MAHUBIRI YA JUU YA FAMILIA TAKATIFU YA YESU, MARIA NA YOSEFU.
MASOMO:
1. YbS 3: 2-6. 12 -14
|
2.
Kol 3: 12 - 21
|
3.
Mt 2: 13-15. 19-23
|
TAFAKARI:
Ni
wajibu wa wazazi na walezi kuwalea na kuwakuza watoto katika maadili ya
Kikristu.
Tunavyosheherekea
juu ya jumapili ya Familia takatifu, tunaalikwa kutafakari maisha ya familia ya
kikristu ambayo ndo chimbuko la jumuiya ndogondogo za Kikristu na Kanisa kwa
ujumla. Tukiongozwa na tafakari yetu, basi tunaalikwa sote tuwe wazazi au
walezi kuwakuza watoto katika maadili ya Kikristu.
Katika
familia jambo la kwanza ni kwa upande wa watoto kuwaheshimu wazazi wao yaani
Baba na Mama. (YbS 3: 2-6. 12 -14) Heshima hiyo inapatikana katika familia shule ya
malezi. Hapa tunakumbushwa wajibu wa watoto walionao kwa
wazazi wao.
Katika Familia ya
Yesu, Maria na Yosefu, kuna jambo la kujifunza, kuwa maisha ni safari, kwenye
maisha kuna milima na mabonde. Hayo yote tunayaona katika maisha ya Familia ya
Maria, Yesu, na Yosefu.
Nyumbani ni Shule ya
malezi, katika kukaa nyumbani na wazazi watoto wengi huona kuwa kukaa na wazazi
wao ni msalaba, na pia hutamani kuhama nyumbani kwao na kwenda kusikojulikana,
japo kimsingi malezi mema ya Kikristu huanzia kwenye familia. Kwa upande wa
wazazi na walezi ni wajibu wao kuwa nyumbani wapafanye mahali pa kukalika.
Katika kitabu cha methali kuna haya juu ya familia, rejea “ Mwanangu sikiliza mwongozo wa Baba yako,
wala usiyapuuze maagizo ya mama yako” ( Methal 1:8) Zawadi kubwa ambayo mzazi
anaweza kumpa motto ni kumlea na kumpa mifano mizuri juu ya maadili ya
Kikristu. Lakini hapa kunajambo linashangaza kwamba baadhi ya wazazi
wanawapenda baadhi ya watoto wao ambao ndo wamewazaa wenyewe, wakati hawajui
kuwa watoto walionao hakuna hata mtoto
mmoja ambaye aliwachagua wamzae au hakuna mzazi hata mmoja ambaye alichagua
kuzaa watoto alionao mbali ya mazuri yao, mapungufu yao na maumbile yao.
Mhubiri mmoja mahili Rev. Fr. Faustine Kamugisha alikuwa na haya ya kusema juu
ya kulea watoto “Kulea
watoto ni kama kujenga orofa ya nyumba ishirini kwenda juu. Orofa ikiwa nyumba
ya pili kama imelemaa hakuna anayegundua haraka. Lakini nyumba ya ishirini kila
mtu ataona kuwa orofa imelemaa. Mtoto akifikia umri mkubwa kama kuna jambo
halikwenda vizuri kimalezi litajulikana.”
Katika
Familia tunaona yakuwa ni Kanisa dogo, ambapo sala na maombi hushamili. Kwa
fanya nyumba kuwa kanisa dogo pia watoto hujifunza maadili mema ya Kikristu,
ikiwemo kumcha Mungu. Katika familia inayomtegemea Mungu matunda na kazi yake
vyote huonekana. Katika familia inayosali na kumcha Mungu, utaona hata mienendo
ya wanafamilia na waziwazi utajua kuwa hii ni familia ya Kikristu. Mzaburi anasema kuwa Mungu asipoijenga nyumba
waijengao wanafanya kazi bure (Zaburi 127:1)
Katika
kutafakari juu ya maisha ya familia takatifu tunajifunza kuwa nyumbani ni
mahala pa kufanya kazi, Yosefu alikuwa seremala na alimfundisha Yesu Kazi hiyo,
hivyo tunakumbushwa wajibu kama wazazi au walezi kuwafundisha watoto kazi.
Tunavyofanya kazi mbalimbali tunakuwa tumeshiriki kuendeleza ile kazi ya Mungu
ya uumbaji. Hili linajidhihirisha katika maandiko matakatifu ambapo mtume Paulo
ana sisitiza kuwa asiyefanya kazi na asile. Lakini katika jumuiya zetu tunakuta
mambo ni kinyume kwamba kuna ambao huweka mikono yao mifukoni lakini ikifika
mda wa chakula wanakula bila kuweke hiyo mikono mifukoni ( wategeaji) Inashangaza
kwamba katika familia ni mtu mmoja anafanya kazi lakini wanakula ni tisa na
kenda.
Ili nyumba iwe nyumbani na
si hoteli kufanya kazi ni jambo la kila mwanafamilia kama hana kilema au umri
unaomzuia kufanya kazi. Tatizo kubwa linalokutwa mijini ni wanafamilia au jamaa
toka vijijini kukaa na jamaa zao mijini pengine bila kushiriki shughuli muhimu
za nyumbani. Mwenyeji wao akienda kufanya kazi anawaacha nyumbani pengine
wanatazama runinga bila hata kufanya kazi za nyumbani. Hapa msemo wa mtegemea
cha nduguye hufa angali masikini una maana kubwa. Hili linafanya nyumbani kwa
huyu mgeni siku ya tatu isiwe nyumbani bali hotelini.
Tunaposema “jisikie
nyumbani,” nyumbani tuna maana ya kwamba pawe mahali pa kukalika, mahali pa
amani, furaha, malezi, undugu, faraja, kusikilizana, maelewano, ukarimu na
mahali pa kazi. Baba Mtakatifu Benedict xvi alikuwa na haya ya kusema juu ya Familia “Familia
ni Hekalu au Kimbilio ambapo maisha huanzia, na Kiini cha jamii na Kanisa kwa
ujumla”( Mahubiri juu ya wajibu wa mwafrika- (Africae Munus ,No 42) Papa
anaongeza kusema kuwa watoto hujifunza upendo, na kupenda ikiwa na wao hupendwa
bila kikomo na wazazi na walezi wao. Papa Benedict xvi anaendelea kusema “
Familia ni mahali ambapo utamaduni wa kusamehe na kupatanishwa hushamiri”
anaendelea kusema zaidi kuwa katika familia iliyo imara na ya Kikristu, ndo
tunakuta haki, amani, upendo na mshikamano kati ya Baba, Mama, Kaka, na Dada.
Baba mtakatifu Benedict anaongeza kusema kwamba ili familia ikue kiafya na
kimaadili kuna haja ya kujifunza juu ya sacramenti ya Ekaristi ambapo maisha ya
Mkristu huwa mapya zaidi na zaidi anavyokuwa karibu na sakramenti ya Ekaristi.
Maisha ya
familia yaani Baba, Mama na Watoto, ya weza kufananishwa na mpira wa Miguu
uwanjani ambapo ili kufunga bao lazima wachezaji wote washirikiane, pasipo
kushirikiana matokeo yake ni kufungwa mabao mengi. Vilevile katika Familia
lazima kuwepo moyo wa ukarimu wa kushirikishana mapaji, nguvu, akili, na mapato
yote yatokanayo na kila mmoja akipatacho kwa akili na jasho lake. Mtoto
akikuzwa kwa maadili mema maadili mema pia hii ni kuipunguzia familia aibu kwa
watu. “Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; kazidi kupendwa na
Mungu na watu” (Lk 2: 52) Yesu Kristu mwenyewe amekuwa mfano wa kuigwa ambapo
amekua katika hekima na kimo, lakni kwetu hapa cha kushangaza ni kuwa watoto
wanakuwa katika kimo na si katika hekima.
Watoto wengi hapo awali walizaliwa wakiwa na sura ya malaika lakini hadi
sasa waishabatizwa majina ambayo siyo mazuri kuyatamka, kama vile mwizi, mlevi,
mzinzi, jambazi, tukijiuliza kuwa kwa nini wanaitwa hivyo, jibu ni kuwa malezi
kama malezi kwao yaliwapita pembeni au waliyapiga malezi ya wazazi chenga, na
pia mazingira, saikolojia na vingine vingi vinachangia katika kuwafanya watoto
wawe walivyo kwa sasa. Hivyo twendelee kumwomba Mungu neema ili tufanye hayo
yote kwa sifa na utukufu wake.
0 Response to "MAHUBIRI YA JUU YA FAMILIA TAKATIFU YA YESU, MARIA, NA YOSEFU."
Chapisha Maoni