MAHUBIRI YA JUMAPILI YA 4 YA MAJILIO MWAKA A


Masomo:
I.Isa.7:10-14
II.Rum. 1:1-7
III. Mt. 1:18-25
TAFAKARI: PALIPO NA MKONO WA MUNGU HAPAKOSI HAKI NA HURUMA.
Tunapotafakari juu ya masomo yetu ya leo, tafakari inayotuongoza ni kuwa palipo na Mkono wa Mungu hapakosi haki na huruma.  Katika somo la kwanza tunasikia Bwana akinena kwa mfalme Ahazi  kupitia kwa nabii Isaya “Tazama , Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanaume, naye atamwita jina lake Imanuel” Leo katika somo la injili hayo yaliyosemwa na nabii isaya yanatimia.
Katika somo letu la injili hatuna budi hasa kuwaangalia wahusika waliotajwa , yaani Yusufu na Maria.Tunaona wazi Yusufu alipokuwa akifikiria hayo Basi tazama malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto akisema Basi Yusufu  mwana wa Daudi usihofu kumchukua Mariamu Mkeo maana amepata Mimba kwa uwezo wa roho mtakatifu.(Yoh1:20) Tukitafakari zaidi maandiko haya matakatifu, kwanza tunakutana na jina ‘Yusufu’ likiwa na maana ya “Mungu atakuongoza”.  Katika maisha yetu sisi wakristu huyu Yusufu anakuwa kielelezo kwetu na tunajifunza yafuatayo kutoka kwake.
Yusufu, kadiri ya Sheria ya wakati ule ( Dt: 22:23-24) iliweka wazi na bayana kuwa kama mwanamke Bikira angelijiusisha na zinaa kabla ya kuolewa na akapatikana na mimba adhabu yake ilikuwa kupigwa mawe hadi kufa. Hivyo kadiri ya sheria hiyo Yusufu alikuwa na haki ya kumhadhibu mke wake ambaye kabla hajajihusisha naye alimkuta akiwa na mimba, kwa msingi huu Bikira Maria angelipigwa mawe hadi kufa, na Yusufu alijua hilo, ila yeye kwa hekima yake na huruma hakufanya hivyo, neno lilomwongoza asifanye hivyo ni kusikia sauti ya Mungu kupitia kwa malaika, hapa tunajifunza juu ya kutokuwa wepesi kuanika mabaya na mapungufu ya wenzetu ambao tunao katika jamii, kwani kila mmoja ana mapungufu yake na hakuna mkamilifu. Tukilitafakari jina Yusufu, yaani Mungu atakuongezea tunaona kabisa kwamba Yusufu kukubali ujumbe wa malaika wa kuwa usiogope, na kuvumilia kwake Yusufu ilikuwa ni mpango wa Mungu kutuletea Mkombozi, yaani Yesu Kristu.
Yusufu anatoa somo au fundisho kuwa binadamu hayupo kwa ajili ya sheria ila sheria ipo kwa ajili ya kumsaidia mwanadamu, na kama haiwezi pia sheria hiyo yaweza vunjwa. Hilo linajionesha pale Yusufu alipokuwa na moyo wa Huruma na uvumilivu kwa Bikira Maria alipokuwa na mimba ya mtoto yesu, kadiri ya sheria angelifanya kama ilivyotaka ,na Maria angelipigwa mawe hadi kufa, lakini kinyume chake Yusufu anahubiri huruma na msamaha,  na hili pia linajitokeza kwa Kristu mwenyewe ambaye alizaliwa naye akafanya matendo ya huruma jinsi hiyo, tukikumbuka pale yesu alipoletewa mwanamke aliyekamatwa kwenye uzinzi ili apigwe mawe kadiri ya sheria, kinyume chake yesu aliwageukia na kuwaambia waliomleta ili wampige mawe, kuwa  ambaye hana kosa au hajawahi kutenda kosa awe wa kwanza kumpiga Yule mwanamke, aliposema hivyo, hata hakuna aliyethubutu kumpiga Yule mwanamke. Hii inaonesha kuwa Kristu mwenyewe alikuwa ni mwanamapinduzi wa sheria zilizokuwa zipo kwa ajili ya kuwakandamiza watu.  Hapa tunapata fundisho nasi kuwa kabla hatujatoa hukumu kwa wengine nasi pia yatubidi tujichunguze na tuone pia madhaifu na mapungufu yetu.
Yusufu anatufundisha juu ya kupigana na kuondoa roho ya woga. Kuna Mhubiri mmoja alisema yafuatayo katika mahubiri yake:
“Siri ya kutoogopa ni kuelewa lile linalokuogopesha,” alisema Deborah Wiles. Alipokuwa akifikiria hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea ghafla katika ndoto, akasema: “Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumpokea Maria kuwa mke wako, maana mimba yake ameipata kwa uwezo wa Roho Mtakatifu:” (Mathayo 1: 20). Malaika wa Bwana anaufunua utambulisho wa Yesu na anamwezesha  Yozefu  kuelewa mpango wa Mungu wa wakovu. Nakubaliana na Corrie Ten Boom aliyesema: “Usiogope kamwe kuweka yajayo yasiyojulikana mikononi mwa Mungu anayejulikana.” Kazi ya Roho Mtakatifu ambaye ni Mkono wa Bwana ni kuelewesha: “Lakini atakapokuja yeye, Roho wa ukweli, atawaongoza katika ukweli wote” (Yohane 16: 13). Askofu wa kianglikana ilitokea akasoma insha juu ya ukoma. Alivutiwa kijifunza kuwa dalili ya ugonjwa ni kutokuwa na hisi katika sehemu zilizoathiriwa. Baadaye Askofu alihudhuria mhadhara na mke wake. Walikuwa wamekaa pamoja wakisikiliza kwa makini, ghafla Askofu alisikia mguu wake wa kulia ukiwa na mwasho. Mara moja aliinama na kujikuana, alishangazwa na kutohisi chochote. Askofu kwa hofu alimgeukia mke wake na kumnong’onezea, ‘Mpendwa, nafikiri nimepata ukoma! Nimejikuna mguu wangu hapakuwepo na hisi yoyote.” “Sifikiri kuwa umepata ukoma, mpendwa,”  alimhakikishia mke wake. “Mguu ambao umeukunakuna ni wangu, sio wako.”
Mwisho Yosefu anatupa fundisho juu ya kuwa watii na kutoa ushirikiano na Mungu. Mungu katika mipango yake na mwito wake kwetu sisi binadamu anatuita pia nasi tutoe ushirikiano naye. Mfano mzuri ni kama tulivyosikia jinsi Yosefu alivyotoa ushirikiano na Mungu katika kufanikisha mpango wa Mungu wa kutuletea Masiha ambaye tuna ngojea kuzaliwa kwake kati yetu. Yusufu hakushiriki kwa maneno hata kwa matendo, hili linajionesha katika injili ya  mtakatifu Mt.2:13-14, 19-23. Wagiriki huwa wanamsemo usemao kuwa “ Jifunze kutii kabla ya kuamrisha” Tunavyoongelea juu ya kusikia neno, kulitenda na kutii neno, hilo neno laweza kuwa ushauri wa wale waliotuzidi, sheria, sala, upendo, n.k , hivyo vyote tunaalikwa tuvizingatie na tuvitende katika maisha yetu tukiiga mfano wa Yusufu aliyesikia neno la Mungu na akatenda

Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI YA JUMAPILI YA 4 YA MAJILIO MWAKA A"

Chapisha Maoni