MAHUBIRI YA JUMAPILI YA 30 YA MWAKA C WA KANISA

MASOMO

1.Ybs 35: 12-14, 16-19
2.Tim 4:6-8, 16-18
3.Lk 18:9-14

TAFAKARI: UNYENYEKEVU KATIKA MAISHA YA MKRISTU NI NJIA ITUPASAYO KUMFUASA KRISTU.

Katika Masomo yetu ya Jumapili ya 30 Ya mwaka tunaongozwa na tafakari juu ya unyenyekevu. Kuanzia somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Yoshua Bin sira, tunasikia jinsi Mungu anavyokazia juu ya kuisikiliza sala ya mnyonge na myenyekevu asiye na majigambo, kiburi na majivuno."Mungu hatayadharau kamwe malalamiko ya yatima, wala ya mjane amwelezapo habari zake"(Ybs 35:14) hii ni kudhihirisha kuwa Mungu kwake kila mtu ana haki sawa mbele yake, na Mungu hana upendeleo kwani yeye ni Baba wa watoto wote, na kila mtoto mbele yake anahitaji haki sawa kama wengine. Katika Maisha yetu sisi wakristu tunaalikwa kutokuwa watu wa majivuno kutokana na kile ambacho tumejaliwa na mwenyezi Mungu. Mara nyingi kutokana na udhaifu wetu hii inatokea kwenye jumuiya zetu tunamoishi, makazini tufanyapo kazi na sehemu nyingine nyingi tunapojikuta hasa katika jamii iliyotuzunguka. 
Fundisho hili tunalipata kutoka katika injili ya Mtakatifu Luka 18:9-14 ambapo tunaona yesu anatoa mfano wa Farisayo na Mtoza ushuru walipokuwa wapo hekaluni wakisali. Kwanza kabla ya yote yatubidi tuangalie wasifu wa kila mmoja kati ya hawa waliotajwa kwenye injili. Kwanza, Farisayo, tujue kuwa  katika jamii ya Wayahudi alikuwa na wadhifa wa kuimarisha kwanza sheria za kiyahudi, na kuakikisha kuwa sheria ya Musa kwa vyovyote vile lazima izingatiwe.vilevile hawa mafarisayo walitetea sana imani juu ya ufufuko, kuwepo malaika na pia maisha baada ya kifo. kwa huo wasifu ni mzuri, ila cha Kujiuliza hapa ni kwa nini hawa walikuwa na mgongano na Yesu mbali ya kufuata sheria zote kwa umakini na ukaribu namna hii?? jibu ni kwamba sheria ilizingatiwa kinwyani na si kwenye matendo na  na maisha yao, na hii ndo ilimfunya yesu kuwapa changamoto ya kuishi kile walichohubiri. Tukiendelea zaidi hebu tuone wadhifa wa mtoza ushuru, watoza ushuru kadiri ya maandiko matakatifu hawa walionekana kama wadhambi kwenye jamii kwa kuwa walikuwa mara nyingi wanatuhumiwa kukusanya zaidi ya kile kilichohitajiwa na waajili wao, yaani serikali ya Kirumi kwa wakati ule, na pia hao walionekana kusaliti jamii yao waliyoishi kwa kuwa walishirikiana na utawala wa kirumi kuwanyanganya masikini hata kwa kile kidogo walichokipata ilibidi kitolewe kama ushuru kwa serikali ya warumi hata kwa shuruti. Hivyo kwa msingi huu, tunavyoona wadhifa wa kila mmoja hapa, Farisayo alivyojilinganisha na mtoza ushuru, alijiona yeye kuwa mbele ya Mungu hakuwa na dhambi. Kwa mantiki hiyo tunaona kwamba, huyu Farisayo hakwenda hekaluni kusali na kumwomba Mungu msamaha kwa yale mapungufu na makosa yake kama yule Mtoza ushuru, ila yaonekana alienda kujionesha na kumwambia Mungu juu ya kuwa yeye hana dhambi na yeye ni mwema daima. Farisayo anaamua kumweleza Mungu juu ya maisha na dhambi ya mtoza ushuru, kwa maana nyingine mfarisayo anatoa hukumu baadala ya Mungu, farisayo anaonekana kuchukua nafasi ya Mungu kuhukumu. Na sisi tujiulize swali kama hilo kwamba ni marangapi tunawafunga vitanzi shingoni wenzetu waonekanao kukosea kidogo katika familia zetu, makazini kwetu, mashuleni, na pia hata kanisani?? Je kati ya hawa wawili tunachukua pichagani au tunajifananisha na nani kati yao? katika jamii yetu ya sasa watu wametawaliwa na usemi wa bila ya mimi kitu fulani hakiwezekani, fulani hawezi kufanya kama mimi nifanyavyo etc, hayo yote ni matunda ya majivuno, na Kiburi, wakati vyote tujivuniavyo vyatoka kwa Mungu. Huruma ya Mungu hakika yahitaji unyenyekevu. Kuna hadithi moja iliyosimuliwa na Mhubiri mmoja aitwaye John Rose kutoka kule Bangalore, anahadithia kisa cha mtu mmoja ambaye alikuwa na busara sana na alimjua Mungu kuliko mtu yeyote kijijini kwake alipoishi, kwa hiyo huyo mtu siku hadi siku alijigamba kuwa yeye hakuna wa kumzidi kijijini kwake. Sikumoja Mungu akamtokea kwenye ndoto akamwambia kuwa aende kijiji cha jirani na atamkuta mtu mmoja ambaye ni Mkulima na maskini aishi kwake. Kweli huyo Bwana mwenye Busara alifanya kama alivyoambiwa na Mungu, alifunga safari na kuenda kukaa na yule mkulima. katika kukaa kwao, mwenye busara akagundua kuwa huyu mkulima kabla ya kwenda shambani husema neno Mungu nisaidie maramoja tu kwa siku, na pia hulisema hilo neno wakati wa kulala tu. Hivyo yule ndugu mwenye busara kuona hivyo alimwambia Mungu, kuwa ni vipi huyu mkulima hutaja jina lako mara moja mbili tu kwa siku, yaani kabla ya kwenda shambani, na kabla ya kulala? Mungu baada ya kusikia malalamiko ya huyu Mkulima akamwambia achukue ndoo na aijaze maziwa hadi pomoni na aanze kutembea mji mzima na ile ndoo imejaa maziwa hadi pomoni na ahakikishe kuwa hakuna hata tone moja la maziwa linadondoka chini, kweli ndugu mwenye busara alifanya kama Bwana alivyomwambia, na kurudi nyumbani jioni, tena Mungu akamuuliza, ni mara ngapi umenikumbuka katika safari yote ya kuzunguka na ndoo iliyojaa maziwa? mwenye busara akajibu " hata mara moja Bwana wangu" "akamwambi ningelikukumbuka vipi wakati uliniambia nichunge ndoo ya maziwa hata tone moja lisidondoke?" Mungu akamwambi kuwa mawazo yako yote yalimezwa na ndoo ya Maziwa uliyobeba kichwani na ndo maana hata hukunikumbuka au kunifikiria! Bwana akazidi kumwambia mwenye busara kuwa, "haya angalia huyu Mkulima ambaye na mbali ya kuelemewa na mizigo mingi ikiwemo kulima shamba, kuangalia familia yake watakula nini na wavae nini walau huwa ananikumbuka mara mbili kwa siku kuliko wewe ambaye umenisahau". hivyo hii inatukumbusha kuwa kujitukuza kunamfanya mwanadamu awe na kiburi na hatimaye anamsahau Mungu muumba wake. kama yule farisayo alivyosahau kwamba na yeye ni mdhaifu baadala yake akamhukumu mtoza ushuru machoni pa Mungu. Kwenye familia au serikali wengi tunaona huwa wanapenda wapewe nafasi za mbele na watukuzwe kwa sababu ya vyeo vyao walivyonavyo, na huwa wanapenda wapewe nafasi za pekee katika kanisa ili kutumia mwanya huo kutangaza sera zao ziwe ni mbaya au nzuri, si jambo la kuficha ni mambo ambayo yapo kwenye jamii. Ni mara ngapi tunaona wanasiasa wanatumia kanisa kama uwanja wa mapambano au majukwaa ya kisiasa?? Mbele ya Mungu sote tu sawa na kila mmoja ana hukumu yake. Wengi wetu tunajikuta tunachukua nafasi ya huyu Farisayo. Nabii Micah 6:8 anasema kuwa " mwenye haki, mwenye upendo na unyenyekevu" kuwa wanyenyekevu mbele ya Mungu, ndo kitu ambacho Mungu anahitaji kutoka kwetu. Njia ya mwenye majivuno mbele ya Mungu yaweza kulinganishwa na mtu mwenye baiskeli anataka kumgonga mwenye trekta, mtu mwenye majivuno mbele ya Mungu na mbele ya jamii huwa haishi kwa amani na wenzake, mnyenyekevu ndo huwa anainuliwa na Mungu kuwa mtumishi wake. Tukiendelea zaidi tunaona kuwa mawazo mazuri ya mtu au mawazo mabaya, yote hutoka moyoni mwa mtu. mtoza ushuru hali akijua yeye ni mwenye dhambi alijipigapiga kifua bila ya kuangalia mbiguni akimwambi Mungu kuwa yeye ni mkosefu, na Mungu akasikiliza kilio cha ombi lake. Ndugu zangu tunavyoendelea kutafakari masomo yetu ya leo hebu tuendelee kutafakari juu ya mioyo yetu iliyovunjika na kupondeka, tuzidi kumwomba Mungu neema ili atuimarishe katika sala tuache majivuno, kiburi na masengenyo juu ya wengine ambao ni marafiki zetu, au ndugu zetu tulionao kwenye familia zetu, makazini mwetu, mashuleni mwetu na kwenye jamii kwa ujumla. tujinyenyekeshe kwa Mungu tukijua kuwa pia na sisi tuwakosefu na twahitaji huruma ya Mungu na Neema zake ili kuweza kujua mapungufu yetu na tuweze kuyaungama kupitia sakramenti ya kitubio na hapo tutakuwa tumepatanishwa naye kama watoto wake.

Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI YA JUMAPILI YA 30 YA MWAKA C WA KANISA"

Chapisha Maoni