MAHUBIRI YA
MKESHA WA KRISIMASS
MASOMO: 1. Isa 62: 1-5
2. Mate 13:16-17. 22-25
3. Mt 1: 1-25
TAFAKARI:
YESU KRISTU KUZALIWA KWETU NI ISHARA YA MAISHA YENYE FURAHA NA AMANI.
Tunaposherekea
mkesha wa kuzaliwa kwa mtoto Yesu Kristu, yaani Emmanuel, Mungu yu pamoja nasi,
yatubidi tutafakari juu ya maana ya Krismass au Noel ina maana gani kwenye
maisha yetu. Katika somo la kwanza kutoka nabii isaiya 62:1-5 tunasikia habari
ya Matumaini kwa waisrael ambao walikuwa kwenye mahangaiko na utumwani,
tunasikia ahadi ya kuzaliwa mkombozi na mwokozi ambaye analeta matumaini,
amani na haki. Tunaposherekea kuzaliwa
kwa mtoto Yesu, tunakumbushwa kuwa, kuzaliwa kwake, ni ishara ya maisha yenye
uzima wa Milele. Kipindi hiki cha Noel,
watu utakuta wamepamba nyumbani kwao kwa miti ya Krismas, Mti wa Krismas ni
ishara ya uhai na uzima kwetu sisi. Pia
kwenye banda la wanyama ambapo Kristu amezaliwa ni ishara ya kuonesha kuwa
Kristu alizaliwa katika mazingira duni, na ni kuonesha kuwa yu kati yetu,
Immanuel, Mungu yu Pamoja nasi.
Katika
kipindi hiki cha kuzaliwa Mtoto Yesu, tunaona wengi wetu tunapeana zawadi na
pia tunaandikiana barua na message zenye ujumbe wa kutakiana amani ya Krismas, Je twaweza kujiuliza swali moja
kuwa kupeana zawadi na kutengeneza chakula kizuri na vinywaji ndio maana ya
Krismass? Jibu ni hapana, hivi vyote ni mapambo na ishara ambazo zinamaanisha upendo wa Mungu kwetu sisi kwa
kuzaliwa Mtoto Yesu. Yesu Kristu, yaani Emmanuel, Mungu yu pamoja nasi
anazaliwa katika mazingira ya ajabu na kawaida. Emmanuel, yaani Mungu yu pamoja
nasi, anazaliwa katika holi la kulishia ngombe, hakupata nafasi katika nyumba
ya wageni, kuzaliwa katika mazingira haya inamaanisha kuwa Kristu alikuja
kushiriki maisha yetu sisi binadamu kama mtu wa maisha duni na maisha ya
kiwango cha chini. Kumbe kuzaliwa kwa
mtoto yesu katika maisha duni, kunatukumbusha ni namna gani Mungu ametupenda.
Tunavyotoa
zawadi za Krismas kwa wakati huu, hatutoi hizo zawadi kwa kuwa ni wajibu wetu
kuzitoa, bali ni kwa sababu ya upendo tulionao kwa nduguzetu, kama sisi twaweza
kufanya hivyo, je Mungu mwenyewe tumfananishe na nani ambaye ametoa zawadi
kwetu ya Kuzaliwa mtoto yesu, ambaye jina lake ni Emmanuel, yaani Mungu pamoja
nasi. Hivyo, kama Mungu yu pamoja nasi, hatuna budi kumpokea na kumfungulia
milango ya Mioyo yetu ili awe nasi. Tukiendelea kutafakari fumbo la umwilisho
wa Kristu, tujiulize kuwa Kristu anapozaliwa
ni kweli anazaliwa mioyoni mwetu? Kwa mazingira ya wakati ule Kristu
hakupata nafasi katika nyumba ya wageni, hivyo Mama yake akapata nafasi katika
holi la kulishia ngombe na mifugo wengine, Je sisi nyumba zetu,yaani roho zetu
ziko tayari kumpokea Kristu ambaye ni Mungu pamoja nasi, na je Kama kufuri za
mioyo yetu zimefungwa Mtoto Yesu ambaye amezaliwa kati yetu tunamkaribisha wapi?
Kwa hali
zetu za maisha, Kristu anapozaliwa anakuja na kanuni mpya za maisha, anatuondoa
kwenye maisha ya unyonge, anakuja kuishi na watu wote bila ubaguzi wa aina
yoyote ile, aidha uwe ni ubaguzi wa rangi, ukabila, udini, na matabaka ya aina
yote ambayo yapo kwenye jamii. Mtoto yesu anapozaliwa kati yetu anakuwa mwanga
wa mataifa, anakuwa mtu wa kuleta upendo, matumaini na kuondoa roho za chuki,
wivu, uchoyo na uzembe. Katika kutafakari kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristu
usiku huu pia tunaalikwa kutafakari juu ya ukimya na kutafakari matendo makuu
ya Mungu( Silent Night) Ukimya unaoongelewa ni hali ya ‘Vigelegele’ na si
‘kelele’ Wakati huu wa Krismas ni wakati wa kugawana kile tulicho nacho
mifukoni mwetu, ni wakati wa kutakiana amani, zawadi hizo basi zisihishie
wakati wa kipindi cha Krismas bali ziendelee katika maisha yetu yote. Krismas
ni kipindi cha kutoa na si kutapanya, kila mmoja ana haki ya kutumia
alichonacho kwa ustaarabu, Krismasi
inatukumbusha juu ya wito wetu wa kutoa hazina zetu kwa wahitaji ambao maisha
yao ni duni. Kristu mwenyewe amezaliwa katika maisha duni, na kupitia maisha
hayo duni anakuja kuwainua wanyonge na waliokandamizwa. Basi sisi
tunavyosheherekea Krismas tukumbuke kugawana mkate wetu wa Krismas na wale ambao maisha yao ni duni, na
kufanya hivyo tutakuwa tumemkaribisha Masiha ambaye anazaliwa katika mazingira
duni mioyoni mwetu.
0 Response to "MAHUBIRI YA MKESHA WA KRISIMASS"
Chapisha Maoni