MAHUBIRI JUMAPILI YA 5 YA PASAKA.


MASOMO: 1. Mat 6: 1-7
                    2. 1Pet 2: 4-9
                    3.Yn 14: 1-12


TAFAKARI: NYUMBANI MWA BABA MNA MAKAO MENGI

Tukianza na tafakari yetu kwanza kabisa hatuna budi kumshukuru Mungu  kwa kuweza kutuvusha hii wiki tuliyoimaliza na tunaanza wiki mpya.  Kutoka  somo la kwanza, Mat 6:1-7 tunaona  ni jinsi gani na namna ilivyowachukua mda mrefu mitume wa Yesu  kutangaza habari njema kwa watu wa mataifa( Wapagani) na hatimaye kuwabatiza. Tunaona Wayahudi ambao walipata kuwa wakristu lakini wako katika makabila mawili tofauti, yaani Wayunani na Wahebrania. Wahebrania: hawa ni wale ambao waliishi huko Palestina na walifanya ibada yao katika sinagogi ambapo Neno la Mungu lilisomwa na kuhubiriwa pia hawa walishika sana mapokeo ya Mababu zao na walishika sana torati ya Musa. Wayunani: hawa walikuwa Wayahudi pia, ila wao walitofautiana na wenzao wa Kiebrania kutokana na sababu kuwa walikulia katika mataifa mengine( Uhamisho wa Babuloni) hivyo walikuwa na mchanganyiko wa mila na tamaduni za hayo mataifa walipokulia. Ni kwa msingi huu wayunani hawakujisikia kufungwa sana na tamaduni za walimu wa sheria za kiyahudi na mapokeo ya kiyahudi. Hawa pia walikuwa hawana uelewa sana  wa lugha ya kiyahudi, waliongea sana Kigiriki. Ni kwa msingi huu tunaona tofauti baina yao zinajitokeza. Tofauti hizo na mtafaruku huu tunauona umekua na kufikia katika kiasi cha kujitokeza katika kugawana mafao/ Mahitaji ya kila siku ya msingi katika jumuiya zao. Wayunani tunaona wanalalamika juu ya mgawanyo wa mahitaji kwa wajane wao ambao walikuwa kwa kiasi fulani wamebaguliwa katika hizo huduma za msingi. Ni kwa msingi huu tunaona  mitume wa Yesu Kristu wanaweka utaratibu wa jinsi ya kugawana na kugawa hizo huduma za msingi kwa usawa, hivyo wanateuliwa watu maalumu ambao wangelifanya hizo kazi( Mashemasi) kwa ajili ya kuhakikisha kuwa usawa unakuwepo. Tunajifunza kuwa watu wa huduma kwa wote bila ubaguzi chini ya mwavuli wa ukabila, utaifa, na udini. Huu ni mwaliko kwetu sote kutoka katika hali ya kukumbatia dhambi na kumvaa Kristu.

Kutoka somo la pili ( 1Pet 2:4-9). Tunaona Peter anatumia mfano wa kulinganisha Kanisa na Jengo. Hapa mjenzi ni Mungu na mawe ya kujengea in sisi waumini ambao tu mawe hai. Tunaambiwa juu ya jiwe la msingi basi hili jiwe ndo Kristu mwenyewe ambaye amefufuka kati yetu. Kufufuka kwa Kristu kumeimarisha imani yetu na kuzaliwa kwa Kanisa, hivyo imani yetu juu ya Kristu ambaye ni Jiwe la msingi  inatufanya tuwe mawe hai juu ya huo msingi.

Kutoka katika somo la Injili( Yn 14: 1-12) Tunakumbushwa maneno ya Yesu wakati wa ile karamu kuu. Maneno ya Injili hii ni Wosia wa Kristu kabla ya mateso na kifo chake. Swali la kujiuliza ni kuwa kwa nini Liturjia inatuletea maneno hayo ya Injili ( Wosia wa Yesu) baada ya Pasaka? jibu ni kwa sababu wosia husomwa baadaa ya kifo cha yule aliyetoa huo wosia. Tupate hayo maneno na maana yake. " Ninakwenda  kuwaandalia mahali" ( Jn 14:2-4), " Yesu anaongelea pia njia, nami niendako mwaijua njia", Hapa tuelewe kuwa njia iongelewayo na Yesu ya maanisha juu ya mtu kujitolea kwa wengine, kuutoa uhai wake kwa ajili ya wengine kama yeye mwenyewe alivyofanya. " Nyumbani kwa Baba" Hii inamaanisha Jumuiya ya wakristu. " Nyumbani kwa Baba kuna makao mengi" Hii sentensi ambayo ndo kiini cha tafakari yetu ina maana kuwa katika kuwatumikia watu, katika kuwahudumia watu wa Mungu, tunaona kuwa kuna mambo mengi  na huduma nyingi za kufanya kuwahudumia watu. Watu katika maisha wanakumbana na changamoto za kila aina( Vyumba vingi/ Makao mengi). Ni kwa msingi huu tanaalikwa kutumia vipaji vyetu, na karama zetu za namna mbalimbali katika kuwahudumia na kuwasaidia watu wahitaji. Hivyo kama nyumbani mwa Baba kuna majukumu mengi ya kufanya tunaalikwa tusiwe watu wa vinyongo, wivu, na tamaa juu ya yafanywayo na wengine kutokana na karama na vipaji vyao. Kwa kuwa kila mmoja kwa namna ya pekee amepewa karama na kipachi cha aina yake, karama hizo na vipaji hivyo vikitumiwa vitakuwa vimewasaidia wale wenye uhitaji wa hivyo vipaji na karama.

Katika maisha watu huthaminiwa kufuatana na hali zao za kimaisha, mfano watu huthaminiwa sana kufuatana na vyeo vyao, utajiri walionao n.k, kwa Yesu Kristu hayo yote ni batili. Nafasi kwa Kristu, yaani makazi mengi kwa Baba, ni ile hali ya kujitolea( utumishi) kwa wengine bila kuangalia malipo.Kristu hapa anatualika tuwe tayari kwa ajili ya kuwatumikia wengine, na ikibidi tutoe uhai wetu kwa ajili yao.

Tukiamini kazi azifanyazo Kristu tunakuwa tumemwona Mungu Baba kwa kuwa Kristu ni ufunuo wa Mungu.Kutokana na Ushuhudawa yale ayafanyayo tuanaalikwa kuamini kuwa Kristu ni ufunuo kamili wa Mungu. Tusifanane na filipo aliyetaka amwone Mungu. Yesu ni njia, ukweli na uzima.

Related Posts:

3 Responses to "MAHUBIRI JUMAPILI YA 5 YA PASAKA."

  1. Asante sana father. Mahubiri yako nimeyapenda na nitakuwa najitahidi kufuatilia mara kwa mara. Hongera sana kwa kukigundua chumba (makao) yako na kuyamiliki. Hapa nimejifunza nijitahidi kufurahiwa na vipaji vya wengine kuliko kukwazika, hasa kama kazini kwa mfano, isionekane kipaji cha fulani ni kikwazo kwangu, nk. Asante sana naendelea kutafakari

    JibuFuta
  2. Asante sana kwa maoni yako mazuri juu ya chapisho langu la tafakari ya juma la tano la pasaka@ Mkatoliki Leo.

    JibuFuta
  3. Naashukuru Sana, ninefarijika kwa neno naomba nafasi ya kulewa mahubiri Karina domonika hizi ambazo bado rupo katika kupambana na Corona sababu mahudhurio yangu ya kuhudhuria Misa no machache mno

    JibuFuta