MAHUBIRI JUMAPILI YA 4 YA MAJILIO MWAKA B




1.2Sam7:1-5,8b-12,14a, 16
2.Rom 16:25-27
3.Lk 1:26-38

Tafakari “ Kristu fumbo la wokovu wetu.”
Tunavyoadhimisha jumapili ya 4 ya majilio na tunavyojiandaa Kristu azaliwe upya katika maisha yetu tunaalikwa sote kutafakari juu ya Kristu anayezaliwa kama fumbo la wokovu wetu sote.
Kuna mtu mmoja aliyeitwa William Phelps huyu alikuwa ni mwalimu na mtaalamu sana wa lugha ya Kiingereza miaka ya 1900. Siku moja akiwa anasahihisha mitihani ya wanafunzi wake siku chache kabla ya siku ya Krismasi, katika moja ya karatasi ya majibu ya wanafunzi wake alikuta jibu la swali alilouliza limejibiwa “ Mungu mwenyewe ndo anajua jibu la swali ulilouliza, Heri ya Krismasi” na pia mwalimu alimrudishia majibu mwanafunzi aliyejibu namna hiyo akiwa amemwandikia “ Mungu ajuaye ndiye amepata alama A” na wewe usiyejua alama yako ni F, maana yake Fail au kushindwa”. Katika jumapili hii ya mwisho kabla ya Krismasi somo la pili kutoka barua ya mtume Paulo  kwa warumi tumesikia Paulo akigusia juu ya fumbo la Kristu yesu ambalo linajulikana na kufahamika kwa Mungu tangu mwanzo, lakini kwa sasa fumbo hili limedhihirishwa kwa vizazi vyote  katika Kristu.
Mji wa Roma kwa kipindi paul anaawandikia warumi ulionekana kama sehemu muhimu na kitovu cha dunia nzima, hivyo ni kwa msingi huu mji wa Roma ulieleweka kama mwisho wa dunia. Hivyo wakristu wa hapo awali walifahamu tosha kuwa kama injili ya Kristu iliweza kufika Roma basi ilikuwa imefika dunia nzima. Ni kwa msingi huu pia tunamsikia paul katika barua yake kwa warumi,Rum 10:18 anauliza swali “ Lakini nauliza je hawakuwasikia? Sivyo! Wamewasikia: “ uvumi wao umeenea duniani kote, na maneno yao yanasikika hata mikapa ya dunia.”
Mitume wa Yesu Kristu kwa kutofahamu Kristu mwenyewe ambaye ndiye alikuwa fumbo walimwomba awaongezee imani, Lk 17:5 “ Bwana tuongezee imani” mbali ya mitume wake kristu kukaa naye miaka mitatu katika utume wao bado hawakuelewa vizuri juu ya hili fumbo, yaani fumbo la umwilisho wa Kristu. Peter ndiye anakuja kufumbuka akili na kulijua hilo fumbo baada ya muda mrefu baada ya kupata ufunuo kutoka kwa Mungu Peter alipata kutambua na kujua siri ya hilo fumbo. Kutoka katika maandiko matakatifu tunapata kusikia kuwa “ kwa maana sheria imetolewa kwa njia ya Musa, lakini neema na kweli zimepatikana kwa Yesu Kristo.”( Yohane 1:17). Hivyo Paulo anatuambia juu ya utii wa imani ( Rum 16:26). Ni kwa msingi huu Paulo anabainisha kuwa wokovu ni kwa kila mmoja wetu, na sharti ni kuwa na imani ya utii, sheria ya Musa haina nguvu tena kwa kuwa Kristu amezaliwa na kufa kwa ajili yetu. Hivyo tunaambiwa kuwa siyo matendo yetu tu yatatuletea wokovu, bali pia hayo matendo yaendane na imani yetu katika Kristu.
Kutoka katika somo la injili tunajifunza unyenyekevu wa Bikira Maria katika kuukubali mpango wa Mungu. Ni mwaliko kwetu sote kuyakubali mapenzi ya Bwana kama vile Bikira Maria alivyonyekea kuyakubali mapenzi ya Bwana kupitia kwa Malaika. Mara nyingi sana mipango yetu tuipangayo siyo mipango ya Mungu, sisi tunapanga hili na lile lakini Mungu anampango mwingine na sisi, yatubidi tujifunze kutoka kwa Bikira Maria. Tunaalikwa kuwa wasikivu wa Neno la Mungu kupitia maandiko matakatifu. Maria anasema “ nitendewe ulivyonena” hili jambo la kututafakarisha tuanavyojiandaa na Kipindi cha Krismas kuwa tukiulizwa swali hilo tupo tayari kujibu vile alivyojibu Maria? “ Nitendewe ulivyonena.” Kujiweka mikononi mwa Mungu maana yake ni kuweka yale yote pembeni ambayo yanatutenga na upendo wake, kuwaweka pembeni marafiki wabaya, kuacha ulevi, wivu, uzembe, wizi, uzinzi n.k.
Mungu kwa kumteua Bikira Maria kufanya mapenzi yake, pia ametuteua sisi, kwa kukubali kwa Bikira Maria katika kutimiza mapenzi ya Mungu sote tumepata wokovu.
Tunaona pia kutoka somo la kwanza kutoka katika kitabu cha pili cha Samuel, Daudi anataka kumjengea Mungu hekalu, lakini Mungu kupitia kwa nabii nathani anamwambia Daudi kuwa yeye hana haja na hilo hekalu. Tunajifunza kuwa sisi hatumpi Mungu, ila Mungu huwa ndiye ajuaye shida zetu sisi wahitaji. Hapo Mungu ndiye afanyaye jambo kwa mtumishi Daudi hasa katika uzao wake. Hivyo ilikuwa ni mwito kwa Daudi kuachilia mbali mipango yake na kumkaribisha neema ya Mungu katika maisha yake. Kuwakaribisha wengine katika maisha yetu na kuwapokea jinsi walivyo ni jambo jema na lakupendeza katika maisha yetu kama wakristu.

Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI JUMAPILI YA 4 YA MAJILIO MWAKA B"

Chapisha Maoni