MAHUBIRI YA MKESHA WA KRISIMASS

MAHUBIRI YA  MKESHA WA KRISIMASS
MASOMO: 1. Isa 62: 1-5
                     2. Mate 13:16-17. 22-25
                     3. Mt 1: 1-25

TAFAKARI:  YESU KRISTU KUZALIWA KWETU NI ISHARA YA MAISHA YENYE FURAHA NA AMANI.
Tunaposherekea mkesha wa kuzaliwa kwa mtoto Yesu Kristu, yaani Emmanuel, Mungu yu pamoja nasi, yatubidi tutafakari juu ya maana ya Krismass au Noel ina maana gani kwenye maisha yetu. Katika somo la kwanza kutoka nabii isaiya 62:1-5 tunasikia habari ya Matumaini kwa waisrael ambao walikuwa kwenye mahangaiko na utumwani, tunasikia ahadi ya kuzaliwa mkombozi na mwokozi ambaye analeta matumaini, amani  na haki. Tunaposherekea kuzaliwa kwa mtoto Yesu, tunakumbushwa kuwa, kuzaliwa kwake, ni ishara ya maisha yenye uzima wa Milele.  Kipindi hiki cha Noel, watu utakuta wamepamba nyumbani kwao kwa miti ya Krismas, Mti wa Krismas ni ishara ya uhai na uzima kwetu sisi.  Pia kwenye banda la wanyama ambapo Kristu amezaliwa ni ishara ya kuonesha kuwa Kristu alizaliwa katika mazingira duni, na ni kuonesha kuwa yu kati yetu, Immanuel, Mungu yu Pamoja nasi.
Katika kipindi hiki cha kuzaliwa Mtoto Yesu, tunaona wengi wetu tunapeana zawadi na pia tunaandikiana barua na message zenye ujumbe wa kutakiana amani  ya Krismas, Je twaweza kujiuliza swali moja kuwa kupeana zawadi na kutengeneza chakula kizuri na vinywaji ndio maana ya Krismass? Jibu ni hapana, hivi vyote ni mapambo na ishara ambazo  zinamaanisha upendo wa Mungu kwetu sisi kwa kuzaliwa Mtoto Yesu. Yesu Kristu, yaani Emmanuel, Mungu yu pamoja nasi anazaliwa katika mazingira ya ajabu na kawaida. Emmanuel, yaani Mungu yu pamoja nasi, anazaliwa katika holi la kulishia ngombe, hakupata nafasi katika nyumba ya wageni, kuzaliwa katika mazingira haya inamaanisha kuwa Kristu alikuja kushiriki maisha yetu sisi binadamu kama mtu wa maisha duni na maisha ya kiwango cha chini.  Kumbe kuzaliwa kwa mtoto yesu katika maisha duni, kunatukumbusha ni namna gani Mungu ametupenda.
Tunavyotoa zawadi za Krismas kwa wakati huu, hatutoi hizo zawadi kwa kuwa ni wajibu wetu kuzitoa, bali ni kwa sababu ya upendo tulionao kwa nduguzetu, kama sisi twaweza kufanya hivyo, je Mungu mwenyewe tumfananishe na nani ambaye ametoa zawadi kwetu ya Kuzaliwa mtoto yesu, ambaye jina lake ni Emmanuel, yaani Mungu pamoja nasi. Hivyo, kama Mungu yu pamoja nasi, hatuna budi kumpokea na kumfungulia milango ya Mioyo yetu ili awe nasi. Tukiendelea kutafakari fumbo la umwilisho wa Kristu, tujiulize kuwa Kristu anapozaliwa  ni kweli anazaliwa mioyoni mwetu? Kwa mazingira ya wakati ule Kristu hakupata nafasi katika nyumba ya wageni, hivyo Mama yake akapata nafasi katika holi la kulishia ngombe na mifugo wengine, Je sisi nyumba zetu,yaani roho zetu ziko tayari kumpokea Kristu ambaye ni Mungu pamoja nasi, na je Kama kufuri za mioyo yetu zimefungwa Mtoto Yesu ambaye amezaliwa kati yetu  tunamkaribisha wapi?

Kwa hali zetu za maisha, Kristu anapozaliwa anakuja na kanuni mpya za maisha, anatuondoa kwenye maisha ya unyonge, anakuja kuishi na watu wote bila ubaguzi wa aina yoyote ile, aidha uwe ni ubaguzi wa rangi, ukabila, udini, na matabaka ya aina yote ambayo yapo kwenye jamii. Mtoto yesu anapozaliwa kati yetu anakuwa mwanga wa mataifa, anakuwa mtu wa kuleta upendo, matumaini na kuondoa roho za chuki, wivu, uchoyo na uzembe. Katika kutafakari kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristu usiku huu pia tunaalikwa kutafakari juu ya ukimya na kutafakari matendo makuu ya Mungu( Silent Night) Ukimya unaoongelewa ni hali ya ‘Vigelegele’ na si ‘kelele’ Wakati huu wa Krismas ni wakati wa kugawana kile tulicho nacho mifukoni mwetu, ni wakati wa kutakiana amani, zawadi hizo basi zisihishie wakati wa kipindi cha Krismas bali ziendelee katika maisha yetu yote. Krismas ni kipindi cha kutoa na si kutapanya, kila mmoja ana haki ya kutumia alichonacho  kwa ustaarabu, Krismasi inatukumbusha juu ya wito wetu wa kutoa hazina zetu kwa wahitaji ambao maisha yao ni duni. Kristu mwenyewe amezaliwa katika maisha duni, na kupitia maisha hayo duni anakuja kuwainua wanyonge na waliokandamizwa. Basi sisi tunavyosheherekea Krismas tukumbuke kugawana mkate wetu wa  Krismas na wale ambao maisha yao ni duni, na kufanya hivyo tutakuwa tumemkaribisha Masiha ambaye anazaliwa katika mazingira duni mioyoni mwetu.

Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI YA MKESHA WA KRISIMASS"

Chapisha Maoni