MAHUBIRI JUMAPILI YA 5 YA MWAKA B


1.Job 7:1-4
2.1Cor 9:16ff
3.Mk 1:29-39

TAFAKARI “ Kristo anateseka na wanaoteseka”
Tukianza tafakari yetu tunapoadhimisha jumapili ya 5 ya Mwaka B wa Kanisa hatuna budi kumshukuru Mungu kwa mema yake yote aliyotukirima katika wiki hii nzima. Katika masomo yetu yote ya jumapili ya tano ya mwaka wa kanisa hatuna budi kujifunza yafuatayo
Kujifunza somo kutoka maisha ya Ayubu na Yesu
Kutoka somo la Kwanza katika kitabu cha Ayubu tunasikia habari ya kuteseka kwa ayubu na mbali ya kuwa mcha Mungu, Mungu anampa majaribu ambayo yanaambatana na mateso ambayo Ayubu hakutarajia. Mungu anamruhusu shetani kumjaribu Ayubu. Marafiki zake Ayubu waonekana kumdhihaki na kumlaumu kuwa hayo yote yanampata kwa kuwa alimkosea Mungu, lakini Ayubu anaona hayo yote ni ubatili na utupu wa maisha.(Ayubu 8:13-19) “ Ndivyo ulivyomwisho wa wale wamsahauo Mungu, na Matumaini yake huyo mbaya huangamia (13).” Uthabiti wake utavunjika, na matumaini yake huwa ni nyuzi za buibui.”(14). Hayo yalikuwa ni maneno ya mmoja wa rafiki zake ayubu aliyeitwa Bildadi aliyonena wakati Ayubu yuko kwenye mahangaiko. Kutoka katika fundisho hili tunajifunza kuwa hata wale waonekanao kuwa ni marafiki waweza pia kuwa maadui wakati wa dhiki, waweza pia kunena mabaya juu ya wenzao walio katika dhiki au katika mafundisho kama tunavyoambiwa katika kitabu cha Ayubu juu ya rafiki zake.
Katika maisha yetu tunasikia historia ya yale yaliyotokea kwa Ayubu tuko mbali nayo kiwakati, ila nasi hatuko mbali na hayo yaliyotokea kwake bali tunayashuhudia katika maisha yetu wenyewe, tunashuhudia watu wasio na hatia jinsi wanavyoteseka, tunashuhudia ndoa zinavunjika, tunashuhudia maovu ya kila aina yanaendelea katika jamii zetu na hasa katika mifumo mbalimbali ya utawala, tunashuhudia mifumo mibovu ya kiuchumi, tunashuhudia umwagaji wa damu kwa sababu ya uchu wa madaraka kwa baadhi ya watu. Dunia tunayoishi kwa sasa inaningia juu ya utovu wa maadili ambapo tabaka za wanyonyaji, wala rushwa, wanafiki na wavunja amani zinatawala.
Katika maisha yetu kama wakristu tunaweza tukasema nini juu ya habari ya Ayubu kulingana na imani yetu na hali zetu za maisha?? Tuna nini la kusema kwa ndugu zetu walio katika vilio na majonzi kwa sababu ya maisha? Huzuni, kilio na machungu ni moja ya sehemu ambazo tunazikuta hasa katika ujumbe wa neno la Mungu; hilo pia tunaliona kinywani mwa Bwana wetu Yesu Kristu ile siku ya ijumaa kuu (Lk 23:34). Katika dunia Yetu ya leo tunasikia vilio vingi mno tunaishi katika dunia iliyojaa kelele za majonzi, sisi kama wakristu tunaitikia namna gani kwa watu wenye majonzi na vilio?
Katika somo la injili tunaona wenye magonjwa mbalimbali wanaletwa kwa Yesu akawaponye, na mara moja Yesu bila ya kuuliza nini maana ya mateso katika maisha anawaponya. Kama wakristu, na wafuasi wa Kristu tunaalikwa kufanya kama Kristu alivyofanya, tunaalikwa kuwa waponyaji wa roho na mwili, na kweli hili linawezekana. Uwepo wetu kwa wale wenye masumbuko ya kimwili na kiroho ni faraja kubwa sana kwao hata kuliko chochote kile, maneno yenye faraja, na ushauri mzuri kwao ni njia mojawapo ya kuponya wenzetu wenye mahangaiko katika maisha. Hasa tunaalikwa kuwa karibu na wale waliopoteza imani kwa Kristu na matumaini kuwafariji ili wapate kumrudia Mungu muumba wao, hayo yote yanawezekana pindi tukimwachia Kristu Yesu atawale katika mioyo yetu na atutumie kama vyombo vyake ili kufanya utawala wake uenee duniani kote.
Maandiko matakatifu leo yanatupa motisha kuwa tuwe daima watu wa kusikiliza wenzetu walio katika raha na pia katika unyonge (upweke,utupu wa maisha- waliokosa ajira, walioonewa, wagonjwa n.k,), tumwombe Mungu awabariki hao wote wenye kusumbuka kupitia vinywa vyetu na mikono yetu.
Ishara ya uponyaji wa Mungu
Kuna mjadala ambao huendelea kwa baadhi ya watu hasa wale walioshikilia msimamo wa kisayansi na kipagani kuhusu uponyaji wa Yesu kwa watu waliokuwa wagonjwa, mawazo ya watu kama hawa ni kuwa, je Yesu aliweza kabisa kuponya wagonjwa wa mwili au aliponya wale waliokuwa na pepo peke yake? Mjadala kama huo haufai na uko nje ya malengo ya imani ya Kikristu. Ukweli ni kwamba Kristo aliponya mwili na roho. Kristu anavyofanya uponyaji hafanyi huo uponyaji kama miujiza ili kushangaza watu, Kristu anafanya miujiza kuonyesha huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake, pia uponyaji aliofanya Kristu ilikuwa ni ishara kuwa mkono wa Mungu daima upo unafanya kazi daima duniani.
Ilitokea siku moja madaktari walikuwa na maongezi juu ya uwezo wa sala kuwasaidia wagonjwa kupona,waliuliza swali kuwa sala inatenda zuri lolote kwa wagonjwa?kundi moja la watu waliokuwepo hapo, walisema kuwa “ sala huwa inasaidia wale wanaosali kujisikia kuwa wanafanya kitu kwa mgonjwa, ila haimsadii mgonjwa kupona kamwe.” Kundi jingine la watu lililokuwepo lilisema “ sala kimsingi inamsaidia mgonjwa kupona.” Kundi la kwanza lilipinga kundi la pili kwa kusema hii kisayansi haiwezekani haiwezi thibitishwa kamwe. Hivyo ilibidi ifanywe jaribio kuthibitisha kama sala yawezekana ikamfanya mgonjwa akapona. Jaribio hili lilifanywa kwa wale wagonjwa wa moyo. Hivyo ilichukuliwa shauri kuwa baadhi ya wagonjwa wa moyo waombewe bila ya wao kujua kuwa wanaombewa na pia kuwafanya wanaowambea wasijue ni nani wanamwombea. Hivyo waombaji walipewa idadi ya watu waliopaswa kuombewa bila ya kuwafahamu, na madaktari waliokuwa wanatibu hao watu hawakuwafahamu kama walikuwa wanaombewa. Nini kilitokea? “ ona waliokuwa wanaombewa walipona haraka” lilisema lile kundi lilokuwa linadai kuwa sala ina matokeo mazuri kwa mgonjwa, tukimtanguliza Mungu mbele kuna makubwa yapatikanayo kuliko kuitanguliza sayansi.
Imani na msalaba wa Kristu
Kila mmoja wetu kwa namna moja au nyingine anajua ninini maana ya mateso iwe ni mateso ya kimwili, kihisia, kiakili au kiroho. Hakuna namna ambayo mateso yaweza kuzuilika maana ni sehemu ya asili na maisha yetu. Twaweza jiuliza kuwa mateso kadiri ya imani yetu yanatufundisha nini?? Mateso huja kwa namna nyingi na huja katika hatua mbalimbali katika maisha ya mwanadamu, mateso yaweza kuja wakati wa utoto, ujana, au katika uzee. Mateso yako ya namna nyingi ila hatuna kipimo na hayawezi pimwa kwa kipimo chochote kile. Kilio na machozi ya Ayubu kama tulivyosikia katika somo la kwanza ni kilio ambacho mateso yake hayana mbele wala nyuma ila limebaki kama fumbo. Ayubu baada ya kupata hayo majaribu na mateso yote anaonekana kumsahau Mungu. Ayubu alikuwa akiishi maisha ya kumcha Mungu, sasa anashangaa kwa nini Mungu analeta hiyo mikasa katika maisha yake na familia yake. Mungu ambaye alikuwa kama rafiki yake wa karibu sasa anaonekana kama adui. Kadiri ya mazoea mikasa na matatizo hasa ya kiwemo yale ya kiafya, kifamilia, na kiuchumi huwa yanawafanywa wengi wamsahau Mungu na kukimbilia miungu wengine ikiwemo pia kubadili madhehebu. Ayubu ni kielelezo cha kila mwanadamu. Ni kielelezo kinachoonyesha binadamu akiwa katika mwanga na akiwa katika giza pia. Hasa ni kielelezo kinacholenga sehemu ya giza(kumweka Mungu pembeni mbele ya shida) ya mwanadamu duniani.

Imani na msalaba wa Kristu ni vitu visivyoweza kutenganishwa. Ni chini ya msalaba wa Kristu imani yaweza kuimarika. Kristu mwenyewe alishiriki kikamilifu mateso ya mwanadamu. Kristo alikubali kuubeba udhaifu wetu sisi binadamu. Msalabani tunaona Kristu ndipo Kristu alipoonyesha upendo na unyenyekevu wake. Pale msalabani tunamwona Yesu akilia “ Mungu mbona umeniacha”( Mt 27:46), kilio hicho ni tendo la kiimani, ni lugha ya kiimani hasa pale unapohitajika msaada wa Mungu pindi giza likitawala katika maisha ya kila mmoja wetu. Mungu hakumwacha Yesu ateseke, bali kuteseka kwake ndo kumeleta uzima kwa watu wote duniani. Hivyo tunavyoadhimisha jumapili ya tano ya mwaka B mwaka wa Kanisa, hatuna budi kutambua kuwa katika magumu yetu yote kristu bado hajatuacha bado anatembea nasisi kutufariji.

Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI JUMAPILI YA 5 YA MWAKA B"

Chapisha Maoni