1.Mat1:1-11
|
2.Ef4:1-13
|
3.Mk16:15-20
|
TAFAKARI “ Yesu
hamilikiwi na baadhi ya watu ila ni wa ulimwengu wote”
Jumapili ya leo
tunaadhimisha sherehe ya kupaa kwa Bwana wetu Yesu Kristo mfufuka. Watu wengi wamekuwa
na mawazo kwamba Kristu kupaa kwa Kristu kulikuwa ni kupotea mawinguni au
hewani kwa sababu ya nguvu za kimungu alizofufuka nazo. Mawazo kama hayo huwa
yanawapoteza wengi na hatimaye kuwafanya wasielewe mafundisho juu ya fumbo la
kupaa kwa Bwana. Kristu kwa kupaa anamaanisha kuwa bado yupo na sisi kwa namna
ya pekee.
Sikukuu ya kupaa kwa
Kristo inamaanisha kuwa sasa Kristu hafungwi kwenye sehemu, kabila, au tabaka
bali yeye sasa ni wa ulimwengu mzima. Kristu kupaa kwake anatufunulia kuwa anapatikana,
katika viumbe vyote na duniani kote. Kupaa kwa Kristu Yesu hakumaanishi kuwa
Kristu sasa hayupo nasi tena, bali ni kusheherekea Kristo kuwa pamoja nasi hadi
ukamilifu wa dahali. Kristu yupo sasa katika jumuiya zetu, makazini mwetu,
makanisani mwetu na kwa wale wote tunaokutana nao, hivyo ni jukumu letu
kumfanya huyo Kristu aonekane pia kwa wale ambao bado hawajatambua uwepo wake
katika maisha yao.
Mwinjili Marko katika
injili yake hakuwa amejumuisha kipengele Mk 16:9-20 hivyo inaonekana kuwa ni
kipengele kilichoongezewa baadaye katika hii injili kikiwa na maana yake na
ujumbe mahususi kwetu sote. Kipengele hiki kilipata kuongezewa katika Injili ya
Mtakatifu Marko ili kufanya fumbo la kupaa kwa Bwana lipewe umuhimu na nafasi
zaidi katika imani ya waumini juu ya fumbo la ufufuko wa Bwana wetu Yesu
Kristu. Wataalamu wa maandiko matakatifu waliweza kuongezea hicho kipengele ili
kudhihirisha kuwa Kristu bado yupo kati yetu na kazi yake ya ukombozi
inaendelea duniani kote.
Sherehe ya kupaa kwa
Bwana inatukumbusha wajibu wetu wa
kuendelea kumhubiri na kumtangaza Kristu katika wale ambao hawajaonja upendo
wake duniani kote. Kila mmoja wetu anaalikwa kuwa chombo cha utangazaji wa huyo
Kristu aliyepaa kwa wote walio na kiu ya kumwona huyo Kristu katika maisha yetu
ya kama wakristu wabatizwa.
Tunaalikwa kutambua
kuwa Kristu yupo kwa viumbe vyote ulimwenguni tukianzia watu wanyonge katika
jamii, kama vile maskini, wafungwa ( Mt25:34-46). Tutambue kuwa Kristu yupo kwa
kila kiumbe hapa duniani. Mwaliko wa kutunza na kuhifadhi mazingira, raslimali
za dunia ni mwito kwetu wakristu kupaza na kuinua sauti zetu dhidi ya wale
wanaoharibu mazingira, japo hizo sauti kwa namna moja au nyingine huwa
zinajaribu kuzimwa na watawala wenye uchu na kiu ya kupora hizo raslimali
asilia. Sauti ya Kinabii inaenda mbele hata kwenye mifumo ya kisiasa isiyokidhi
mahitaji ya binadamu, sauti ya kinabii inaenda pia zaidi kwenye mifumo ya
kitabibu isiyo kidhi utu wa mwanadamu na baadala yake inaharibu utu wa mtu,
mfano, utoaji mimba, kifo cha kujitakia, watoto wanazalishwa kwenye mifuko (
Test tube babies), Ni mazingira hayo tunamkuta Kristu. Sauti ya Kinabii ya
Kanisa japo huwa mara nyingi inazimwa pia inajikita katika kutetea usawa juu ya
mgawanyo wa madaraka na mifumo ya kiuchumi inayobagua walio nacho na wasio
nacho katika mataifa mbalimbali ya dunia. Kristu ataendelea kuwepo katika
maisha yetu pindi sisi kama wakristu tutakuwa katika nafasi ya kupaza sauti
zetu katika mifumo ya Kijamii, Kisiasa, na Kiutamadauni ambazo kwa namna moja
huwa zinakiuka maadili na utu wa mwanadamu. Hivyo ni mwaliko kwa kila mmoja
wetu kutambua wajibu wake wa kumhubiri na kumtambua Kristu katika mifumo
kandamizi isiyotambua utu wa mwanadamu katika jamii yetu tunayoishi.
0 Response to "MAHUBIRI JUMAPILI YA KUPAA KWA BWANA MWAKA B"
Chapisha Maoni