MAHUBIRI YA JUMAPILI YA PILI YA MWAKA B


MASOMO
1.      1Sam 3:3-10,19
2.      1Kor6:13-15,17-20
3.      Yn 1:35-42

Tafakari “ Njoo nanyi mtaona”
Tunavyoadhimisha jumapili ya 2 ya mwaka B wa Kanisa tunaongozwa na tafakari isemayo “ njoo nanyi mtaona” hii ni tafakari inayotutafakarisha juu ya maisha ya kumfuasa Kristu anawaambia wafuasi wake kuwa waende nyumbani kwake wakaone.
Katika kuenenda na kukaa katika nyumba ya Bwana ni lazima tutambue na tujiulize swali moja  kuwa kwa nini  Kristu anawaambia wanafunzi wake ya kuwa nao waende wataona? Anawaambia hivyo kusudi wapate kuona, kusikia na kujifunza anawaambia waone ili wapate kuwa si ili mradi wafuasi bali wapate kuwa wafuasi wazuri.
Tunaambiwa kuwa katika maisha ya ufuasi wa Kristu lazima pawepo mwongozo na kiongozi, pawepo mtu wa kuelekeza namna ya kufanya, katika maisha ya kiroho lazima pawepo mwongozaji na zaidi ya hapo ni lazima pawepo mpatanishi. Hivyo ni mwaliko na wajibu wetu kuwa kabla ya kufanya utume wetu, kumtangaza Kristu, na kuwa tayari kutumwa na yeye, ni lazima ni lazima kwanza kuona kristu anavyofanya, kujifunza na kufundishwa namna ya kufanya. Bwana aliwaita wanafunzi wake waone , wajifunze na wafundishwe. Hivyo Kristu anavyowaambia wanafunzi wake kuwa “ njoo nanyi mtaona” alitaka waone kuwa nyumba aliyokuwa anakaa lilikuwa siyo jengo bali ilikuwa nyumba ya roho, ilikuwa siyo nyumba iliyojengwa kwa mawe, matofari na mbao bali ilikuwa nyumba iliyojengwa kwa mikono ya mioyo safi na myeupe. Hivyo twaweza sema kuwa ni kwa msing huu Nazareti nyumbani kwa Yesu ni shule inayofundisha ukimya, na namna ya kutengeneza maisha ya pamoja, ikiwemo maisha ya familia. Kristu anawaita wanafunzi wake wajifunze shule ya upendo, uvumilivu, ukimya, ukarimu, na fadhila nyinginezo. Maisha kuanzia katika familia ni pale ambapo tunaona na kugundua karama na vipaji mbalimbali. Ili kuweza kufanikisha hilo ni lazima kuwa katika umoja, kuwa na roho ya ushirikiano katika kuhakikisha kazi na neno la Mungu linaenda duniani kote.
Tunavyosikia Kristu akiwaita wafuasi wake waende waone nyumbani mwake, hapa yatubidi tutofautishe nyumba na jengo. Nyumba imejengwa kwa upendo, heshima, upole, na utii, wakati jengo  limetengenezwa kwa matofali na mawe.  Katika nyumba ya Kristu wanafunzi wake walijifunza shule ya utii na hili andiko limedhihirishwa katika maandiko matakatifu kama yasemavyo “ akashuka pamoja nao akafika Nazareti na aliwatii”(Lk2:51). Yesu alipowaambia wanafunzi wake  “ njoo muone waliona pia utii wake kwa mama yake Bikira Maria, waliona upendo wake na pia wakaona upole wake. Katika nyumba kuna upole sauti kubwa haimlei mtoto ( Fr. F.Kamugisha). Jengo ni kwa ajili ya watu na nyumba ni kwa ajili ya binadamu. Binadamu ni wachache lakini watu ni wengi, kuwa mwanadamu maana yake ni kuishi fadhila za kiutu, yaani kuwa na fadhila ya upendo kama wa Kristu, fadhila ya shukurani, fadhila ya uvumilivu, na fadhila ya upole kama ilivyosemwa hapo awali.
Kuna mhubiri mmoja katika mahubiri yake alipata kusema “ Familia ya Yesu, Maria na Yosefu ilikuwa ni Nyumba na si jengo, ilikuwa familia ya binadamu, jengo wanapokaa wezi wanyanganyi wa kutumia silaha, makahaba, wachonganishi, waongo, wafanya mipango mibaya hilo ni jengo siyo nyumba.” Jengo hutoa ulinzi wa namna moja, lakini nyumba hutoa ulinzi wa kimaadili, kisaikolojia, kimwili , kiroho na kidini. Haya maneno yamethibitishwa na kudhihirishwa na maandiko matakatifu kama yasemavyo “ Bwana asipoijenga nyumba waijengao wanafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji waulindao hufanya kazi bure ( Zab127:1)
Tunafundishwa somo la kuwasikiliza walezi ( wazazi, ndugu, jamaa na walimu wetu) kwa kuwa kupitia kwao Mungu hujifunua  kutuonyesha njia ya kwenda, mfano kutoka somo la kwanza kutoka kitabu cha Samweli tunaona Samweli alikua na kulelewa na Eli ambaye alikuwa kuhani, na Samweli alikuzwa katika malezi ya kiroho na huyu kuhani Eli hivyo Samuel alikuwa amejaa ufahamu mwingi juu ya mambo ya dini na mambo ya Kiroho. Cha kushangaza  ni kuwa na mbali ya kuwa na ujuzi na ufahamu juu ya mambo ya Kiroho, tunaona Samweli bado anashindwa kuitambua sauti ya Mungu kuwa ndiye aliyekuwa akimuita na baadala yake anafikiri kuwa Eli ndiye aliyekuwa akimwita. Hivyo kwa msingi huu tunapata mwaliko kuwa kuitambua sauti ya Mungu ni lazima kuhitaji msaada na usaidizi kutoka kwa watu tunaoishi nao nyumbani mwetu. Vivyo hivyo katika injili ya leo tunaona jambo la namna hiyo kwamba Yesu anawaita mitume wajifunze kutoka kwa Yesu  kama tulivyosikia hapo kabla. Wanafunzi wa Yesu walikuwa na mwito wa kumtumikia Mungu ila walihitaji maelekezo ili kufikia lengo lao la kumtumika Mungu na ni kwa msingi huu tunaona Kristu anawaita ili waone na wakajifunze kutoka kwake namna ya kumtumikia Mungu na kutimiza mapenzi yake.

Ni mwaliko kwa kila mmoja wetu, kuwa tayari kujifunza, kupata maelekezo ya kiroho kutoka kwa viongozi wa kiroho, hasa kuishi maisha ya Sakramenti, kufuata amri za Mungu na amri za Kanisa.

Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI YA JUMAPILI YA PILI YA MWAKA B"

Chapisha Maoni