MAHUBIRI JUMAPILI YA 29 MWAKA A WA KANISA KIPINDI CHA KAWAIDA



MASOMO
1.      Isaya 45:1. 4-6
2.      1Thes 1:1-5b
3.      Mt 22: 15-21
TAFAKARI “ Tusichanganye Serikali na Mungu
Tunavyoadhimisha jumapili ya 29 Ya mwaka wa Kanisa, tunaalikwa kutafakari kwa kiundani juu ya nini tumepewa na Mungu na tunarudisha kwa Mungu. Pia katika jumapili hii tunaalikwa pia kujiuliza hili swali kuwa tunatoa nini katika serikali zetu.
Tunaona waandishi na Mafarisayo wanatoa swali lenye utata kwa Yesu juu ya kulipa Kodi kwa Kaisari au kutolipa kodi kwa kaisari, hivi na sisi tujiulize kuwa hili swali lilikuwa linamadhumuni gani na lilikuwa lina lenga nini hasa kwa Yesu? Na hili swali pia kwa maisha yetu na wakati wetu lina maana gani?
Tukianza kabisa kuchambua swali ambalo Yesu aliulizwa twaweza tambua maramoja kuwa kumbe hili lilikuwa ni swali tata na pia swali mtego kwa Yesu, tujiulize pia kuwa lilikuwaje swali tata na lenye mtego kwa Yesu? Jibu ni kwamba swali aliloulizwa Yesu lilikuwa tata kwa kuwa majibu ambayo angeliyatoa ndo yangelimwingiza kwenye matatizo makubwa ambayo yasingelitarajiwa. Lilikuwa ni swali mtego kwa sababu, kama Yesu alivyoulizwa na hao mafarisayo juu ya kulipa Kodi au kutolipa Kodi kwa Kaisari, Yesu angelitoa jibu la ni halali kulipa kodi kwa Kaisari ina maana kwamba ingelionekana kuwa alidharau dini ya wayahudi na pia kuzarau taifa lao na hivyo kukumbatia utawala wa kikoloni wa warumi, hivyo machoni pao ingelionekana kuwa amewadharau, pia kama angelijibu hilo swali kuwa ilikuwa siyo halali kwao kulipa kodi kwa Kaisari, hii maana yake ingelionesha kuwa Yesu alidharau mamlaka na Serikali ya Kirumi, na ni kwa msingi huo hao wafarisayo wangelipata nafasi ya kumshitaki kwa hayo mamlaka kwa kuonyesha dharau ya kutoheshimu hayo mamlaka. Ni Kwa msingi huu tunaona Yesu Kwa hekima yake anawajibu kuwa “mpe Kaisari yaliyo ya Kaisari na pia mpe Mungu yaliyo yake Mungu” ( Mt 22:21)
Hii inamaanisha nini? Maana nyingi sana zimetafsiriwa juu ya haya maandiko, na ni kwa msingi huu kuwa wengi hasa viongozi wa serikali hualalisha yasiyoweza kuhalalishwa kwa kifungu hiki kidogo cha maandiko matakatifu, mfano utasikia wengine wanasema kuwa dini isiingilie serikali, na pia dini nayo inasema serikali isiingilie dini kamwe. Ni kwa msingi huu tunaona kuwa dini inaweza kutumika kama mvuli wa kutenda maovu, kwa kisingizio kuwa serikali isiingilie dini, na vilevile serikali inaweza kutumia mumvuli wa kutenda maovu dhidi ya wananchi wake na kushutumu viongozi wa dini wasikemee maovu ya viongozi wa serikali kwa kubainisha kuwa dini haina la kusema juu ya serikali
Kristo anavyosema kuwa “ mpeni Kaisari yaliyoyake Kaisari, na Mungu yaliyoyake Mungu anamaanisha kuwa kama vya Kaisari ( Mamlaka/ Serikali) vinatumika kwa ajili ya manufaa ya pamoja ( Common good) na kwa ajili ya maendeleo yetu, basi itakuwa siyo halali kutumia hivyo vya kaisari bila ya kuwajibika kuvilipia kodi, na pia ni mwaliko kwa wakristo kuheshimu madaraka na mamlaka ya tawala hapa duniani, kwa maana kama Kristo mwenyewe aliheshimu hayo mamlaka kwetu inakuwaje? Hakuna sababu ya msingi ambayo inaweza kuhalalishwa na dini kuharibu au kuiba mali ya Serikali kwa kisingizio kuwa dini na serikali haviingiliani. Ni mwaliko na ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa mshikamano na ushirikiano upo katika kujenga tawala na serikali zetu. Jibu la Yesu kwa wafarisayo linatoa ushuhuda kuwa nayeye anatambua umuhimu wa mamlaka na utawala wake. Kila kitu tulichonacho kinatoka kwa Mungu hivyo hatuna budi kutii hayo mamlaka.
Tunaona kwamba Yesu anapotoa jibu kwa mafarisayo kwa kuwauliza juu ya picha iliyochorwa juu ya hela wanajibu kuwa ni picha na sura ya Kaizari. Sisi vilevile kama wana wa Mungu tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ( Mwanzo 1:27) hivyo kama Kristo anasema kuwa “ Kaisari arudishiwe vilivyovyake, na Mungu apewe vilivyovyake” tunapata somo juu ya Kuheshimu mamlaka na pia kumrudishia Mungu kile alichokiumba kwetu kikiwa na sura yake.  Tunaalikwa kuheshimu utu wa binadamu, hasa kuheshimu wale wote ambao katika jamii hawana wa kuwatetea, hasa watoto yatima, kuepukana na unyanyasaji hasa kwa  wakina mama wajane,maskini wasiojiweza, na pia kuheshimu sura ya nchi na uasili wake. Tukifanya vile ni kuwa tutakuwa tunamrudishia Mungu na kumshukuru kwa yale yote aliyotukirimia kama watoto wake.
Tunavyomrudishia Mungu aliyotukirimia pia inabidi tumshukuru, Mhubiri mmoja alipata kutoa mfano wa kushukuru, naye si mwingine bali ni Fr. Faustine Kamugisha na alikuwa na haya “ Siku ya Kushukuru iliyvokuwa imekaribia wanafunzi wa darasa la awali- Chekechea waliambiwa kuchora picha ya kitu ambacho katika maisha yao kiliwasaidia sana na hivyo wamshukuru Mungu kwa kitu hicho, baadhi ya wanafunzi walichora gari, ndege, chakula, kinyago n.k, lakini mtoto mmoja alichora mkono. Wanafunzi wenzake walianza kujiuliza ni mkono wa nani?, wa Mungu? Mkono wa Polisi? Mkono wa Mkulima? Hakuna aliyeweza kutoa jibu sahihi. Wakati wa mapumziko mwalimu alimwendea mwanafunzi huyo na kumuuliza. “Mkono huu ni wa nani?” mwanafunzi wa darasa la awali alijibu “ ni mkono wako mwalimu.”(Fr.Kamugisha) Mwalimu alitokwa na machozi alivyokumbuka alivyokuwa anamsaidia mwanafunzi huyo kuvuka barabara akimshika mkono kwa vile alikuwa ni mlemavu wa mguu pia alimshika mkono kumsaidia kuandika a, e, i, o, u.” Ni kwa msingi huo Mungu anatushika mkono tutoke katika mlango wa majaribu
Mungu apewe kipau mbele. Hata Kaisari alikuwa mtawaliwa kwa Mungu. Viongozi kama binadamu wengine wote wako chini ya Mungu kuna wakati watatakiwa na Mungu kutoa hesabu kwake. Mchungaji mmoja alikuwa anahubiri na akakazia mambo matatu “ jipatie unayoweza kuyapat”Mkristu mmoja mzee kiumri lakini tajiri alisema “ Amina.” Baadaye mchungaji alisema  “ Tunza yote kadiri unavyoweza.” Yule mzee alisema tena “ Amina.” Mchungaji alisema pia  “ Toa yote kadiri unavyoweza.” Mzee alisema, “ Hii ni aibu unaharibu mahubiri mazuri.”( Fr. Faustine Kamugisha)

Related Posts:

0 Response to "MAHUBIRI JUMAPILI YA 29 MWAKA A WA KANISA KIPINDI CHA KAWAIDA"

Chapisha Maoni