MASOMO
1.2Sam: 5: 1-3
2. Col 1: 11-20
3. Luk 23: 35-43.
TAFAKARI: UFALME WA MUNGU NI UFALME MKUU KATI YA FALME ZOTE ZILIZOWAHI KUWEPO NA ZITAKAZOKUWEPO
Tunapotafakari juu ya Masomo yetu ya leo, hasa kwenye dominika ya Kristu mfalme, tafakari yetu kwa ujumla inatutafakarisha juu ya ufalme wa Mungu, na ufalme wa Kristu ambao aliuanzisha hapa duniani na ambao upo kati yetu. Mara nyingi waumini wengi na Wakristu kwa ujumla wengi hubaki wanababaika kujua nini maana ya ufalme wa Mbinguni au ufalme wa Mungu?? wengine huenda mbali zaidi wakijiuliza kuwa ufalme wa mbinguni unapatikana wapi hapa duniani, au wengine hufikiria kuwa labda ufalme na utawala wa Mungu uko mahali fulani, au wengine hufikiria kuwa ufalme huo utaonekana baada ya kifo.kumbe la hasha, ufalme huo upo miongoni mwetu, na wala hauko mbali na sisi, Kristu mfalme ambaye tunasheherekea utawala na ufalme wake alishauzindua ufalme wake hapa duniani. Ufalme na utawala wa Kristu, ni tofauti na tawala nyingine za hapa duniani. Ufalme na utawala wa Kristu ni wa namna ya pekee na ni wa aina yake kama tutakavyo ona baadaye.
Ufalme wa Mbinguni na ufalme ambao Kristu aliutangaza ni yale mambo yote ambayo Kristu mwenyewe aliyahubiri. Mambo yenyewe ni kama vile, upendo kwa jirani, msamaha kwa aliyekukosea, kusali, unyenyekevu, uvumilivu, utumishi kwa wote bila kuangalia faida na fadhila nyingine za Kikristu, hayo yote ndo yanafanya utawala wa Mbinguni na ndo tunaona hayo yote yanampa sifa Kristu kuwa mfalme. Na ndipo hapo tunaona kuwa falme za dunia zinakuwa tofauti na ufalme wa Kristu. Tukiweza kuishi hizi fadhila zilizotajwa hapo juu sisi tutajihesabu kuwa wana wa ufalme wa Mungu.
Kristu katika maisha yake tunaona anatangazwa Mfalme ( Christ as the King). Tangu kuzaliwa kwake Kristu alitabiriwa kuwa mfalme na wale magi watatu waliokwenda kushuhudia juu ya kuzaliwa mfalme, na walifanya jitihada kujua alipozaliwa mfalme wa amani na pia walienda na zawadi kwa ajili ya mfalme aliyezaliwa ( Mt 2:2). Wakati wa Kifo chake pia ziliandikwa anwani zikisema "Yesu Mfalme wa Wayahudi" hizo anwani ziliandikwa kwa lugha tatu yaani Kiebrania, Kilatini na Kiyunani, na ile ambayo hadi leo huwa inaonekana na kusomeka vizuri ni ile ya Kilatini, tukiangalia kwenye Misalaba mikubwa makanisani, tunaona anwani imeandikwa juu ya msalaba kwa maneno ya kilatini ambayo huwa yamefupishwa " INRI" ambapo kirefu cha haya maneno kwa Kilatini ni " IESUS NAZARENUS REX IUDEOURUM= IESUS- I- Jesus, NAZARENUS= Nazaret, REX= King, IUDEORUM= Juda- Jews. Kwa kuandika kifupi Ukichukua kila herufi mojamoja kwa kila neno tunapata mojawapo ya anwani iliyoandikwa juu ya msalaba aliposulibiwa kristu ambayo iliandikwa kwa kilatini " INRI"
Pilato aliandika kuwa yesu alikuwa mfalme wa wayahudi, kwa kuandika hivyo pilato aliandika hivyo kwa lugha tatu kama tulivyoona, Kigiriki, kilatini na Kihebrania, Pilato kuandika hivyo hakumaanisha kwa dhati kuwa Yesu alikuwa mfalme wa wayahudi ila aliandika hivyo kwa madharau juu ya Yesu Kristu. Mbali ya kuandika hivyo, Mungu alimtumia Pilato kama nyenzo kufikisha ujumbe kuwa kweli huyu alikuwa mfalme wa wayahudi
Katika msalaba msalaba aliposulubiwa Yesu Kristu, juu yake kama tulivyoona hapo awali kuwa ziliandikwa lugha tatu yaani Kilatini, Kigiriki na Kihebrania, hii ilikuwa na maana yake kiteolojia. Kwanza tujue kuwa Mungu ndani ya Maovu aweza leta mazuri, japo kwa akili ya kibinadamu hii haieleweki. Tuanze na ile Lugha ya Kigiriki, hii inamaanisha lugha ya watu wa mataifa ( Gentile Nations) ambapo hii anwani iliandikwa kumaanisha kuwa yesu alikuwa siyo tu mtu wa watu fulani ila alikuwa ni mfalme wa mataifa.tukumbuke kuwa pia Kigiriki ilikuwa pia lugha ya mawasiliano kwa nyanja ya taaluma kama vile falsafa kwa wagiriki na watu wengine duniani. Kilatini, hii ni lugha ambayo ilitumiwa na Warumi katika kufanya mawasiliano, hasa katika uwanja wa utawala na sheria, hivyo Krisstu kama mfalme alijulikana pia kwenye dola ya warumi kama mfalme wao. Kihebrania, pia kama anwani iliyoandikwa juu ya msalaba iliongea kama lugha ya neno la Mungu maana ndo lugha iliyotumika katika Biblia kwa upande wa Agano la kale. Ni kwa msingi huu Katika Lugha zote tatu yesu anatangazwa kuwa mfalme wa wafalme.
Kristu alikuja duniani kama tulivyoona hapo awali kuwa alikuja kuleta ufalme wa Mbinguni na yeye mwenyewe alisema kuwa tubuni na kuamini maana ufalme wa mbinguni umefika ( Mk 1:15) alikuja kuanzisha ufalme huo ili watu wapate wokovu. Katika moja ya maandishi yake, Mtakatifu Augustino alisema haya " Ufalme wa Kristu ni kwa wale ambao siyo wa dunia hii maana wao kwa neema ya Mungu siyo tena wana wa nguvu ya giza" sisi tumsikilizaye na kumfuata Kristu, ni wana wa ufalme wa Mungu. Mwandishi mmoja kwa jina Dehaut anasema haya " Asili ya ufalme wa Mungu ni kutoka Mbinguni, na huo ufalme hauishii hapa duniani ila unaenda zaidi ya mipaka ya hapa duniani lengo la ufalme wa mbinguni siyo kufurahia furaha za hapa duniani ila lengo lake ni kutufanya sisi viumbe wake Mungu kuwa na uzima usiofifia, au uzima wa milele."Kwetu sisi ili kuwa na uzima wa milele na kuwa wana wa ufalme wa Mungu, yatubidi tuishi maagizo ya Kristu.
Utawala wa Mungu ni wa ulimwengu mzima, na utawala wa Kristu unajikita kwenye upande wa Kiroho zaidi, wakati wa mateso yake Kristu, alivyoulizwa na Pontius Pilate juu ya ufalme wake alijibu kuwa " utawala wangu si wa dunia hii ( John 18:33,36) utawala wa Kristu unapingana na utawala wa Shetani. Ndugu zangu tunapofunga maadhimisho ya mwaka wa imani, basi tunaalikwa kutafakari kwa kina juu ya nini tumefanya juu ya ufalme wa Kristu ndani ya Kipindi chote cha mwaka wa Imani. Je tumeukaribisha ufalme wa Kristu maishani mwetu? Tunavyoadhimisha kilele cha mwaka wa imani tujue kuwa Kristo ndiye mtawala na kielelezo cha maisha yetu, tujue kuwa Kristu ni mfalme wa wote, ni Bwana wa mabwana ( Mat 2:36) utawala wake ni wa milele. Tawala zote zitatikisika na kuanguka lakini yeye utawala wake utabaki umesimama imara milele na Milele.
Tukumbuke kuwa ili tuwe mfano na tuvae sura ya Kristu, sifa kuu iliyomfanya kuwa mfalme wa wafalme, na kumtofautisha na wengine ilikuwa ile fadhila ya utumishi au kuwatumikia wengine bila kuangalia faida, au tusema ufalme wa Kristu ulijikita juu ya kuwa mtumishi wa wote, maana yeye alisema kuwa atakaye kuwa mkubwa kati ya wote ni lazima awe mtumishi wa wote. Ni mwaliko kwetu kuwa tulipo kwenye familia, kazini, mashuleni pamoja na madaraka tuliyopewa kwenye taasisi hizo, tunaitwa kuwa watumishi wa wote bila kuangalia faida, na kufanya hivyo tutakuwa tumevaa sura ya Kristu ambaye alikuwa ni mfalme, lakini mfalme mtumishi ambaye hakupenda kutumikiwa kama tuonavyo kwenye falme za duniani. Kristu na mbali ya Kuwa mfalme wakati wa kifo chake msalabani aliendelea kuwa mtumishi wa wote, mfano unajidhihirisha pale aliposikiliza maombi na dua za yule mwivi aliyekuwa amesulubiwa naye pale msalabani. Hivyo tunaalikwa katika jumapili hii ya Kristu mfalme kuishi maisha ya Kristu na kupingana na vyote ambavyo vinaenda kinyume na mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristu.
0 Response to "MAHUBIRI YA JUMAPILI YA 34 YA MWAKA WA KANISA. SIKUKUU YA KRISTU MFALME.-"
Chapisha Maoni