MAHUBIRI YA JUMAPILI YA 3 KWARESMA MWAKA A

Masomo. I. Kut 17:3-7  II. Rum 5:1-2, 5-8  III. Yn 4:5-42
TAFAKARI: “KRISTU NI MAJI YA UZIMA.”
Tunapoadhimisha Jumapili ya 3 ya Kwaresma hatuna budi kumshukuru Mungu kwa yale yote ambayo ametutendea katika kipindi kizima cha wiki tuliyomaliza.
            Tukianza tafakari yetu  kutoka somo la kwanza ( Kut 17: 3-7) tunaona Waisrael wakiongozwa na Musa kupita Bahari ya Shamu wakienda ile nchi ya ahadi wakipitia jangwa la Sinai. Mwanzoni mwa safari yao mambo yanaonekana kuwanyokea na wanapata uhakika kuwa Mungu yu Pamoja nao Katika safari yao na pia wanakuwa na furaha kwa kuimba nyimbo za furaha. Kadiri safari inavyoendelea kumbe mambo yanabadilika kinyume cha matazamio yao, katika hiyo safari wanaanza kukumbana na changamoto za kila aina kama vile joto kali njiani wanakumbana na wanyama kama vile nyoka wakali, na pia wanakuwa na kiu jangwani, sehemu ambayo ni kame na haina maji. Ni Kwa msingi huu tunaona wana wa Israel wanaanza kumhisia Mungu vibaya na wanaanza  kuwa na mashaka naye. Wanaanza kuwaza Mungu kuwatoa utumwani Misri ilikuwa ni mbinu ya Mungu ya Kuwaangamiza. Mungu kweli yu pamoja nasi? ( Kut 17:7) Sehemu ambapo haya yote yanafanyika paliitwa “ Massah – Meribah”  Kwa Kiebrania maana yake “ Majaribu”
            Haya yaliyowapata wana wa Israel katika maisha ya Mkristu pia hayakosekani. Kama wao tunaambiwa kuacha maisha ya utumwa wa dhambi na kumrudia Mungu. Wengine kati yetu ni Wakatekumeni, ambao watakuwa wana wa Kristu kupitia ubatizo. Tukishabatizwa huwa tunafikiria kuwa ndo mwanzo na mwisho wa shida zote, kwa kuwa tunafikiria kuondolewa dhambi zetu. Mara nyingine kama mambo hayajaenda salama huwa tunamgeuzia mgongo Mungu. Ni kwa msingi huo sisi changamoto tukumbananazo huwa tunafikia hatua ya kumweka Mungu Pembeni na kufuata njia nyinginezo.
            Katika somo la pili ( Rum 5:1-2. 5-8) tunaambiwa kuwa fadhila ya matumaini haipatikani katika yale tuyafanyayo, mf, matendo mema, bali fadhila hiyo hupatikana kutokana na Roho ya Mungu na Upendo wake. Mungu upendo wake ni tofauti na sisi tufikiriavyo. Mt. Paul anasema “ Matumaini yetu siyo danganyifu si kwamba sisi tu wema, lakini kwa kuwa Mungu wetu ni mwema ( Cf. Rum 5:1-2)
            Kutoka somo la Injili tunaona Yesu akiwa amechoka na anakaa Kisimani kuwasubiri wanafunzi wake walioenda kutafuta chakula. Kisimani tunaona pia mwanamke anakuja kuteka maji, Yesu anamuulizia Yule mwanamke maji ya kunywa. Yule mwanamke anamshangaa Yesu kumuulizia maji ya Kunywa kutoka kwake. Sababu ya kushangaa Yule mwanamke ni kuwa yeye alijua wazi kuwa yesu alikuwa ni Mgalilaya, lini na wapi Mgalilaya akaulizie kitu kutoka kwa Msamalia??na Kwa nini Yesu alivunja mila ya Wayahudi  iliyokataza kwa wakati ule kuongea na mwanamke asiyemjua sehemu faragha! Walimu wa Kiyahudi ( Rabbi) kwa wakati ule waliweka  taratibu kuwa kama mwanaume ingelitokea akakutana na mwanamke hakuruhusiwa kuongea naye kwa muda mrefu. Wanafunzi wake Yesu nao wanashangaa kuja na kukuta Yesu anaongea na Yule mwanamke??( Msamaria). Fundisho: “Upendo wa Kristu unaenda hadi nje ya Mipaka ya Binadamu Kristu anachotaka kutoka kwetu sisi wafuasi wake ni kile kitokacho moyoni  na siyo kutoka katika mwonekano wa nje.”
            Tuone kidogo juu ya huyu mwanamke.Mwinjili Yohane hapa anatuletea mwanamke ikiwa ishara ya jambo Fulani. Kisima katika Biblia ni ishara ya mahali pa makutano  kwa watu wanaopanga kuoana. Katika kitabu cha agano la Kale Isralel ni Ishara ya Bibi arusi na Mungu akiwa Bwana arusi. Hivyo Israel ni mchumba wake Mungu. Israel kama mchumba wake Mungu, ni mara ngapi huyu mchumba amefarakana na Bwana arusi wake?( Mungu) ni mara ngapi huyu Bibi arusi amefarakana na wamisri, wagiriki, wa Babuloni, wa Persia na Warumi?
            Injili ya Mt. Yohane inatuonyesha jinsi Kristu alivyo Bwana arusi  kwa watu wake ambao ni wakosefu, huyu Bwana arusi anakuja kurudisha urafiki wa binadamu na Mungu ulioanguka  kwasababu ya dhambi. Katika Injili tumesikia kuwa wanafunzi wa Yesu walienda kutafuta chakula. Mwanamke alikuja kuteka maji kisimani. Kristu anachakula na maji ya uzima ambayo wao hawayajui ( Yn 4:10,30). Mwanamke anaenda Kisimani kilasiku kuteka maji kwa kuwa maji atafutayo kila siku hayawezi kuzima kiu yake ya kweli. Maji katika kisima  ni Ishara ya starehe, na anasa za kila namna ambazo watu hutafuta kutoshereza mahitaji yao ya kimwili. Starehe na Anasa  haviwezi kutuletea uzima wa milele. Ni upendo na Roho ya kimungu viletavyo raha ya milele.
            Maji ya uzima ambayo Kristu anayasema ni Roho ya Kimungu na Upendo wa Kimungu nafsini mwetu ndo vyaweza kuleta uzima wa milele. Mwinjili Yohane anatuambia kuwa mwanamke anaacha jagi la maji na anaonekana kugundua maji ya aina nyingine. Katika mazungumzo yao, yaani Yesu na yule mwanamke Msamaria, mwanamke anaonekana  kuwa na hamu na shida ya maji ya kunywa, na anaonekana kuridhishwa na raha, na Starehe za dunia. Polepole mwanamke anakuja kuelewa kuwa Kristu anataka nini kutoka kwake.  Mwanamke msamaria baada ya kugundua na kuelewa taratibu nini Kristu anataka kutoka kwake anaanza kubadilisha mtazamo wake na mawazo yake juu ya Kristu.  Mwanzo kabisa mwanamke Msamaria anapokutana na Kristu anamchukulia  kama Myahudi na mpita njia ( Yn 4:9) Baadaye anamtambua kama “ BWANA” ( Yn 4:11). Baadaye kama nabii ( Yn 4:19), na baadaye kama Masiha ( Yn 4:19). Baadaye mbele ya watu wote yule mwanamke Msamaria anamtambua Yesu kama mwokozi wa Dunia (Yn 4:42)
            Kwetu sisi sote na Wakatekumeni wanaojiandaa kuwa wana wa Kristu kwa njia ya ubatizo, hivyo ni mwaliko kwetu kuwa na imani na kumfuasa Kristu tukifuata mfano wa mwanamke Msamalia alivyofanya kumtambua Kristu na kumfuata.

            Kwa upande wetu sisi wakristu tunakutana na Kristu wapi?? Tunakutana naye sehemu nyingi sana, mf. Katika maeneo yetu ya kazi, njiani, na katika nyanja mbalimbali za maisha hasa katika maisha yetu tuliyoyachagua kama wakristu kumfuata. Tukumbuke kuwa katika kuwa wakristu wa kweli tunapitia katika hatua na njia mbalimbali hadi tunapata ufunuo na kumjua Kristu kuwa ni mwana wa Mungu, na mwokozi wa dunia kama mwanamke Msamaria alivyofanya.

Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI YA JUMAPILI YA 3 KWARESMA MWAKA A"

Chapisha Maoni