Masomo,
1.Hek.11:22-12:2
2.2Thes.1:11-2:2
3.Lk.19:1-10
TAFAKARI: HURUMA YA MUNGU NI KWA WALE WOTE WALIO TAYARI KUTUBU MAKOSA YAO NA DHAMBI ZAO.
Tunavyoadhimisha jumapili ya 31 ya mwaka wa kanisa, taifa la Mungu tunaalikwa kutafakari juu ya huruma ya Mungu kwetu sisi wakosefu. Mungu katika mpango wake wa ukombozi ana mpango na kila mmoja wetu. Kila mmoja wetu ana nafasi kwa Mungu, na Mungu humpa kila mtu mda, ili aweze kufanya toba na kumrudia kwa mapungufu na madhaifu ambayo hujitokeza kwa kila maisha ya binadamu.
Katika kutafakari maisha yetu kama wakristu, leo katika somo la injili tunapewa mfano wa zakayo ambaye alionekana mkosefu, na asiyefaa au kuhitaji huruma ya Mungu. Zakayo kwa jitihada yake ya kutaka kumwona Yesu na Kuona utukufu wake anamsujudia Yesu Kristu. Basi hebu tuone kwanza maisha ya Zakayo. Huyu zakayo tunayeambiwa kwenye maandiko matakatifu hasa kwenye injili ya luka 19:1-10, tunaona kuwa alikuwa mtoza ushuru, chini ya dola ya warumi. Na kwa mantiki hiyo ushuru uliotozwa ulikuwa kwa ajili ya serikali ya warumi, tena mtoza ushuru mkuu.Zakayo alikuwa mtu tajiri, na pia na mbali ya kuwa tajiri, wayahudi hawakumpenda kwa kuwa aliwatoza ushuru na utajiri alioupata ulitokana na jasho lao. Hivyo alichukiwa na jamii yote ya wakati ule,kiasi kwamba hata hakuna aliyependa kumkaribisha Zakayo nyumbani mwake, hivyo alionekana kama myanganyi na pia mwenye dhambi.Kwa kufanya hivyo pia Zakayo hakuwa na rafiki wa kukaa naye karibu, hivyo aliishi upweke. Hivyo Zakayo kusikia habari ya Yesu, alikuwa na Kiu ya kukutana naye,kwa kuwa hakuwa na rafiki, hivyo kimbilio lake au chaguo lake la mwisho lilikuwa ni kwa Yesu. Zakayo anakimbilia kwenye umati ili akutane na Yesu, lakini kwa ufupi wake na wingi wa Umati, hafanikiwi kumwona Yesu, baadala yake anatafuta njia mbadala ya kuweza kumwona Yesu, hivyo anakwea mti ili amwone yule aliyekuwa anamtafuta. Kwa kukwea mti na mbali na matarajio yake, yesu mwenyewe anaangaza macho juu na kumwona zakayo na kumwambia ashuke waende pamoja nyumbani kwake zakayo. Zakayo kuona hivyo anasikia furaha isiyo kifani kwa kuwa amekutana na Yesu, tena anamkaribisha nyumbani mwake. Jambo hili linawashangaza wengi, kwamba, inakuwaje Yesu anakwenda nyumbani kwa mdhambi na tena mtoza ushuru usio halali kwao? Ni kweli hili ni swali la kujiuliza kuwa kwa nini huyu anashiriki na mdhambi tena mtoza ushuru?? Zakayo, kwa kumkaribisha Yesu Nyumbani kwake, anakuwa tayari kutubu na anatubu na anakuwa tayari kurudisha vile ambavyo alichukua pasipo halali, yupo tayari tena mara nne, yupo tayari kugawa nusu ya mali yake kwa maskini. Hapa tunapata fundisho kwamba zakayo na mbali ya kuwa mdhambi, sasa anabadirisha dira ya maisha yake, anabadilisha mwenendo wake, anabadilisha moyo wake, anabadilisha mtazamo wake juu ya ndugu zake, na juu ya jamii iliyomzunguka, zaidi ya hapo anabadilika kiroho na kumwelekea Mungu. Zakayo, kama inavyofahamika, kimaumbile alikuwa mfupi, mbali na kuwa mfupi, hilo kwake lilikuwa siyo tatizo, Zakayo anamshukuru Mungu kwa kupata wokovu nyumbani mwake. Ufupi siyo ugonjwa, ugonjwa mkubwa ni ufupi wa Moyo, na ufupi wa fikra. Moyo wake Zakayo haukuwa mfupi vile, moyo wake uliangaza na ulikuwa na kiu ya kuona mbali. Fikra zake ndo zilimfanya Yesu akavutiwa kwenda nyumbani mwake. Kumbe twaweza elewa kuwa Yesu alimwona zakayo siyo kwa kimaumbile akiwa juu ya mti, yesu aliona ndani ya moyo wa Zakayo na ndiyo ikampasa kumwambia ashuke chini ili aende nyumbani mwake. Moyo wa zakayo ulikuwa umejifungua kwa Kristu. Sisi leo pia twaweza kujifananisha na Zakayo? zakayo alikuwa mfupi kiasi kwamba alizingirwa na umati, na hapo hasingeweza kumwona yesu, lakini alitafuta namna ya kumwona Kristu. Kwa jamii yetu na mazingira yetu, sisi ufupi wetu uko wapi, na tuko kwenye umati gani ambao unatusonga kiasi kwamba tunashindwa kumwona Kristu maishani mwetu? Tuna mifano mingi, katika dunia ya leo hasa dunia ya utandawazi na technolojia, tunajikuta tumemezwa na huo utandawazi na tekinolojia kiasi kwamba hatuwezi kupaza sauti kumwita Kristu. Katika dunia hii wengi wetu tumefunikwa na njia ambazo ni za kisasa na siyo mpango wa Mungu, kama vile uzazi ambao siyo wa asili, utoaji mimba, ndoa za jinsia moja, euthanasia ,pia itikadi za siasa, udini, ukabila na mengineyo mengi yanatufanya tufanane na zakayo jinsi alivyozingirwa na umati na akashindwa kumwona yesu, lakini na mbali ya hayo Zakayo hakuishia hapo, alipaza sauti ili wokovu ufike nyumbani mwake. Je kwetu sisi tunapaza sauti gani kuepuka enzi ya utandawazi, ukabila, udini, ubaguzi wa rangi etc. ? japo tujue kuwa tekinolojia siyo mbaya, au utandawazi siyo mbaya, ila matumizi kuzidi kiasi, na malengo ndo yanafanya utandawazi na tekinolojia vionekane kuwa ni vibaya. Tukiwa kwenye ulimwengu huu yatubidi tujiulize maswali mengi kuwa je tunapaza sauti zetu kama Zakayo alivyopaza sauti yake akimtka Kristu apeleke wokovu nyumbani mwake?
Tuone uhusiano uliopo kati ya Zakayo na Yesu ambapo Zakayo ni Mdhambi, na Yesu ameona moyo wa zakayo na anamsikiliza kilio chake, Zakayo alitengwa na watu kwa sababu ya hali yake. Yesu kwetu anakuwa kimbilio la kila mmoja, zakayo alitengwa na watu na hakuwa na rafiki, lakini anapata rafiki wa maisha yesu, Yesu anakuwa rafiki wakati wa matatizo na mahangaiko, Yesu anakuwa rafiki wa wale ambao wamedharauliwa na wengine, Yesu anakuwa rafiki wa wale ambao wametengwa na jamii, Yesu anakuwa rafiki wa wale ambao hawana wa kuwatuliza, Yesu anakuwa rafiki wa wale ambao wamekosa upendo kutoka kwenye jamii au familia, upendo wa Yesu unapenya mpaka moyoni mwa mtu, urafiki wa Yesu usafisha mtu na kumfanya atoke kwenye matendo mabaya na kuwa na matendo mema. Na sisi kufuatana na mapungufu yetu, maisha yetu, hebu tumkaribishe Yesu Kwenye maisha yetu kama Zakayo alivyofanya.
Mwandishi wa Vitabu na Mtaalamu wa kuandika vitabu vya tamthiliya William shakespear alisema "Kwenye maisha kuna mawimbi, bila kuangalia umuhimu wa hayo Mawimbi mwisho wa maisha unaishia kuwa utupu na kituko" Kwa Zakaria alikubali hayo mawimbi, na ndani ya mawimbi ya kutopokelewa na watu akakutana na Kristo yesu ambaye alimletea neema na wokovu nyumbani mwake.
0 Response to " "
Chapisha Maoni