MAHUBIRI YA JUU YA FAMILIA TAKATIFU YA YESU, MARIA, NA YOSEFU.

MAHUBIRI  YA JUU YA FAMILIA TAKATIFU YA  YESU, MARIA NA YOSEFU.
MASOMO:
1. YbS 3: 2-6. 12 -14
2.  Kol 3: 12 - 21
3.  Mt 2: 13-15. 19-23

TAFAKARI: Ni wajibu wa wazazi na walezi kuwalea na kuwakuza watoto katika maadili ya Kikristu.
Tunavyosheherekea juu ya jumapili ya Familia takatifu, tunaalikwa kutafakari maisha ya familia ya kikristu ambayo ndo chimbuko la jumuiya ndogondogo za Kikristu na Kanisa kwa ujumla. Tukiongozwa na tafakari yetu, basi tunaalikwa sote tuwe wazazi au walezi kuwakuza watoto katika maadili ya Kikristu.
Katika familia jambo la kwanza ni kwa upande wa watoto kuwaheshimu wazazi wao yaani Baba na Mama. (YbS 3: 2-6. 12 -14) Heshima hiyo inapatikana katika familia shule ya malezi. Hapa tunakumbushwa wajibu wa watoto walionao kwa wazazi wao.
Katika Familia ya Yesu, Maria na Yosefu, kuna jambo la kujifunza, kuwa maisha ni safari, kwenye maisha kuna milima na mabonde. Hayo yote tunayaona katika maisha ya Familia ya Maria, Yesu, na Yosefu.
Nyumbani ni Shule ya malezi, katika kukaa nyumbani na wazazi watoto wengi huona kuwa kukaa na wazazi wao ni msalaba, na pia hutamani kuhama nyumbani kwao na kwenda kusikojulikana, japo kimsingi malezi mema ya Kikristu huanzia kwenye familia. Kwa upande wa wazazi na walezi ni wajibu wao kuwa nyumbani wapafanye mahali pa kukalika. Katika kitabu cha methali kuna haya juu ya familia, rejea  “ Mwanangu sikiliza mwongozo wa Baba yako, wala usiyapuuze maagizo ya mama yako” ( Methal 1:8) Zawadi kubwa ambayo mzazi anaweza kumpa motto ni kumlea na kumpa mifano mizuri juu ya maadili ya Kikristu. Lakini hapa kunajambo linashangaza kwamba baadhi ya wazazi wanawapenda baadhi ya watoto wao ambao ndo wamewazaa wenyewe, wakati hawajui kuwa watoto walionao  hakuna hata mtoto mmoja ambaye aliwachagua wamzae au hakuna mzazi hata mmoja ambaye alichagua kuzaa watoto alionao mbali ya mazuri yao, mapungufu yao na maumbile yao. Mhubiri mmoja mahili Rev. Fr. Faustine Kamugisha alikuwa na haya ya kusema juu ya kulea watoto Kulea watoto ni kama kujenga orofa ya nyumba ishirini kwenda juu. Orofa ikiwa nyumba ya pili kama imelemaa hakuna anayegundua haraka. Lakini nyumba ya ishirini kila mtu ataona kuwa orofa imelemaa. Mtoto akifikia umri mkubwa kama kuna jambo halikwenda vizuri kimalezi litajulikana.”
Katika Familia tunaona yakuwa ni Kanisa dogo, ambapo sala na maombi hushamili. Kwa fanya nyumba kuwa kanisa dogo pia watoto hujifunza maadili mema ya Kikristu, ikiwemo kumcha Mungu. Katika familia inayomtegemea Mungu matunda na kazi yake vyote huonekana. Katika familia inayosali na kumcha Mungu, utaona hata mienendo ya wanafamilia na waziwazi utajua kuwa hii ni familia ya Kikristu.  Mzaburi anasema kuwa Mungu asipoijenga nyumba waijengao wanafanya kazi bure (Zaburi 127:1)
Katika kutafakari juu ya maisha ya familia takatifu tunajifunza kuwa nyumbani ni mahala pa kufanya kazi, Yosefu alikuwa seremala na alimfundisha Yesu Kazi hiyo, hivyo tunakumbushwa wajibu kama wazazi au walezi kuwafundisha watoto kazi. Tunavyofanya kazi mbalimbali tunakuwa tumeshiriki kuendeleza ile kazi ya Mungu ya uumbaji. Hili linajidhihirisha katika maandiko matakatifu ambapo mtume Paulo ana sisitiza kuwa asiyefanya kazi na asile. Lakini katika jumuiya zetu tunakuta mambo ni kinyume kwamba kuna ambao huweka mikono yao mifukoni lakini ikifika mda wa chakula wanakula bila kuweke hiyo mikono mifukoni ( wategeaji) Inashangaza kwamba katika familia ni mtu mmoja anafanya kazi lakini wanakula ni tisa na kenda.
Ili nyumba iwe nyumbani na si hoteli kufanya kazi ni jambo la kila mwanafamilia kama hana kilema au umri unaomzuia kufanya kazi. Tatizo kubwa linalokutwa mijini ni wanafamilia au jamaa toka vijijini kukaa na jamaa zao mijini pengine bila kushiriki shughuli muhimu za nyumbani. Mwenyeji wao akienda kufanya kazi anawaacha nyumbani pengine wanatazama runinga bila hata kufanya kazi za nyumbani. Hapa msemo wa mtegemea cha nduguye hufa angali masikini una maana kubwa. Hili linafanya nyumbani kwa huyu mgeni siku ya tatu isiwe nyumbani bali hotelini.



Tunaposema “jisikie nyumbani,” nyumbani tuna maana ya kwamba pawe mahali pa kukalika, mahali pa amani, furaha, malezi, undugu, faraja, kusikilizana, maelewano, ukarimu na mahali pa kazi. Baba Mtakatifu Benedict xvi alikuwa na haya ya kusema juu ya Familia “Familia ni Hekalu au Kimbilio ambapo maisha huanzia, na Kiini cha jamii na Kanisa kwa ujumla”( Mahubiri juu ya wajibu wa mwafrika- (Africae Munus ,No 42) Papa anaongeza kusema kuwa watoto hujifunza upendo, na kupenda ikiwa na wao hupendwa bila kikomo na wazazi na walezi wao. Papa Benedict xvi anaendelea kusema “ Familia ni mahali ambapo utamaduni wa kusamehe na kupatanishwa hushamiri” anaendelea kusema zaidi kuwa katika familia iliyo imara na ya Kikristu, ndo tunakuta haki, amani, upendo na mshikamano kati ya Baba, Mama, Kaka, na Dada. Baba mtakatifu Benedict anaongeza kusema kwamba ili familia ikue kiafya na kimaadili kuna haja ya kujifunza juu ya sacramenti ya Ekaristi ambapo maisha ya Mkristu huwa mapya zaidi na zaidi anavyokuwa karibu na sakramenti ya Ekaristi.


Maisha ya familia yaani Baba, Mama na Watoto, ya weza kufananishwa na mpira wa Miguu uwanjani ambapo ili kufunga bao lazima wachezaji wote washirikiane, pasipo kushirikiana matokeo yake ni kufungwa mabao mengi. Vilevile katika Familia lazima kuwepo moyo wa ukarimu wa kushirikishana mapaji, nguvu, akili, na mapato yote yatokanayo na kila mmoja akipatacho kwa akili na jasho lake. Mtoto akikuzwa kwa maadili mema maadili mema pia hii ni kuipunguzia familia aibu kwa watu. “Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; kazidi kupendwa na Mungu na watu” (Lk 2: 52) Yesu Kristu mwenyewe amekuwa mfano wa kuigwa ambapo amekua katika hekima na kimo, lakni kwetu hapa cha kushangaza ni kuwa watoto wanakuwa katika kimo na si katika hekima.  Watoto wengi hapo awali walizaliwa wakiwa na sura ya malaika lakini hadi sasa waishabatizwa majina ambayo siyo mazuri kuyatamka, kama vile mwizi, mlevi, mzinzi, jambazi, tukijiuliza kuwa kwa nini wanaitwa hivyo, jibu ni kuwa malezi kama malezi kwao yaliwapita pembeni au waliyapiga malezi ya wazazi chenga, na pia mazingira, saikolojia na vingine vingi vinachangia katika kuwafanya watoto wawe walivyo kwa sasa. Hivyo twendelee kumwomba Mungu neema ili tufanye hayo yote kwa sifa na utukufu wake.

Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI YA JUU YA FAMILIA TAKATIFU YA YESU, MARIA, NA YOSEFU."

Chapisha Maoni