MAHUBIRI JUMAPILI YA 2 YA MAJILIO MWAKA B




MASOMO
     11.Isaya 40:1-5, 9-11
2.Peter3:8-14
3.Marko1:1-8

TAFAKARI “  Mungu awe nasi daima katika maisha yetu
Katika shule fulani, ilitokea kwamba mmoja wa walimu wa shule hiyo hakuhudhulia kazi, hivyo ilimbidi mkuu wa shule achukue hatua ya kumtafuta huyo mwalimu kujua kulikoni hajafika shule kama kawaida.  Hivyo mkuu wa shule alienda nyumbani kwa yule mwalimu ili apate kujua ninini kilimsibu hadi hasionekane shuleni. Mkuu wa shule alipofika nyumbani kwa huyo mwalimu alikutana na mtoto mdogo aliyekuwa akipiga mruzi, na hivyo yule mkuu wa shule alipata kuhojiana na yule mtoto kama ifuatavyo: Baba yako yupo nyumbani? Mkuu wa shule aliuliza, mtoto alijibu, Ndiyo. Naweza nikaongea naye? Mkuu wa shule aliuliza, hapana, mtoto alijibu, Mama yako yupo, mwalimu aliuliza, mtoto alijibu, ndiyo, naweza nikaongea naye? Mkuu wa shule aliuliza, mtoto pia alijibu hapana huwezi ongea naye. Kuna mtu mwingine yeyote hapa? Mkuu wa shule aliuliza, mtoto alijibu ndiyo, mkuu wa shule aliuliza huyo ninani? Mtoto alijibu “ ni police” naweza kuongea naye? Mkuu wa shule aliuliza, mtoto pia alijibu huwezi kuongea naye maana anashughuli nyingi sana, yupo anaongea na mama, baba, na askari wa kikundi cha wazima moto, mkuu wa shule alivyosikia pia juu ya kuwepo askari zimamoto aliuliza kwa mshangao kuwa, “ Ina maana nyumba iliungua? Mtoto alijibu hapana. Na mkuu wa shule akauliza tena sasa hawa askari police na zima moto wanatafuta nini hapa? Mtoto kwa sauti ya upole alijibu “ wananitafuta mimi”
Hivyo ni vigumu kwa police na waokoaji kumpata huyu mtoto pindi akiendelea kunyamaza bila ya kusema alipo. Katika injili ya leo, jumapili ya pili ya majilio tunaona Yohane mbatizaji nyikani akipaaza sauti nyikani kuwaita watu wa Yuda kuja kutoka walipojificha ili waweze kusikia sauti ya Mungu iliayo nyikani.
Kuingia na kukaa nyikani maana yake, ni kuacha yale maisha ambayo yanamtenga mkristu na upendo wa Mungu, yaani kuacha maisha dunia ikiwemo anasa na starehe ambavyo ndo vikwazo vinavyomfanya mtu asiwe karibu na Mungu. Ni mwaliko kuwa kama wakristu hatuwezi kuwa karibu na Mungu pindi tukiweka roho zetu na akili zetu katika mambo ya dunia. Kama moyo umejaa ina maana Mungu hana nafasi kamwe ya kuingia katika moyo uliojaa mambo ya dunia. Ili Mungu aingie mioyoni mwetu lazima mioyo ifunguke. Fadhila ya utii na unyenyekevu itawale mioyo yetu ndo hapo tutaweza kuisikia sauti ya Mungu. 
Katika maandiko matakatifu, jangwa linamaanisha ile sehemu ya kukutana na kuongea na Mungu. Ilikuwa ni jangwani ambapo tunaona kuwa watu waliweza kukutana na kuongea na Mungu. Ili kukutana na Mungu watu hao waliachana na maisha dunia, na waliona kuwa maisha dunia kilikuwa siyo kitu cha kushikamana nacho kwa nguvu, hili limedhihirishwa na maandiko matakatifu, Hes 11:5 “ Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure, na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu
Kristu kabla ya kuanza utume wake ilimchukua siku  arobaini  usiku na mchana jangwani akifunga. Ulikuwa ni muda kwake wa kutafakari na kuwa karibu na Mungu. Yohane  kwa kupaza sauti na kuwaita watu ilikuwa ni kuwafanya waache yale yote yaliyokuwa yakiwatenganisha na Mungu na hivyo kuwafanya wawe karibu na Mungu. Yohane mbatizaji maisha yake yanaonyesha kuwa aliishi kile alichokihubiri kwa watu. Yeye alihubiri ujumbe wa toba. Kwa jinsi hiyo maisha yake yalibadirika, namna yake ya kuvaa, kula na mengine mengi yalibadilika ikiwa ni kielelezo kuwa maana ya maisha haimaanishi kuwa na mali nyingi na kutegemea raslimali dunia. Kila mmoja hapa duniani ana maficho( madhaifu) ambapo hayo maficho hufanya uhusiano na Mungu usiwe mzuri. Kwa kukubali kurekebisha hayo madhaifu ni kuwa mlango unakuwa umefunguliwa ili Mungu abishe hodi maishani mwetu.
“Wito wa injili ya Marko ni “ itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake” ( Marko 1:3). Kunyosha mapito ni kufukia mabonde ya vilema ( madhaifu) na kushusha milima ya kuzidisha fadhila kupindukia ili tuwe na tambarare ya fadhila. Hivyo tunavyojiandaa kwa Krismas tuna jiandaa kukutana na njia. Yesu Kristu mwenyewe ni njia.Katika kukutana na njia tunaalikwa wote kuwa na fadhila ya ukarimu. Fadhila ya ukarimu inasimama katikati ya kukusanya na kutapanya hovyo Krismasi tunayoingojea siyo kipindi cha kutapanya hovyo, bali ni kipindi cha kushirikishana yale yote tuliyojaliwa na mwenyezi Mungu”( Rev. Fr. Kamugisha).
Tunapoadhimisha dominika ya 2 ya Majilio tujiulize kuwa ni mabonde mangapi ambayo yapo maishani mwetu na bado yanahitaji kusawazishwa ( Mapungufu yetu) kama vile, ulafi, uchoyo, uwongo, uzinzi, wivu, wizi, n.k
Fadhila ya subira katika maisha yetu itawale daima. Kukosa subira ndiyo kiini cha kuwafanya watu wengi wajikute katika dhambi ndogo na dhambi ya mauti. Kukosa subira ni bonde. Subira ni tambarale. Ni jambo wazi la kujiuliza kuwa ni kwa kiasi gani na jinsi gani tumekuwa watu wa subira katika safari ya imani? Je mambo yasipofanikiwa kadiri ya malengo na matarajio yetu huwa tunafanyaje? Hivyo tunapoadhimisha jumapili ya pili ya majilio tunaalikwa na tunakumbushwa daima kuishi fadhila za Kikristu, yaani subira, ukarimu, unyenyekevu na ujasiri. Hayati Nelson Mandela alipata kunena kuwa “Nimejifunza maishani kwamba ujasiri maana yake si ukosefu wa woga, bali ni ushindi dhidi ya woga, na kwamba shujaa si yule ambaye hana woga bali ni yule anayeushinda woga.”( Rev Fr. Kamugisha)

Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI JUMAPILI YA 2 YA MAJILIO MWAKA B"

Chapisha Maoni