MAHUBIRI JUU YA
JUMAPILI YA MATAWI MWAKA B.
Matukio ambayo
tunaadhimisha leo, ndoo mwanzo wa kile tukiitacho juma kuu. Matukio ya jumapili
ya matawi linaanzia bethania ambayo ni kilometre nne kuelekea kusini mashariki
mwa Yerusalemu. Ni katika mahali hapo ambapo maelfu ya wayahudi walikwea
Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu ya pasaka wanakutana naye Yesu.
Kwa kifupi hebu tuone
injili zinasema nini juu ya safari ya kutoka Bethania kwenda Yerusalemu. Injili
ya Mt. Luka inatumbia kuwa baadhi ya watu walitandaza mavazi yao njiani na
wengine walitandaza matawi njiani ambapo Yesu angelipita. Mwinjili Matayo
anasema vilevile kuwa baadhi walitandaza nguo zao na matawi njiani ambapo Yesu
angelipita. Hivyo kwa hawa wainjili tunaona juu ya kutandaza nguo na Matawi.
Mwinjili Luka natuhabarisha kwamba watu walitandika mavazi yao njiani. Hivyo
tunaambiwa kuwa kutoka injili ya Matayo, Luka, na Mariko kuwa walitandaza
matawi, ni kutoka katika injili ya Yohane tunaambiwa juu ya matawi ya mizeituni
na kwenda kumlaki bwana.
Matawi ya Mizeituni
yana maanisha nini? Hebu tuone historia: Kwa kipindi cha miaka 1000 kati ya
Mfalme Daudi na Yesu. Taifa la Israeli lilitawaliwa na dola mbalimbali. Mnamo
karne ya nane Israel ilitawaliwa na Waasiliano. Wasiria walitawala miliki ya
kaskazini ya Israel.Katika karne ya sita tunaambiwa kuwa wababiloniani
walivamia na kutawala waasiria. Miliki
ya Kusini ambayo ilikuwa miliki ya Yuda ilipinga vikali utawala wa wababiloni.
Kwa msingi huo babiloni iliharibu Yerusalemu na hivyo maelfu ya wayahudi
wakapelekwa uhamishoni babiloni, ila wapersia waliivamia na kuitawala babiloni.
Hivyo wayahudi mateka waliokuwa wamepelekwa uhamishoni babiloni walipewa nafasi
ya kurudi nchini mwao kama wangelitaka. Hivyo hekalu lililoharibiwa na wababiloni linajengwa upya.
Hata hivyo wayahudi walibaki chini ya utawala wa wa persia. Mnamo karne ya nne
Alexander Mkuu aliivamia persia na kuitawala. Hivyo kwa sasa wayahudi wanakuwa
katika utawala wa wagiriki. Baada ya kifo cha Alexander, himaya yake
inagawanywa kwa wafuasi wake. Hivyo wayahudi wanatawaliwa na mataifa mawili,
yaani mataifa ya misri na siria.
Mwisho tunaambiwa kuwa
mnamo karne ya kwanza Yerusalemu inachukuliwa na Roma. Hata hivyo kulikuwa na
kipindi kirefu kati ya utawala wa wagiriki na warumi ambapo wayahudi walikuwa
huru na walifurahia uhuru wao. Waselusian chini ya mtawala antiochus epifanes
walijaribu kwa nguvu zao zote kupenyeza namna yao ya maisha, zikiwemo tamaduni
zao, na mila kwa wayahudi, lakini wayahudi walipinga vikali chini ya utawala wa
makabayo. Neno makabayo maana yake ni Nyundo hivyo makabayo aliwapinga na
kuwapiga vikali maadui wa wayahudi kati ya mwaka 163-164. Hivyo Juda makabayo
aliwafukuza wagiriki wote waliokuwa wamekalia mji wa Yerusalemu. Hekalu la
Yerusalemu lililokuwa limeharibiwa liliwekwa wakfu tena mnamo mwaka 164.KB.
Tukio hili bado hata sasa linasheherekewa na wayahudi, sherehe ya hanuka.
Wakati wagiriki wanataka kulipa kisasi cha kufukuzwa Yerusalem, lakini wayahudi
wakiongozwa na Simon kaka yake na Makabayo, walifanikiwa kuurudisha mji wa
Yerusalemu mikononi mwao. Hivyo kipindi cha utawala wa amani na haki
kilishamiri chini ya utawala wa Simoni.
Kutoka kitabu cha
kwanza cha wamakabayo wayahudi walichukua mji wa Yerusalemu kama ngome yao.
Hivyo waliingia mjini humo wakiwa na matawi ya mizeituni, kwa shangwe na
vigelegele huku wakiga baragumu, kwa kuwa adui mkubwa alikuwa ameshindwa na
ameondolewa Yerusalemu.
Hivyo matumizi ya
matawi ya mizeituni ni ishara ya ushindi mkubwa. Matawi ya Mizeituni yalitumika
pia kama alama ya uhuru kwa waisraeli. Hivyo picha ya matawi ya mizeituni
yalionekana pia katika fedha ya wayahudi tokea mwaka 140-70 baada ya Kristu.
Lakini kabla ya hapo wayahudi chini ya utawala wa warumi walikuwa na kiu ya
kumpaka mpakwa mafuta aidha kutoka katika familia ya makabayo/ Daudi ambaye
angeliangamiza dola ya warumi, na hivyo kuiondoa Yerusalemu chini ya utawala wa
watu wa mataifa. Hivyo umati unamkaribisha Yesu kwa matawi, ishara ya utaifa wa
makabayo, mtu ambaye alikuwa anasubiriwa akiwa kielelezo cha Makabayo, Simoni
au Daudi. Hivyo huyo alitegemewa kuwa mmoja ambaye angelitupilia mbali utawala
wa warumi.
Hivyo hayo ndoo
alikumbana nayo Yesu. Kumbuka alivyowalisha maelfu vipande vitano vya mikate na
samaki wawili kwa fikra zao walijua kuwa ni mwenye uwezo mkubwa hivy0 walitaka
kumfanya mfalme ili awaondoe katika utawala wa warumi. Kadiri ya injili ya
Mtakatifu Yohane, Yesu baada ya kuona hivyo aliondoka na kwenda katika milima
ya mizeituni kuomba na kusali. Kitu cha namna hiyo kinatokea pia katika
jumapili ya matawi, ambapo watu wanamshangilia Yesu na kumwita Hosana mwana wa
Daudi, mbalikiwa ni yeye ajaye kwa jina la Bwana Mfalme wa wayahudi.
Yesu kwa kujua kilicho
akilini mwao, anaingia Yerusalemu siyo kwa farasi au gari la kukokotwa na
farasi, bali anaingia mjini humo kwa punda. Hilo ni jibu lake kwao lenye ujumbe
mkubwa japo haongei ila tendo ambalo analifanya ni jibu tosha kwao. Hivyo huyo
siye mfalme ambaye alikaribishwa kwa matawi ya mizeituni. Yesu anawaweka watu
huru, siyo kwa namna ya makabayo na wenzake. Ushindi wa Yesu unaenda mbele
zaidi ya ule wa makabayo. Ushindi wa Yesu siyo ule ushindi wa mtizamo wa
kivita. Ijumaa kuu tutaona Yesu amenyanyuliwa Juu ya Msalaba, kunyanyuliwa
kwake Juu ya msalaba ndoo ushindi mkubwa ambao utatuweka huru kutoka nguvu za
dhambi na mauti.
0 Response to "MAHUBIRI JUU YA JUMAPILI YA MATAWI MWAKA B"
Chapisha Maoni