MAHUBIRI JUMAPILI YA 2 KWARESMA MWAKA A

MASOMO
1.Mwa. 12: 1-4a
2.2Tim. 1: 8b-10
3.Mt 17:1-9
TAFAKARI:  KUITWA KWA ABRAHAMU NA MUNGU KUWE MFANO WA KUIGWA NA SISI TULIO WAFUASI WA KRISTU.
Tukiwa tunaadhimisha dominika ya 2 ya Kipindi cha Kwaresma tunaalikwa kutafakari juu ya masomo yetu Jumapili ya leo. Tukianza na somo la kwanza tunamwona Baba yetu wa Imani, Abrahamu anaitwa na Mungu. Miaka takribani 1850 Kabla ya Kristu ilikuwa ni mpango wa Mungu kuleta mabadiriko katika Historia ya mwanadamu. Mungu alimchagua Abrahamu ambaye amekuwa Baba yetu kiimani ambapo kupitia kwake wokovu ulikuja duniani.
            Kipindi Abrahamu alichoishi kilikuwa ni kipindi ambapo nchi ya Mesopotamia ilikuwa nchi ambayo ilikuwa imeendelea kiuchumi, kitechnolojia, Kielimu na Pia ilikuwa ni nchi iliyojaliwa rutuba ya kustawisha mazao mbalimbali. Abrahamu mbali ya kukaa katika nchi iliyokuwa na maendeleo ya namna hiyo Abrahamu anaambiwa na Mungu kuhama nchi ile na kwenda nchi asiyoijua.Abrahamu baada ya Kusikia sauti ya Mungu anachukua uamuzi wa Kuhama nchi yake na kwenda nchi asiyoijua bila ya kusita.  Kwa macho na akili ya Kibinadamu siyo rahisi na si jambo jepesi  mtu kuacha nyumba yake, mali, na mfumo mzuri wa maisha na kwenda nchi isiyojulikana. Hapa twajifunza suala juu ya Imani, yaani kusadiki hata tusiyoona. Mungu anayetuita ndiye anayetuongoza na kutuonyesha mahala pa kwenda. Mungu atuitapo huwa hatuonyeshi njia mojakwa moja, Silaha ya Imani, Matumaini na Sala ni nyenzo Muhimu katika kutambua njia na kwenda ile nchi Mungu anapotuita kama Abrahamu alivyoitwa.
            Katika kutambua mwito wa Abrahamu kuitwa kufanya kazi ya Mungu, tunajifunza somo la maisha ya kujitoa na pia maisha ya sadaka kwa wengine. Tunaona katika somo la pili( 2Tim1:8b-10) Kipindi Timothi anahubiri Injili ya Kristo kule Ephesus mambo yalikuwa siyo salama na wale wote waliionyesha upinzani  katika Serikali ya Efesus hasa wahubiri Injili ya Kristu waliwekwa Kitanzini, hali hiyohiyo ndo Timoth anakumbana nayo kule Efeso. Mtume Paul anaandika barua yake ya kitume kule Efeso akiwafariji na kuwaambia kuwa “njia ya kumfuata Kristu changamoto hazikwepeki” Maisha ya ufuasi wa Kristu yanamadai yake ambapo pia na changamoto tunakabiliana nazo. Katika mazingira yetu tunaona sisi wakristu tunakumbana na changamoto ambazo zinakabili kanisa letu hasa hapa Tanzania kama vile Kuchoma makanisa moto nk.
            Kutoka somo la Injili ( Mt 17:1-9) tunaambiwa kuwa Yesu juu mlimani akiwa na wanafunzi wake alitimiza mapenzi ya Baba yake na kuonyesha kuwa yeye ndiye alikuwa ukamilisho wa yote yaliyofanywa na watangulizi wake, Musa na Manabii. Hapa tunaona Yesu akiwa na wanafunzi wake, Yohane, Peter, na James. Pia Yesu anaonekana kuwa na Musa, na Eliya. Yesu anageuka sura na kungaa kama jua. Swali la kujiuliza ni kuwa kwa nini Yesu anaonekana akiwa na Musa na Eliya? Hii ina maana kuwa Yesu amekuja kukamilisha Torati ( Musa) na Manabii( Eliya) Ni kwa msingi huo tunasema kuwa Kristu ndiye ufunuo wa mwisho wa Sheria( Musa) na Manabii( Eliya).  Kubadilika sura na kuwa mweupe ni ishara ya uwepo wa Mungu katika utu wa Kristu. Wingu jeupe lilowafunika ni Ishara ya uwepo wa Mungu. Tukumbuke katika kitabu cha Kutoka i.e, Kut 13:21, ilikuwa ishara ya Mungu kuwa alikuwa na watu wake. Musa alipopokea Sheria kutoka kwa Mungu pia kulikuwepo Wingu jeupe ambapo pia ilikuwa ni ishara ya kuwepo kwa Mungu  Kut 24:16-18.
            Kristu anapobadilika sura anatufundisha kuwa tuwe watu wa Mwanga na pia tuwe Mwanga kwa wengine( Matendo mazuri kwa wengine) na tusiwe watu wa giza. Kristu anangaa kama jua, kwa msingi huu ni kuwa yeye ni Jua la haki.

            Katika Injili ya Mt. Lk9:32 tunaambiwa  kuwa wakati yesu anabadilika sura kule mlimani alikuta wanafunzi wake wamelala( Peter, John na James). Ni mara ngapi tunakosa kuuona utukufu wa Mungu kwa sababu tunakuwa tumelala kiroho japo kimwili tu wazima. Kuna vitu vingi ambavyo vyaweza kutufanya kulala Kiroho, navyo ni maisha yasiyo na mwelekeo wa Kumtafuta Mungu Mungu, Maisha au njia za mkato. Anasa zaweza pia kutufanya tulale kiimani na hivyo kuusahau ule utukufu wa Kristu.

Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI JUMAPILI YA 2 KWARESMA MWAKA A"

Chapisha Maoni