MASOMO
1.
Isaya 45:1. 4-6
2.
1Thes 1:1-5b
3.
Mt 22: 15-21
TAFAKARI “ Tusichanganye Serikali na Mungu”
Tunavyoadhimisha jumapili ya 29 Ya mwaka wa
Kanisa, tunaalikwa kutafakari kwa kiundani juu ya nini tumepewa na Mungu na
tunarudisha kwa Mungu. Pia katika jumapili hii tunaalikwa pia kujiuliza hili
swali kuwa tunatoa nini katika serikali zetu.
Tunaona waandishi na Mafarisayo wanatoa swali
lenye utata kwa Yesu juu ya kulipa Kodi kwa Kaisari au kutolipa kodi kwa
kaisari, hivi na sisi tujiulize kuwa hili swali lilikuwa linamadhumuni gani na
lilikuwa lina lenga nini hasa kwa Yesu? Na hili swali pia kwa maisha yetu na
wakati wetu lina maana gani?
Tukianza kabisa kuchambua swali ambalo Yesu
aliulizwa twaweza tambua maramoja kuwa kumbe hili lilikuwa ni swali tata na pia
swali mtego kwa Yesu, tujiulize pia kuwa lilikuwaje swali tata na lenye mtego
kwa Yesu? Jibu ni kwamba swali aliloulizwa Yesu lilikuwa tata kwa kuwa majibu
ambayo angeliyatoa ndo yangelimwingiza kwenye matatizo makubwa ambayo
yasingelitarajiwa. Lilikuwa ni swali mtego kwa sababu, kama Yesu alivyoulizwa
na hao mafarisayo juu ya kulipa Kodi au kutolipa Kodi kwa Kaisari, Yesu
angelitoa jibu la ni halali kulipa kodi kwa Kaisari ina maana kwamba ingelionekana
kuwa alidharau dini ya wayahudi na pia kuzarau taifa lao na hivyo kukumbatia
utawala wa kikoloni wa warumi, hivyo machoni pao ingelionekana kuwa
amewadharau, pia kama angelijibu hilo swali kuwa ilikuwa siyo halali kwao
kulipa kodi kwa Kaisari, hii maana yake ingelionesha kuwa Yesu alidharau mamlaka
na Serikali ya Kirumi, na ni kwa msingi huo hao wafarisayo wangelipata nafasi
ya kumshitaki kwa hayo mamlaka kwa kuonyesha dharau ya kutoheshimu hayo
mamlaka. Ni Kwa msingi huu tunaona Yesu Kwa hekima yake anawajibu kuwa “mpe
Kaisari yaliyo ya Kaisari na pia mpe Mungu yaliyo yake Mungu” ( Mt 22:21)
Hii inamaanisha nini? Maana nyingi sana
zimetafsiriwa juu ya haya maandiko, na ni kwa msingi huu kuwa wengi hasa
viongozi wa serikali hualalisha yasiyoweza kuhalalishwa kwa kifungu hiki kidogo
cha maandiko matakatifu, mfano utasikia wengine wanasema kuwa dini isiingilie
serikali, na pia dini nayo inasema serikali isiingilie dini kamwe. Ni kwa
msingi huu tunaona kuwa dini inaweza kutumika kama mvuli wa kutenda maovu, kwa
kisingizio kuwa serikali isiingilie dini, na vilevile serikali inaweza kutumia
mumvuli wa kutenda maovu dhidi ya wananchi wake na kushutumu viongozi wa dini
wasikemee maovu ya viongozi wa serikali kwa kubainisha kuwa dini haina la
kusema juu ya serikali
Kristo anavyosema kuwa “ mpeni Kaisari
yaliyoyake Kaisari, na Mungu yaliyoyake Mungu anamaanisha kuwa kama vya Kaisari
( Mamlaka/ Serikali) vinatumika kwa ajili ya manufaa ya pamoja ( Common good)
na kwa ajili ya maendeleo yetu, basi itakuwa siyo halali kutumia hivyo vya
kaisari bila ya kuwajibika kuvilipia kodi, na pia ni mwaliko kwa wakristo
kuheshimu madaraka na mamlaka ya tawala hapa duniani, kwa maana kama Kristo
mwenyewe aliheshimu hayo mamlaka kwetu inakuwaje? Hakuna sababu ya msingi
ambayo inaweza kuhalalishwa na dini kuharibu au kuiba mali ya Serikali kwa
kisingizio kuwa dini na serikali haviingiliani. Ni mwaliko na ni wajibu wa kila
mmoja wetu kuhakikisha kuwa mshikamano na ushirikiano upo katika kujenga tawala
na serikali zetu. Jibu la Yesu kwa wafarisayo linatoa ushuhuda kuwa nayeye
anatambua umuhimu wa mamlaka na utawala wake. Kila kitu tulichonacho kinatoka
kwa Mungu hivyo hatuna budi kutii hayo mamlaka.
Tunaona kwamba Yesu anapotoa jibu kwa
mafarisayo kwa kuwauliza juu ya picha iliyochorwa juu ya hela wanajibu kuwa ni
picha na sura ya Kaizari. Sisi vilevile kama wana wa Mungu tumeumbwa kwa sura
na mfano wa Mungu ( Mwanzo 1:27) hivyo kama Kristo anasema kuwa “ Kaisari
arudishiwe vilivyovyake, na Mungu apewe vilivyovyake” tunapata somo juu ya Kuheshimu
mamlaka na pia kumrudishia Mungu kile alichokiumba kwetu kikiwa na sura
yake. Tunaalikwa kuheshimu utu wa
binadamu, hasa kuheshimu wale wote ambao katika jamii hawana wa kuwatetea, hasa
watoto yatima, kuepukana na unyanyasaji hasa kwa wakina mama wajane,maskini wasiojiweza, na
pia kuheshimu sura ya nchi na uasili wake. Tukifanya vile ni kuwa tutakuwa
tunamrudishia Mungu na kumshukuru kwa yale yote aliyotukirimia kama watoto
wake.
Tunavyomrudishia
Mungu aliyotukirimia pia inabidi tumshukuru, Mhubiri mmoja alipata kutoa mfano
wa kushukuru, naye si mwingine bali ni Fr. Faustine Kamugisha na alikuwa na
haya “ Siku ya Kushukuru iliyvokuwa
imekaribia wanafunzi wa darasa la awali- Chekechea waliambiwa kuchora picha ya
kitu ambacho katika maisha yao kiliwasaidia sana na hivyo wamshukuru Mungu kwa
kitu hicho, baadhi ya wanafunzi walichora gari, ndege, chakula, kinyago n.k,
lakini mtoto mmoja alichora mkono. Wanafunzi wenzake walianza kujiuliza ni
mkono wa nani?, wa Mungu? Mkono wa Polisi? Mkono wa Mkulima? Hakuna aliyeweza
kutoa jibu sahihi. Wakati wa mapumziko mwalimu alimwendea mwanafunzi huyo na
kumuuliza. “Mkono huu ni wa nani?” mwanafunzi wa darasa la awali alijibu “ ni
mkono wako mwalimu.”(Fr.Kamugisha) Mwalimu alitokwa na machozi alivyokumbuka alivyokuwa
anamsaidia mwanafunzi huyo kuvuka barabara akimshika mkono kwa vile alikuwa ni
mlemavu wa mguu pia alimshika mkono kumsaidia kuandika a, e, i, o, u.” Ni
kwa msingi huo Mungu anatushika mkono tutoke katika mlango wa majaribu
Mungu apewe kipau mbele. Hata Kaisari alikuwa
mtawaliwa kwa Mungu. Viongozi kama binadamu wengine wote wako chini ya Mungu
kuna wakati watatakiwa na Mungu kutoa hesabu kwake. Mchungaji mmoja alikuwa
anahubiri na akakazia mambo matatu “ jipatie unayoweza kuyapat”Mkristu mmoja mzee
kiumri lakini tajiri alisema “ Amina.” Baadaye mchungaji alisema “ Tunza yote kadiri unavyoweza.” Yule mzee
alisema tena “ Amina.” Mchungaji alisema pia
“ Toa yote kadiri unavyoweza.” Mzee alisema, “ Hii ni aibu unaharibu
mahubiri mazuri.”( Fr. Faustine
Kamugisha)
0 Response to "MAHUBIRI JUMAPILI YA 29 MWAKA A WA KANISA KIPINDI CHA KAWAIDA"
Chapisha Maoni