MAHUBIRI JUMAPILI YA 33 YA MWAKA C WA KANISA.


MASOMO

 1.Mal 3:19-20
 2.2Thes 3:7-12
 3.Lk 21: 5-19

 TAFAKARI: MAISHA YA NJE YA MFUASI WA KRISTU YAFAA YAENDANE NA MOYO WAKE 

Tunapotafakari masomo yetu ya leo tunaambiwa habari juu ya kuharibiwa hekalu kule Yerusalemu ambalo lilichukua miongo kadhaa kulijenga. Tukianzia somo la kwanza tunaona kutoka katika kitabu cha malachi 3:19-20 tunaona inaongelewa hukumu na adhabu ya Mungu juu ya waisraeli, kwa kuwa hekalu lililojengwa kwa ajili ya kumwabudu Mungu sasa limekuwa hekalu la kufanyia biashara, ikiwemo kubadilishia fedha. Tunaona juu ya kuharibiwa kwa Hekalu la Yerusalemu mara ya kwanza mnamo mwaka 587 Kabla ya Kristu, Hekalu hilo lilijengwa na mtawala wa wakati huo ambaye alikuwa ni mfalme Solomon. Hekalu la pili lilijengwa mnamo mwaka 515 Kabla ya Kristu kuzaliwa, japo na mbali ya kujengwa kwa hilo hekalu, kunaibuka matatizo ambapo watu kwa wakati huo ile namna ya kusali na kuabudu inakuwa si ile ya kusali na kumsifu Mungu. Kwa kipindi hicho makuhani walikuwa tena siyo waaminifu juu ya kazi zao, wanaume walijikita katika kuoa wapagani, wengine walianza kutoa taraka kwa wake zao na na mengine mengi ambayo yalilichafua hekalu kwa wakati huo, ni kwa msingi huo nabii Malachi anapaza sauti juu ya hiyo mienendo mibaya ambayo ilikuwa imeingia hekaluni na ambapo makuhani walitumia nafasi zao katika hekalu kutenda maovu, ndipo nabii anatoa onyo kali. Nabii Malach analaumu vikali juu ya mwenendo wa wale waliokuwa wakihusika na hekalu na namna yao ya kusali.

Wajibu wetu kama wakristu ni kuishi na kutenda yale yaliyo halali mbele ya Mungu. hii inajidhihirisha katika Barua ya Mtakatifu paul kwa Wathesolonike ambapo anahimiza kuwa kuwa lazima kila mmoja awajibike kiukweli na kiuhalali bila ya kutumia njia za mkato, kama ilivyokuwa inatokea katika hekalu.

Katika somo la injili tunasikia habari ya Yesu Kristu juu ya kuharibu hekalu. Hekalu ambalo Kristu analiharibu, laonekana kuwa ni jengo zuri ambalo hata mitume wake walikuwa wakilishangaa jinsi lilivyokuwa limepambwa kwa umaarufu wa hali ya juu. Lakini Kristu mwenyewe anasema kuwa jinsi hekalu lilivyopambwa, basi hakuna hata jiwe litakalosalia juu ya jiwe jingine. Maana ya ndani kabisa ni kuwa yesu na mbali ya kutabiri juu ya kuharibiwa kwa hekalu, pia hii ilikuwa ni kumaanisha kuwa mfumo mzima wa kuabudu na kusali wa makuhani kwa wakati ule ulikuwa siyo sahihi, hivyo Kristu kwa kutumia taswira ya kuharibiwa kwa hekalu, pia anamaanisha kuharibu pia mfumo wa kuhabudu na kuleta mfumo mpya ambao ungelivunja matabaka ya Makuhani ambao walitumia jina la hekalu kuficha uozo wao ndani yake. Hekalu linaaharibiwa, na pia mfumo mzima wa kuendesha hekalu, ikiwemo sala, kuabudu vyote vinafikia kikomo kabisa. Kristu mwenyewe aliingia kwenye hilo hekalu, akaondoka, na si kuwa aliondoka, alifukuzwa na wale waliokuwa katika hekalu hilo, kuondoka kwa Yesu katika hekalu kunafanya tena lisiwe hekalu tena, patakatifu pa patakatifu hapaonekani tena. Baada ya hapo hekalu linaonekana kuwa siyo hekalu tena, kwa maana kuwa linakuwa limepoteza umuhimu na maana yake.

"Kuna mtu mmoja alisema kuwa kuanguka na kile ambacho wengi wanakiona ni maarufu ni aibu isiyo kifani"
Hii inamaanisha nini? kuwa umaarufu siyo tija, ila cha maana ni kuwa ni kipi kinamfanya mtu aonekane maarufu kwa nje, ni kheri kuwa na moyo safi wenye subira kuliko kuwa maarufu. hili ndo limepelekea nabii na Yesu kutabiri juu ya kubomolewa kwa hekalu, kwa Kuwa makuhani walitafuta umaarufu kwa kutumia jina la hekalu, na wakasahau kuwa hekalu siyo mahali pa kuchezea kamari na kutafuta umaarufu, ndiyo kwa msingi huu kristu anakuja na mbinu mpya ya kuondoa hekalu lile. Kristu na mbali ya kuondoka katika hekalu, hakuwaacha mitume wake, aliendelea kukaa nao, fundisho ni kwamba ni heri kukaa alipo Kristu na kujifunza kutoka kwake kuliko kukaa asipo Yesu. Kuondoka kwa Yesu hekaluni kunamaanisha pia kuwa kama mwenyewe ambaye ilibidi ahabudiwe hayupo tena hekaluni, inamaana hekalu linakuwa kama jengo lolote lile.

Kwa ujumla na sisi pia katika fundisho hilo, Kila mkristu mbatizwa ni hekalu la Roho mtakatifu, jambo la kujiuliza kuwa ni wangapi wanatumia vyeo au jina la Kanisa kufanya yasiyostahili mbele ya jamii yetu, hasa kwa wakati huu ambapo tunakumbana na changamoto nyingi, kama vile madawa ya kulevya, kuwanyima watoto haki zao za msingi kwa kisingizio cha kuwa na hali duni ya maisha n.k. Mtaalamu na mwandishi mahiri wa vitabu na tamthiliya William shakespear, alisema haya " Vitu vitamu huwa vinageuka kuwa vichungu kufuatana na matendo yake" (  For the sweetest things turn sourest by their deeds) kwamba lile hekalu ambalo lilionekana limepambwa kwa mawe safi, ndani yake lilibeba uozo wa kila aina, hivyo Kristu anachukua jukumu la kusafisha hekalu hilo.


.


Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI JUMAPILI YA 33 YA MWAKA C WA KANISA."

Chapisha Maoni