Masomo.
I. Kut 17:3-7 II. Rum 5:1-2, 5-8 III. Yn 4:5-42
TAFAKARI:
“KRISTU NI MAJI YA UZIMA.”
Tunapoadhimisha
Jumapili ya 3 ya Kwaresma hatuna budi kumshukuru Mungu kwa yale yote ambayo
ametutendea katika kipindi kizima cha wiki tuliyomaliza.
Tukianza tafakari yetu
kutoka somo la kwanza ( Kut 17: 3-7) tunaona Waisrael wakiongozwa na
Musa kupita Bahari ya Shamu wakienda ile nchi ya ahadi wakipitia jangwa la
Sinai. Mwanzoni mwa safari yao mambo yanaonekana kuwanyokea na wanapata uhakika
kuwa Mungu yu Pamoja nao Katika safari yao na pia wanakuwa na furaha kwa kuimba
nyimbo za furaha. Kadiri safari inavyoendelea kumbe mambo yanabadilika kinyume
cha matazamio yao, katika hiyo safari wanaanza kukumbana na changamoto za kila
aina kama vile joto kali njiani wanakumbana na wanyama kama vile nyoka wakali,
na pia wanakuwa na kiu jangwani, sehemu ambayo ni kame na haina maji. Ni Kwa
msingi huu tunaona wana wa Israel wanaanza kumhisia Mungu vibaya na
wanaanza kuwa na mashaka naye. Wanaanza
kuwaza Mungu kuwatoa utumwani Misri ilikuwa ni mbinu ya Mungu ya Kuwaangamiza.
Mungu kweli yu pamoja nasi? ( Kut 17:7) Sehemu ambapo haya yote yanafanyika paliitwa
“ Massah – Meribah” Kwa Kiebrania maana
yake “ Majaribu”
Haya yaliyowapata wana wa Israel katika maisha ya Mkristu
pia hayakosekani. Kama wao tunaambiwa kuacha maisha ya utumwa wa dhambi na
kumrudia Mungu. Wengine kati yetu ni Wakatekumeni, ambao watakuwa wana wa
Kristu kupitia ubatizo. Tukishabatizwa huwa tunafikiria kuwa ndo mwanzo na
mwisho wa shida zote, kwa kuwa tunafikiria kuondolewa dhambi zetu. Mara
nyingine kama mambo hayajaenda salama huwa tunamgeuzia mgongo Mungu. Ni kwa
msingi huo sisi changamoto tukumbananazo huwa tunafikia hatua ya kumweka Mungu
Pembeni na kufuata njia nyinginezo.
Katika somo la pili ( Rum 5:1-2. 5-8) tunaambiwa kuwa
fadhila ya matumaini haipatikani katika yale tuyafanyayo, mf, matendo mema,
bali fadhila hiyo hupatikana kutokana na Roho ya Mungu na Upendo wake. Mungu
upendo wake ni tofauti na sisi tufikiriavyo. Mt. Paul anasema “ Matumaini yetu
siyo danganyifu si kwamba sisi tu wema, lakini kwa kuwa Mungu wetu ni mwema (
Cf. Rum 5:1-2)
Kutoka somo la Injili tunaona Yesu akiwa amechoka na
anakaa Kisimani kuwasubiri wanafunzi wake walioenda kutafuta chakula. Kisimani
tunaona pia mwanamke anakuja kuteka maji, Yesu anamuulizia Yule mwanamke maji
ya kunywa. Yule mwanamke anamshangaa Yesu kumuulizia maji ya Kunywa kutoka
kwake. Sababu ya kushangaa Yule mwanamke ni kuwa yeye alijua wazi kuwa yesu
alikuwa ni Mgalilaya, lini na wapi Mgalilaya akaulizie kitu kutoka kwa
Msamalia??na Kwa nini Yesu alivunja mila ya Wayahudi iliyokataza kwa wakati ule kuongea na mwanamke
asiyemjua sehemu faragha! Walimu wa Kiyahudi ( Rabbi) kwa wakati ule
waliweka taratibu kuwa kama mwanaume
ingelitokea akakutana na mwanamke hakuruhusiwa kuongea naye kwa muda mrefu.
Wanafunzi wake Yesu nao wanashangaa kuja na kukuta Yesu anaongea na Yule mwanamke??(
Msamaria). Fundisho: “Upendo wa Kristu
unaenda hadi nje ya Mipaka ya Binadamu Kristu anachotaka kutoka kwetu sisi
wafuasi wake ni kile kitokacho moyoni na
siyo kutoka katika mwonekano wa nje.”
Tuone kidogo juu ya huyu mwanamke.Mwinjili Yohane hapa
anatuletea mwanamke ikiwa ishara ya jambo Fulani. Kisima katika Biblia ni ishara
ya mahali pa makutano kwa watu wanaopanga
kuoana. Katika kitabu cha agano la Kale Isralel ni Ishara ya Bibi arusi na
Mungu akiwa Bwana arusi. Hivyo Israel ni mchumba wake Mungu. Israel kama
mchumba wake Mungu, ni mara ngapi huyu mchumba amefarakana na Bwana arusi
wake?( Mungu) ni mara ngapi huyu Bibi arusi amefarakana na wamisri, wagiriki,
wa Babuloni, wa Persia na Warumi?
Injili ya Mt. Yohane inatuonyesha jinsi Kristu alivyo
Bwana arusi kwa watu wake ambao ni wakosefu,
huyu Bwana arusi anakuja kurudisha urafiki wa binadamu na Mungu ulioanguka kwasababu ya dhambi. Katika Injili tumesikia
kuwa wanafunzi wa Yesu walienda kutafuta chakula. Mwanamke alikuja kuteka maji
kisimani. Kristu anachakula na maji ya uzima ambayo wao hawayajui ( Yn
4:10,30). Mwanamke anaenda Kisimani kilasiku kuteka maji kwa kuwa maji
atafutayo kila siku hayawezi kuzima kiu yake ya kweli. Maji katika kisima ni Ishara ya starehe, na anasa za kila namna
ambazo watu hutafuta kutoshereza mahitaji yao ya kimwili. Starehe na Anasa haviwezi kutuletea uzima wa milele. Ni upendo
na Roho ya kimungu viletavyo raha ya milele.
Maji ya uzima ambayo Kristu anayasema ni Roho ya Kimungu
na Upendo wa Kimungu nafsini mwetu ndo vyaweza kuleta uzima wa milele. Mwinjili
Yohane anatuambia kuwa mwanamke anaacha jagi la maji na anaonekana kugundua
maji ya aina nyingine. Katika mazungumzo yao, yaani Yesu na yule mwanamke
Msamaria, mwanamke anaonekana kuwa na
hamu na shida ya maji ya kunywa, na anaonekana kuridhishwa na raha, na Starehe
za dunia. Polepole mwanamke anakuja kuelewa kuwa Kristu anataka nini kutoka
kwake. Mwanamke msamaria baada ya
kugundua na kuelewa taratibu nini Kristu anataka kutoka kwake anaanza
kubadilisha mtazamo wake na mawazo yake juu ya Kristu. Mwanzo kabisa mwanamke Msamaria anapokutana
na Kristu anamchukulia kama Myahudi na
mpita njia ( Yn 4:9) Baadaye anamtambua kama “ BWANA” ( Yn 4:11). Baadaye kama
nabii ( Yn 4:19), na baadaye kama Masiha ( Yn 4:19). Baadaye mbele ya watu wote
yule mwanamke Msamaria anamtambua Yesu kama mwokozi wa Dunia (Yn 4:42)
Kwetu sisi sote na Wakatekumeni wanaojiandaa kuwa wana wa
Kristu kwa njia ya ubatizo, hivyo ni mwaliko kwetu kuwa na imani na kumfuasa
Kristu tukifuata mfano wa mwanamke Msamalia alivyofanya kumtambua Kristu na
kumfuata.
Kwa upande wetu sisi wakristu tunakutana na Kristu wapi??
Tunakutana naye sehemu nyingi sana, mf. Katika maeneo yetu ya kazi, njiani, na
katika nyanja mbalimbali za maisha hasa katika maisha yetu tuliyoyachagua kama
wakristu kumfuata. Tukumbuke kuwa katika kuwa wakristu wa kweli tunapitia
katika hatua na njia mbalimbali hadi tunapata ufunuo na kumjua Kristu kuwa ni
mwana wa Mungu, na mwokozi wa dunia kama mwanamke Msamaria alivyofanya.
0 Response to "MAHUBIRI YA JUMAPILI YA 3 KWARESMA MWAKA A"
Chapisha Maoni