MAHUBIRI JUMAPILI YA 3 YA MWAKA B WA KANISA


1.Yona 3: 1-5,10
2.1Kor7: 29-31
Mk 1:14-20

TAFAKARI “ Kila mmoja wetu anachakumtolea Mungu”
Moja ya watu maarufu hapa duniani ambao kamwe hawatoweza kusaulika ni mwanamke aliyeitwa Prince Diana. Diana alianza safari na mbio zake kupenda na kutaka kutwaa taji la umalkia wa nchi ya uingereza kwa juhudi na nguvu zake zote. Lakini mbio zake ziliishia kwa yeye kuitwa “ Malkia wa mioyo.” Katika hali ya kupoteza cheo ambacho Diana alikuwa anatarajia, yaani kuwa Malkia wa uingereza baada ya kutofanikiwa kupata cheo hicho, kumbe yawezekana ilisikika sauti ya Mungu ndani mwake ikimwambia “nifuateni mimi name nitakufanya uwe Malkia wa mioyo.” Diana kwa kusikia sauti ya Mungu aliyaacha yote aliyotaka kufanya kama malkia na kumfuata Mungu kwa kutoa kwa watu waliosahulika katika jamii, watu maskini, watu waliotelekezwa na kutupwa pembezeoni mwa jamii n.k.
Ndani ya muda mfupi Diana aliweza kuvuna roho za watu hasa wale watu waliokuwa wakiteseka kwa sababu nyingi ikiwemo kunyimwa haki zao.
Katika masomo yetu ya leo, hasa kutoka somo la Injili tunaona Kristu akiwaita wale ambao wangelikuwa wanafunzi wake hapo baadaye, yaani Simoni, na Andrea wamfuate na kuwa naye maisha yao yote, yaani wabadilishe nia na malengo yao katika maisha ili wapate kuwa wafuasi wazuri wa Bwana wetu Yesus Kristu. Ikumbukwe kuwa hawa walioitwa kumfuata Kristu kazi yao kuu ilikuwa ni uvuvi wa samaki, lakini Kristu anawaita wawe wavuvi wara roho za watu. Swali moja ambalo ni changamoto kwetu, na pia swala la msingi  ni kuwa “ Kama Kristu anawaita na kuwaambia waache yale waliyokuwa wakiyafanya , mfano, kuvua samaki, kitu kinachoashiria kuwa ndo ilikuwa ajira yao na riziki yao, je Yesu alipowaita angelifanyaje ili kuhakikisha kuwa hawa ndugu wanaendelea na ujira wao na riziki zao za kila siku walizokuwa wanapata?? Jambo la msingi kuelewa ni kwamba kile kitu tukifanyacho kila siku basi tukibadilishe na kifanyike kwa ya ufalme na utukufu wa Mungu. Mfano  Simoni na Andrea mbali ya kuitwa na Kristo wamtumikie yawezekana waliendelea na kazi yao ya uvuvi na kuifanya hiyo kazi iwe ni kwa manufaa yaw engine na siyo wao wenyewe.
“Nifuate na nitawafanya wavuvi wa watu.”( Mk 1:17). Waliacha nyavu zao wakamfuata Kristu. Nyavu hizo ni zipi? Yawezekana zile nyavu ni ile mienendo yao ya zamani,ikiwemo misimamo watu walioshikilia kimaisha.Tunaambiwa kuwa ukiamini utaona kazi utakayo ifanya maishani. Hawa ndugu walikuwa na taswira ya kuona samaki maishani mwao, ila Mungu anataka awaonyeshe picha ya watu, kwamba wawe na mtazamo fulani wa kuangalia maisha na siyo kukaa na mtazamo wa namna fulani ambao hauwezi jenga wala leta maendeleo. Katika Biblia bahari au ziwa ni ishara ya nguvu za uovu, hivyo kuwavua watu maana yake ni kuwaepusha na kuwatoa katika minyororo ya uovu.
Mungu atuitapo tumtumikie mara nyingine huwa tunajikuta anatuita tukamtumikie mahali pale ambapo mazingira yake kwanza ni magumu, mahali pale ambapo roho saa nyingine hazipendi kwenda. Diana hakutarajia  kwenda kuhudumia watu wa machimboni, kuhudumia waathirika wa ukimwi, ila kwa mpango na mapenzi ya Mungu alijikuta akifanya hivyo. Mwito wa kwanza kwa Yona ilikuwa ni kwenda Ninawi. Kwa wayahudi wa kizazi cha karne ya kwanza, Ninawi ilikuwa ni kitovu cha maovu ya aina nyingi mfano, utovu wa maadili, rushwa, wizi, n.k. Ninawi ilikuwa ni kitovu cha himaya  ya Siria ambayo ilivamia na kutawala Yuda ambapo tunaona kuwa hekalu lililokuwa limejengwa katika falme ya Yuda liliharibiwa vibaya na utawala wa Kisiria, na hivyo kuwachukua  watu wa Yuda na mali zao uhamishoni mbali na nchi yao.  Ninawi kwa hali hiyo ilikuwa ni makao makuu na kitovu cha nchi ya siria ambapo tabaka ya wale wenye mali na hela vilitawala na kupewa kipau mbele dhidi ya wale ambao hawakuwanacho. Utovu wa maadili , uzinzi, wizi, rushwa hivyo vilikuwa wimbo wa kila siku ambao haukukosa mpiga zumari. Ni kwa msingi huu kwa myahudi mwenye moyo myoofu na mtiifu kwa Mungu, Yoha, Ninawi kwake ilionekana kama mji uliokuwa tayari umelaaniwa na Mungu, kwake Yona huo mji ulionekana kama mji uliojaa maovu ya kila aina. Basi ni kwa msingi huuYona anavyotumwa na Mungu kwenda Ninawi anapata wasiwasi na anaona ni vigumu kwenda huko.
Jambo la kuleta matumaini na faraja ni kwamba pindi Yona anapoenda kuwahubiria watu wa Ninawi wanasikia neno la Mungu na kubadilika, wakafanya toba na kuamini neno la Mungu walilohubiriwa na hivyo walimrudia Mungu wao.
Hivyo na leo hii Mungu bado anawatafuta wanaume kwa wanawake  kwenda Ninawi kuhubiri Neno lake. Swali la kujiuliza  ni kuwa “ Ninawi yetu kwa sasa iko wapi, na ni kina nani wako hiyo Ninawi yapasa wahubiriwe ili wabadilike”? Jibu ni kwamba Ninawi ya sasa tunaikuta mahala pengi mno. Mfano mahali pale ambapo watu wanadhulumiwa haki zao za msingi, kama chakula, malazi n.k, rushwa inakithiri, ufisadi, unyanganyi wa kutumia silaha za moto, na silaha za asilia, Siasa zinazolenga kuwashibisha wale wenye meno makali yenye uwezo wa kutafuna hata kuliko wale wasio na meno makali wakiwemo vibogoyo ( Escrow, Richmond, IPTL), Ninawi yetu pia iko katika ile mitaa inayosadiki na kukubali ndoa za jinsia moja, Ninawi pia ipo pale tunapokuta watoto wananyimwa haki zao za msingi kuzaliwa kama watu wengine ( utoaji mimba), Ninawi tunaikuta pia kwenye jamii iliyogubikwa na matabaka, ukabila, udini na urangi. Neno la Mungu leo linatualika kupenya hayo magumu na hatimaye kufikisha ujumbe wa Mungu.
Mungu anamwita kila mmoja wetu  katika ufalme wake pindi akifuata sharti la kutubu, na kuamini ( kuwa na imani) ili kuweza kuurithi ufalme wa mbinguni. Mungu anavyotuita tufanye kazi yake anatuita pamoja na mapungufu yetu na hili limedhihirishwa na  pale Simoni na Andrea walipoitwa na Yesu wawe mitume wake.  Kimsingi hawa walikuwa ni watu wa kawaida ambapo inaeleweka kuwa kazi yao ilikuwa ni kuvua samaki, ila sasa Kristu anawaita watumie utaalamu wao wa kuvua samaki  kuwavua watu.
Hivyo Kristu anavyotuita tumtumikie tusijibakize nyuma  kwa kusema kuwa hatuna la kumtolea. Kristu huwa anawaita watu wa kawaida kama sisi wote tulivyo ili waweze kumtumikia. Chochote ulichonacho ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu na ni mwaliko kukitumia.

Tunavyoadhimisha jumapili ya 3 ya mwaka B wa Kanisa ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kutupilia mbali utu wake wa kale, maisha ya starehe, na anasa za dunia vitumike kama nyenzo kwa ajili ya kuufikia ufalme wa Mungu. Tunaalikwa kutega masikio na mioyo yetu kusikiliza sauti ya Mungu inatuambia tufanye nini, lini na wapi.

Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI JUMAPILI YA 3 YA MWAKA B WA KANISA"

Chapisha Maoni