MAHUBIRI JUMAPILI YA 6 YA PASAKA

MASOMO:
1. Mat 8:5-8. 14-17
2.1Pet 3:15-28
3.Yn 14: 15-21

TAFAKARI: " AHADI YA KRISTU KUTUPA ROHO WA UKWELI"

Tukianza tafakari yetu tumesikia kutoka katika kitabu cha matendo ya mitume Mat8:5-8.14-17 tunaona kuwa baada ya kifo cha Kristu Kanisa lilikuwa bado kuvuka nje ya Yerusalemu. Wakristu wa kwanza  walikuwa bado hawajatambua juu ya kueneza injili pia ngambo ya Yerusalemu ambapo watu wote walihitaji  kusikia neno la Mungu.

Neno la Mungu  lilipata kuenea nje ya Uyahudi baada ya kuuawa kwa stefano( Mat 8:1-4). Haya mauaji yalihusu wale wayahudi ambao walikuwa siyo wahebrania( Hebrews) ila ilikuwa ni kwa wale wayahudi wakristu waliohesabiwa kuwa siyo wayahudi halisi, wayunani ( Hellenists). Wayunani walionekana kuwa ni wanamapinduzi na walionekana kimaendeleo kuwa juu ya wenzao, wayahudi wa Kiebrania ni kwa msingi huu tunaona wanauawa. Baada ya mauaji hayo wayunani wa kiyahudi wanakimbilia miji mingine ya Israeli wakitangaza habari njema ya Kristu kule Antiokia walipokimbilia hawa wayunani injili ilitangazwa hadi kwa wapagani ( watu wa mataifa). Katika somo la kwanza tumesikia habari juu ya filipo ambaye alichaguliwa kama shemasi kwa ajili ya huduma ya neno na kuwahudumia wajane, huyu pia alikuwa myunani( Hellenist) na huyu baada ya kuona upinzani na mauaji ilimbidi naye akimbilie Kaskazini kuelekea Samaria ili asipate kuuawa kama stefano alivyouawa. Mara baada ya kufika Samaria alihubiri injili ya Kristo na kubatiza pia wale waliomwamini Kristu. 

Roho mtakatifu alimpa filipo nguvu ya kumhubiri Kristu msulubiwa, wengi walibadilika na kungoka kutokana na mahubiri ya filipo na wakamwamini Kristu( Mat 8:5-8) Tunaona pia Peter na Yohane wanawawekea mikono wakristu wapya waliobatizwa. Walipowawekea mikono ishara za ajabu zikatokea. Kutokea kwa ishara hizi kuliashiria kuwa Mungu alitaka kuonyesha kuwa kila Neno lilipotangazwa Jumuiya mpya za Kikristu zilifanyika na hasa kuonyesha umoja wa hizo mpya na zile zilizotangulia kuwepo.

Kutoka somo la pili( 1Pet 3:15-18) tunaona Peter anawasihi wakristu wasikate tamaa katika kumtumikia Kristu kwa sababu ya mateso na mahangaiko ambayo yalikumba jumuiya nyingine za wakristu. Hapa pia na sisi tunapata ujumbe kuwa ni mwito kujua kuwa mbali na changamoto tunazokumbana nazo Kristu bado yu pamoja nasi hajatutupa, imani yetu katika Kristu isikatishwe na changamoto tunazokumbana nazo( Kuuawa kwa mapadri, wachungaji, uchomaji wa makanisa n.k). Peter anatoa fundisho ( 1Pet 3:17-18) juu ya wakristo kuwa wavumilivu, watu wa kutolipa visasi, watu wa kutotumia lugha chafu, na baadala yake wawe watu wa maneno na lugha nzuri kwa wengine, kutokuwa watu wa kejeli, na matusi, watu wataelewa  na kufahamu  kuwa sisi ni watu wa Kristu pindi tukiwa kielelezo cha kutumia lugha nzuri katika kueleza ujumbe wa Neno la Mungu.

Kutoka  somo la Injili ( Yn 14:15-21), Injili ya leo ni mwendelezo wa injili ya jumapili iliyopita ambapo tunaowaona wanafunzi wake Kristu wanahuzunika  juu ya Kristu kuwaacha, Kristu anawaahidi na kuwahakikishia kuwa hatowaacha yatima, anawaahidi kuwaachia msaidizi naye si mwingine bali ni Roho mtakatifu ambaye atakuwa nao. Ni akina nani watampokea huyo roho wake?Yesu anasema kuwa ni wale watakaoishi upendo wake, wale washikao amri zake ( Yn 14:15-17). Kristu pia anaongelea juu ya ulimwengu akisema " huyo roho ndiye roho ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea." Tujiulize ni ulimwengu upi Kristu anaongelea hapa? Jibu ni kuwa ulimwengu ambao Kristu anaongelea ni juu ya ile mioyo ambayo hutunza chuki, uasama, hasira, unafiki, uvivu, na mawazo mabaya ambapo roho wa Kristu hawezi ingia katika roho za namna hiyo. Huyo Roho wa kweli( Advocate) ni yule ambaye ni wakili wetu na msaidizi wetu. Huyu ni yule ambaye anatusimamia pindi tuwapo katika mihangaiko ya maisha na ya kiroho. Hakuna nafasi kanisani  kwa watu waoga, wachovu wa kiroho, na wale ambao hawajampokea roho wa kweli. Ni kwa mgingi huu tunaona wafuasi wa Kristu na mbali ya kukumbana  na changamoto hawakati tamaaa katika kulitangaza  Neno la Mungu.

Msaidizi huyo pia twaweza kumjua kwa jina jingine yaani roho wa ukweli( The Spirit of Truth). Ni ushahidi tosha  kabisa kuwa kanisa letu Katoliki daima limekuwa likiongozwa na wachungaji( Mashemasi, Ma padri, na Maaskofu) ambao siyo wakamilifu, hata hivyo hakuna hata mmoja wao ambaye aliweka pingamizi juu ya injili ya Kristu. Ni huyo roho wa ukweli ambaye ataleta ufunuo wa yale ambayo hata wafuasi wa Kristu hawayajui ili wapate kuyajua.

Hivyo tunahitaji uvumilivu na mbali ya changamoto tunazokumbana nazo katika kumtangaza Kristu. Kristo alivumilia. Hakuna Pasaka bila ijumaa kuu. Kristu alitukomboa. Mfano wa nguvu ya uvumilivu " Fikiria stampu kwenye Bahasha nguvu yake na manufaa yake yapo katika uwezo wake wa kubaki kwenye Bahasha mpaka bahasha imfikie mlengwa ( Fr. Faustine Kamugisha)

Related Posts:

1 Response to "MAHUBIRI JUMAPILI YA 6 YA PASAKA"