MAHUBIRI YA JUMAPILI YA KUPAA KWA BWANA

MASOMO: 1. Mdo 1:1-11
                    2.Efeso 1:1-23
                    3.Mt 28: 16-20


TAFAKARI:  YESU KATIKA KUPAA AMEONYESHA KANISA NJIA YA KWENDA

Tukianza tafakari yetu kutoka somo la kwanza( Mdo 1:1-11) tunaona mwandishi wa kitabu cha matendo ya mitume, Luka anaonyesha kuandika barua kwa mtu aliyeitwa Theofilo ambaye maana yake ni yule mpenda Mungu. Mwandishi, Luka, kwa msingi huu alikuwa hamaanishi kumwandikia barua mtu aliyejulikana kama Theophilo, bali alimtumia huyo kama kielelezo cha wale wote wampendao Mungu( Wale waishio pendo la Mungu). Katika hili somo la kwanza tunaona mwandishi akiongelea juu ya Yesu kuwahusia wanafunzi wake juu ya siku arobaini na kupaa kwake. Yatubidi tuelewe nini maana ya siku arobaini katika maandiko matakatifu. Tujiulize swali kuwa Yesu Kristu baada ya ufufuko wake aliwatokea wanafunzi wake mara kadha wa kadha. Yesu aliwatokea wanafunzi wake mara 10, na baada ya hapo tujiulize kuwa  zile siku nyingine arobaini alikuwa wapi?

Wakati wa ufufuko wake ( Pasaka) Yesu aliwatokea wafuatao
1. Maria Magdalena
2.Wanawake waliokwenda kuona kaburi
3. Kleopa na yule mfuasi( mwanafunzi mwingine walipokuwa Barabarani kuelekea Emausi)
4.Peter
5.Kwa wale wanafunzi 11 isipokuwa Thomasi
6.Juma moja baadaye aliwatokea wanafunzi wake 11 akiwepo na Thomasi.
7. Aliwatokea pia karibu na Bahari ya Galilaya ambapo walikamata samaki wengi.
8.Aliwatokea pia katika ule mlima wa Galilaya alipowaambia wanafunzi wake kwenda kuwafundisha mataifa yote na kubatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu( Mt28:19)
9. Wakati walipokuwa mezani wakimega mkate aliwatokea na kuwaambia maneno haya " kwa jina langu na watatoa mapepo, watanena kwa lugha n.k ( Mark16:17-18)
10. Na mwisho tunaona Yesu anawatokea pale Bethania kabla ya kupaa mbinguni . Kuwatokea wafuasi wake ilikuwa ni uthibitisho kuwa ni kweli  amefufuka na kutoweza kukaa nao siku arobaini ilikuwa ni kudhihirisha utukufu wake tofauti na maisha yake kabla ya kufa.

Na je Yesu alikuwa wapi hizi siku 40? Mt. Thomasi aquina anajibu hili swali kama ifuatavyo" Haifahamiki alikuwa wapi siku zote hizi, na kwa hili maandiko matakatifu hayaongei lolote juu ya Yesu alikuwa wapi siku hizi zote. Utawala wake uko kila mahali ( STIII, Q.55a3ad2) Hivyo yawezekana kwa kipindi hiki chote  cha siku arobaini  alikuwa katika kipindi cha ukimya, sala, na tafakari.

Tukiendelea  na tafakari juu ya siku arobaini tunaona kuwa siku 40 kimaandiko matakatifu inamaanisha maandalizi au matayarisho ya wanafunzi wa Kristu kwa tukio kubwa. Kadiri ya desturi za kiyahudi siku arobaini ilikuwa na maana ya wanafunzi kukaa na mwalimu wakielekezwa mafundisho fulani na baada ya hapo hao wanafunzi walihararishwa  kufanya kazi ya utume na pia kuitwa wanafunzi waliofuzu mafunzo. Katika somo tunana pia Kristu anawaambia wanafunzi wabaki Yerusalemu ili wapate kumpokea roho wa ukweli ( Mk 13:11). Kristu anaongelea juu ya kufanyika upya kwa mbingu, hasa akiwaasa wanafunzi wake kazi watakazofanya ndo zitafanya kufanyika kwa ufalme wa mbingu ambao unakua taratibu na polepole.

Tumesikia juu ya Kristu kupaa mbinguni. Mwandishi wa kitabu cha matendo ya mitume, Mt. Luka amechukua picha hii/ taswira kutoka agano la kale, Mw5:24 ( habari juu ya Enock kuchukuliwa mbinguni), Eliya, 2Falme2:9-15 Eliya naye alionekana kuchukuliwa na upepo wenye nguvu katika wingu.

Kupaa kwa Yesu kunatufundisha juu ya kuwa na Imani thabiti hasa pale ambapo milango yetu ya fahamu haiwezi kuhisi ( Kushika, kuona, kusikia, na kuonja n.k) Kristu anavyoingia katika utukufu hali yake inakuwa tofauti na sisi kwa kuwa hali yake ipo katika ulimwengu mwingine tofauti na ulimwengu wetu( Duniani)

Ni takribani miaka 2000 iliyopita kanisa limeanza safari ya kiimani, swali la kujiuliza ni je kanisa limekuwa likiangalia matatizo yanayoikumba jamii na yanayohitaji ufumbuzi wa haraka? sisi kama kanisa tumeacha wajibu wa msingi na kuangalia mawinguni?kama kanisa tumetetea haki za wanyonge, wanaoonewa, maskini, na matabaka kandamizi katika jamii?

Kutoka katika somo la Injili tunaona Yesu Kristu anakutana na wanafunzi wakeYerusalemu ambapo ndipo alipoanzia utume wake. Galilaya kwa kipindi kile haikuheshimika kama vile sisi pia tusivyoheshimu baadhi ya makabila ya wenzetu, tamaduni zao na mila zao kwa namna fulani. Galilaya haikuheshimiwa kwa kuwa ilikuwa ni sehemu iliyochanganyikana na wapagani. Mathayo anatuambia kuwa ni kwa hawa wapagani ambapo injili ya Kristu inaenda kuhubiriwa( utume wa Kristu hadi miisho ya dunia). Yerusalemu unakuwa tena mji wa amani kama jina lake lilivyo, unakuwa mji uliomkataa Kristu na hatimaye kumsulubisha msalabani.

Sehemu ya pili ya injili inagusia juu ya kazi na utume wa Yesu Kristu hapa duniani, ni kuwa yeye alikuja kutimiza kazi aliyotumwa na Baba wa mbinguni, na ni kwa msingi huu na yeye anawatuma wanafunzi wake waendeleze kazi hiyo aliyoianzisha( Mt28:18-20). Hivyo na sisi ni mwaliko kwetu kuwa tusiwe watazamaji bali tunaalikwa kushiriki katika kazi za kitume hasa katika uwanja mpana wa uinjilishaji. Tunaitwa kuivaa sura ya Kristu na kumtangaza kwa mataifa. Kristu kupaa kwake kunadokezea pia kushuka. Alishuka pia hata Gethesemane, Kalvari na Kaburini, vilevile sisi katika kupaa tunakumbushwa tushuke kwa wale ambao ni wa hali ya chini kimaisha, na kiroho.

HITIMISHO
Siku ya Kupaa mbinguni kwa Yesu Kristu pia kunaashiria majukumu mapya kwa upande wa mitume. Yesu anatuambia kuwa sasa kazi kwetu. Utume wetu utafananishwa na mbio za kupeana vijiti. Kristu hajatuacha yatima bali amemtuma Roho mtakatifu atulinde na kutuimarisha.

" Mbunge mtarajiwa alipoulizwa swali aeleze amesoma hadi kiwango gani, yaani shahada au stashahada, naye alikuwa na haya yakusema kwa wananchi wake alikuwa na haya yakusema  " kuwa hata pete aliyovaa ni ukumbusho wa shahada alizopata huko America. Aliendelea kusema kuwa Elimu ya msingi huanzia na a, e,i, o, u alianza kufafanua herufi hizo a-inasimama baadala ya adabu,hivyo akatamba kuwa yeye ni kiongozi mwenye adabu, e- inasimama baadala ya Elimu, na hivyo akaonyesha kuwa yeye ameelimika vya kutosha, i- inasimama baadala ya imani, hivyo akaelezea kuwa yeyote anayejiinua kuwaongoza watu ni lazima awe na imani nao na hivyo akaonyesha kuwa wananchi wake watamchagua. o-inasimama baadala ya neno ongoza, mbunge mtarajiwa yuko tayari kuongoza, u- inasimama baadala ya unyenyekevu, kiongozi lazima awe mnyenyekevu. Ili kupanda ngazi ya uongozi lazima kushuka na kunyenyekea."(Rev. Fr. Faustine Kamugisha)

Mwisho tunaitwa kuwa na upeo wa kuona na kuangalia mbali, tujue kuwa nyuma ya mlima kuna mlima. Yesu alikuwa na wanafunzi wake katika mlima wa Mizeituni( Mdo1:12). Unapokuwa mlimani unakuwa na picha kubwa kiupeo, Kristu aliwapeleka mlimani mitume wake akawaonyesha dunia, miliki zake na miisho yake, kuwa na picha kubwa akilini tunaalikwa kuepuka udini, ukabila na kuheshimu mila za wenzetu. Picha ndogo katika upeo zinatupeleka katika udini, na ukabila.

Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI YA JUMAPILI YA KUPAA KWA BWANA"

Chapisha Maoni