MAHUBIRI JUMAPILI YA 3 YA MAJILIO

MASOMO

I. Isaya: 35:1-6, 10
II. Jem:5:7-10
III. Matt:11: 2-11

TAFAKARI: UKUU KATIKA UTUMISHI WA KRISTU, NI PIA KUWA WADOGO KATIKA KUWAPA NAFASI WENGINE ILI WAMTUMIKIE KRISTU.

Katika enzi hizo kulitokea Mwandishi mahiri wa vitabu huko Amerika, naye jina lake aliitwa, Henry David Thoreau ( 1817-1862) ambaye katika moja ya maandishi yake aliandika insha yenye kichwa cha habari " Uvunjifu wa Haki za Raia" ( Civil Disobedience). Lengo lake yeye ilikuwa ni kutetea uhuru wa kila mtu kumiliki ardhi. Yeye katika insha hizo alizoandika alitumia mda wake mwingi kutofautisha kati ya ' haki' na 'Sheria' Kwa kipengele hiki yeye alisema kuwa haki kwa watu ndo fadhila ya msingi hata kuliko sheria, kwa kuwa sheria ingeliweza kuwepo lakini isilete haki au ikapindishwa kwa namna yoyote ambapo watu wasingelijua.
Thoreau, alifungwa gerezani kwa sababu ya misimamo yake ya kutetea haki za binadamu hasa kupinga biashara ya utumwa na kukataa kulipa kodi ambayo ilitumika kuendeleza biashara ya utumwa huko Mexico. Hivyo alivyokuwa gerezani amefungwa, alitegemea kuwa marafiki zake wangelikuja kumtembelea na kuunga mkono juhudi zake za kutetea haki za binadamu ili kuifanya serikali ibadilishe mfumo juu ya maslahi ya wanyonge na haki zao, kinyume chake ni kwamba,hakuna hata mmoja wa rafiki zake ambaye alithubutu kumuunga mkono, na baadala yake rafiki yake wa karibu, alilipa kodi baadala yake ili atolewe gerezani siku iliyofuata.
Wakati yupo Gerezani, mwandishi mwingine wa vitabu wa huko Marekani Jina lake Emerson, alimfuata, na kumwuliza ' Thoreau,Thoreau, kwanini upo Gerezani? na Thoreau alimjibu,'Emerson, Emerson, kwa nini uko nje ya Gereza?' Katika hadithi hii tunapata fundisho kuwa Thoreau alikuwa mpenzi wa ukweli, aliteseka kwa sababu alisimamia ukweli. Tujue kuwa kusimamia ukweli katika maisha ni mzigo mkubwa saa nyingine usibebeka, ni heli ukabebe mizigo mingine mizito kuliko kuubeba ukweli, japo kwetu wakristu, ndiyo msalaba na mzigo wetu tunaoitwa na Kristu tuubebe.

Katika Masomo yetu ya leo, yaani jumapili ya 3 ya Majilio tafakari yetu inaongozwa na maisha ya Yohane Mbatizaji kama tulivyomsikia kwenye somo la injili. Yohane Mbatizaji alikuwa mtu mmoja mtiifu juu ya ukweli. Yohane Mbatizaji alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa na msimamo ambao hawakupenda kuyumbishwa hata siku moja. Ni huyu huyu Yohane mbatizajia ambaye alimwambia ukweli Herode ya kuwa ilikuwa siyo halali kwake kumwoa mke wa ndugu yake. Na hatima ya ukweli huo aliisimamia hadi mauti yanamkuta gerezani ambapo alikatwa kichwa.

Yohane mbatizaji, alikuwa nabii wa manabii, au tuseme alikuwa nabii mkuu kati ya manabii, yeye alikuwa mtangulizi wa Massiah, ambaye alitabiriwa na nabii Isaya. Kuwepo kwa Yohane mbatizaji kuliashiria juu ya ujio wa Yesu Kristu Masiha. Leo katika tafakari yetu yatubidi tujifunze juu ya ukuu wa Yohane mbatizaji, utumishi wake, na udogo wake katika utumishi.
Kuzaliwa kwa Yohane mbatizaji kulienda sambamba na kuzaliwa kwa Yesu Kristu, kwa kuwa Malaika wa Bwana aliyetangaza kuzaliwa kwa Yesu Kristu, ni yuleyule aliyetangaza kuzaliwa kwake Yohane Mbatizaji. Alimbatiza Yesu Kristu, na Kristu mwenyewe alimtukuza akisema kuwa yu juu ya uzao wa wanaume wote aliyezaliwa na mwanamke.

 Mtakatifu Yohane Krisostom alimwita Yohane Mbatizaji nabii mkuu, kuliko wote kwa kuwa kati ya manabii hakuna nabii ambaye alitabiliwa na mwingine, na siyo kawaida kwa nabii kumbatiza Mungu, lakini huyu alifanya hivyo. Manabiii wote walihubiri juu ya Kristu, lakini hakuna kati yao ambaye alihubiriwa juu yake, ila Yohane Mbatizaji peke yake. Yohane mbatizaji alikuwa ni sauti iliyotangaza juu ya NENO wa Bwana japo yeye hakuwa neno.

Yohane Mbatizaji alikuwa ni kielelezo na mwanga kwa mataifa juu ya ujio wa Kristu, mwanga unaosemwa juu yake ilikuwa kurekebisha, na pia kukemea mabaya ambayo yalitendeka kwa wakati ule, ili kutayarisha mazingira ambapo Yesu Kristu Mkombozi angelizaliwa. Kwa maisha yetu sisi binadamu, ukiwa una mgeni anakuja, ni lazima ufanye usafi wa mazingira na pia nyumba, vilevile Yohane mbatizaji aliweza kuweka mwanga kwa jamii ya wakati ule, ili kusafisha, kuhakikisha kuwa maovu yote yaliyofanyika kwenye jamii yanakemewa, ili mwokozi alizaliwa azaliwe katika jamii iliyosafi.

Yohane Mbatizaji alikuwa na msimamo, kwamba hata yeye hakutikiswa na upepo, rejea Mt 11:7, ambapo katika bonde la Yordani kulikuwa na mianzi iliyotikiswa na upepo, kwa mantiki hiyo Yohane Mbatizaji hakuwa kama mianzi iliyotikiswa na upepo huku na huku, hii ikimaanisha kuwa alikuwa imara na hakuogopa macho ya watu, au maneno ya watu,  yaani uongo, majivuno, sifa za dunia n.k, alisimamia ukweli wa neno la Mungu.

Katika utendaji wetu wa kazi za kila siku iwe za kanisa, au serikalia au Familia yatubidi na tunaalikwa kuwa na msimamo. Hapa kuwa na msimamo pekee haitoshi, cha muhimu ni kuwa msimamo wetu unalenga na unajikita wapi? Yesu mwenyewe alikuwa na msimamo, kama tunavyosoma katika waraka wa mtume paul kwa wafilipi (filp2:5) " Iweni na Msimamo uleule aliokuwanao Yesu Kristu" Kama tulivyoona hapo awali, ni kuwa ukweli ni mzito na waubebao ni kundi dogo kati ya wengi, kama Yohane Mbatizaji alivyokubali kuubeba ukweli, basi nasi kwetu ni mwaliko kuwa katika hilo kundi la wachache ili kuubeba ukweli.

Mfano, Yohane mbatizaji ni tofauti na Yuda isikarioti, Yuda alimuuza Yesu kwa vipande thelathini vya pesa, alisimamia na kujikita katika tamaa na usaliti, alishindwa kusimamia ukweli, kikulacho kinguoni mwako, tamaa mbele, mauti nyuma.Yuda alikuwa kati ya Mitume kumi na wawili si kwa sifa ila kwa idadi, kimwili na siyo kiroho.

Kuna Methali inayosema " Mwenye nguvu mpishe" Methali hii inatutafakarisha juu ya ukomo wa mamlaka na uwezo wetu. Yohane pindi alipojua ujio wa Kristu, alinena mwenyewe kwamba" yu aja mtu ambaye sisitahili kulegeza kamba za viatu vyake" Tunaalikwa kumkaribisha Yesu Maishani mwetu maana yeye ni mwenye nguvu na jina lake ni kuu kuliko majina yote.Hoja zake zina nguvu, matendo yake yana nguvu. Yesu alisamehe dhambi, wakati Yohane mbatizaji hakuwa na uwezo wa kusamehe dhambi. Sifa mojawapo aliyobeba Kristu katika injili zote ni habari ya msamaha, na huu ndio ukuu wake. Rejea Mk 2:5 " Mwanangu umesamehewa dhambi" Kusamehe dhambi ni sifa ya Mungu. Na tunamwana Yesu hapa anasamehe dhambi.
Nasisi pia tunaalikwa kuwa na wajibu wa kuwa na sifa ya kuwa kiongozi bora na siyobora kiongozi. Kuna Muhubiri mmoja ambaye alisema " Yeyote atakaye kuwa kiongozi ni lazima sifa kubwa anayotakikana kuwa nayo ni nguvu, hii siyo nguvu ya kupigana bali nguvu ya ushawishi,nguvu ya maadili, nguvu ya uwajibikaji nguvu ya kushirikiana na wengine, nguvu ya mipango ya mipango ya kiuchumi, nguvu ya kutambua Mungu,na Nguvu ya kutopendelea upande wowote".( Rev. Fr. Faustine Kamugisha)
Katika Maandiko matakatifu, Yohane mbatizaji, alijiona kuwa nguvu yake ilikuwa na ukomo, hivyo akatoa nafasi kwa Kristu, ili Kristu aendeleze kazi hiyo. Kwenye jamii zetu wale ambao huwania uongozi kwa ngazi mbalimbali wapo tayari kuachia nguvu hizo au madaraka hayo kwa wengine ili nao waoneshe vipaji vyao katika uongozi? Kujikweza kimekuwa ni kikwazo kwa wengi kutopenda kuachia waliposhikilia ili wengine nao waongoze. Husuda na wivu ni vitu ambavyo pia vimejikita katika kuwafanya watu wasiachie madaraka kwa wengine. Katika Africa tuige mifano yaa baadhi ya watu ambao waliongoza na wakaamua kungatuka wao wenyewe kutoka kwenye uongozi bila ya shuruti, mfano, ni Marehemu Julius Kambarage Nyerere, Mwinyi, Rais Benjamin Mkapa n.k, Hivyo kuwepo Yohane Mbatizaji na sisi kwenye ngazi zetu za uongozi ni fundisho kubwa kuwa tujipime na tujue mwisho na upeo wa uwezo wetu katika maisha yetu ya Kijamii na Kiroho. 

Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI JUMAPILI YA 3 YA MAJILIO"

Chapisha Maoni