoona hapo
kabla.
Mwanadamu
katika kumtafuta Mungu hapo kale, tunaona kuwa wengine walimtafuta Mungu kila
mahali, mfano jamii ya wamonaki hapo kale walijitenga na jamii na kwenda kuishi
jangwani wakijaribu kumtafuta Mungu kuona kama angelipatikana huko, wengine walimtafuta Mungu katika vituo
vya hija n.k. Kwa leo tunapata ujumbe kuwa Mungu atafutwaye amekuja na yupo
kati yetu, Yesu Kristu, yaani Immanuel, Mungu yu pamoja nasi yu katikati yetu.
Ni maskini kama sisi ambapo wakati wa kuzaliwa kwake anazaliwa katika mazingira
yasiyopendeza. Anakosa nafasi katika nyumba ya wageni. Kristu katika kuzaliwa
kati yetu anakuwa mwanadamu kama wanadamu wengine, ili aweze kuishi ubinadamu
huo na kuweza kujua mapungufu ya binadamu na hatimaye kukamilisha kile ambacho
kinakosekana kwa mwanadamu, kwa maana hiyo ni kwamba ubinadamu wa Kristu
unatusaidia kutuondolea ile dhambi ya Adam ambayo ilitufanya tuwe wana wa giza,
na Kristu mwenyewe ambaye siyo mdhambi anatufanya tuwe wana wa nuru kupitia
kushiriki ubinadamu wetu. Wale wote ambao humwamini huwa wana wa Mungu
(Jn1:9-13)
Kristu,
yaani Emmanuel kuzaliwa kwake kati yetu, ni ishara tosha ya maisha mapya na
uhai, Kristu analeta uhai kati yetu, hasa kwa wale ambao wamekata tamaa,
wamepoteza dira katika maisha. Tunaposheherekea kipindi hiki cha Krismas wengi
wetu huwa tunanunua miti ya Krismas na pia kutengeneza mapango ambapo tunaona
mwokozi anazaliwa humo. Mti wa Krismas kama tulivyosikia hapo awali, ni ishara ya
uhai na maisha ya uzima usioharibika, na pango ambamo Kristu amezaliwa ni
ishara ya kuzaliwa katika mazingira duni, na kwa jinsi hiyo Kristu anaungana
nasi binadamu katika kushiriki na kutuinua kutoka katika mapungufu na madhaifu
yetu.
Kristu
kuzaliwa kwake anazaliwa kuwasha moto wa upendo kati yetu, anakamilisha kile
ambacho kinakosekana kwetu sisi binadamu. Upendo umeshuka wakati huu kuwasha
moto uwa upendo. Katika kusheherekea
kwetu sikukuu ya Noel, wengi wetu, tunajitahidi kutakiana amani, na upendo wa
kuzaliwa kwa mwokozi Yesu Kristu,
tunadhihirisha hilo kwa kupeana zawadi na kupeana kadi za Krismas, hili
hatulifanyi kutimiza wajibu wetu, ila linafanyika ili upendo ambao Kristu
amekuja kuuwasha kati yetu uweze kudhihirishwa miongoni mwetu. Padri mmoja
mjezuiti alipata kusema kuwa “ Baada ya mtu kupambana na misukosuko na kujua
mwelekeo wa upepo, mawimbi na mivutano ya hapa na pale, Kama upendo wa Mungu
umo ndani ya mwanadamu kiukamilifu, hivyo mwanadamu angeligundua moto kwa mara
ya pili katika historia ya dunia” Wakati tunaendelea kusheherekea sikukuu ya
Krismas pia basi ni mwaliko kwetu sote kuubeba upendo wa Kristu na kuupeleka
majumbani mwetu, maofisini mwetu na katika maeneo yetu ya kazi.
Tusifikirie
kuwa kuzaliwa kwa Kristu au kusheherekea sikukuu ya Krismas ni kula na kunywa
tu, la hasha, wakati tunakula na kunywa pia tuwafikirie wale ambao hawana hata
cha kuwasaidia katika maisha. Tunaalikwa kugawa huu mkate na kinywaji
tunachokula wakati huu wa Krismas kwa wale ambao ni wahitaji. Sauti ya Mungu
husikika kwa wale wamwombao kupitia kwa wale walionacho. Wakati huu
tunaposheherekea Krismas basi kama mtoto Yesu anavyozaliwa katika mazingira
duni,basi pia kwetu ni mwaliko pia kuwa karibu na watato ambao hawana haki zao
za msingi kama vile malazi, elimu, na haki nyingine za msingi, watoto
tuhakikishe kuwa wameandaliwa na wanasheherekea kumpokea mtoto Yesu katika
mazingira ya upendo, furaha na amani.
0 Response to "MAHUBIRI YA KRISMASS"
Chapisha Maoni