1.Job
7:1-4
|
2.1Cor
9:16ff
|
3.Mk
1:29-39
|
TAFAKARI “ Kristo
anateseka na wanaoteseka”
Tukianza tafakari yetu
tunapoadhimisha jumapili ya 5 ya Mwaka B wa Kanisa hatuna budi kumshukuru Mungu
kwa mema yake yote aliyotukirima katika wiki hii nzima. Katika masomo yetu yote
ya jumapili ya tano ya mwaka wa kanisa hatuna budi kujifunza yafuatayo
Kujifunza
somo kutoka maisha ya Ayubu na Yesu
Kutoka somo la Kwanza
katika kitabu cha Ayubu tunasikia habari ya kuteseka kwa ayubu na mbali ya kuwa
mcha Mungu, Mungu anampa majaribu ambayo yanaambatana na mateso ambayo Ayubu
hakutarajia. Mungu anamruhusu shetani kumjaribu Ayubu. Marafiki zake Ayubu
waonekana kumdhihaki na kumlaumu kuwa hayo yote yanampata kwa kuwa alimkosea
Mungu, lakini Ayubu anaona hayo yote ni ubatili na utupu wa maisha.(Ayubu
8:13-19) “ Ndivyo ulivyomwisho wa wale
wamsahauo Mungu, na Matumaini yake huyo mbaya huangamia (13).” Uthabiti wake
utavunjika, na matumaini yake huwa ni nyuzi za buibui.”(14). Hayo yalikuwa
ni maneno ya mmoja wa rafiki zake ayubu aliyeitwa Bildadi aliyonena wakati
Ayubu yuko kwenye mahangaiko. Kutoka katika fundisho hili tunajifunza kuwa hata
wale waonekanao kuwa ni marafiki waweza pia kuwa maadui wakati wa dhiki, waweza
pia kunena mabaya juu ya wenzao walio katika dhiki au katika mafundisho kama
tunavyoambiwa katika kitabu cha Ayubu juu ya rafiki zake.
Katika maisha yetu
tunasikia historia ya yale yaliyotokea kwa Ayubu tuko mbali nayo kiwakati, ila
nasi hatuko mbali na hayo yaliyotokea kwake bali tunayashuhudia katika maisha
yetu wenyewe, tunashuhudia watu wasio na hatia jinsi wanavyoteseka,
tunashuhudia ndoa zinavunjika, tunashuhudia maovu ya kila aina yanaendelea
katika jamii zetu na hasa katika mifumo mbalimbali ya utawala, tunashuhudia
mifumo mibovu ya kiuchumi, tunashuhudia umwagaji wa damu kwa sababu ya uchu wa
madaraka kwa baadhi ya watu. Dunia tunayoishi kwa sasa inaningia juu ya utovu
wa maadili ambapo tabaka za wanyonyaji, wala rushwa, wanafiki na wavunja amani
zinatawala.
Katika maisha yetu kama
wakristu tunaweza tukasema nini juu ya habari ya Ayubu kulingana na imani yetu
na hali zetu za maisha?? Tuna nini la kusema kwa ndugu zetu walio katika vilio
na majonzi kwa sababu ya maisha? Huzuni, kilio na machungu ni moja ya sehemu
ambazo tunazikuta hasa katika ujumbe wa neno la Mungu; hilo pia tunaliona
kinywani mwa Bwana wetu Yesu Kristu ile siku ya ijumaa kuu (Lk 23:34). Katika
dunia Yetu ya leo tunasikia vilio vingi mno tunaishi katika dunia iliyojaa
kelele za majonzi, sisi kama wakristu tunaitikia namna gani kwa watu wenye
majonzi na vilio?
Katika somo la injili
tunaona wenye magonjwa mbalimbali wanaletwa kwa Yesu akawaponye, na mara moja
Yesu bila ya kuuliza nini maana ya mateso katika maisha anawaponya. Kama
wakristu, na wafuasi wa Kristu tunaalikwa kufanya kama Kristu alivyofanya,
tunaalikwa kuwa waponyaji wa roho na mwili, na kweli hili linawezekana. Uwepo
wetu kwa wale wenye masumbuko ya kimwili na kiroho ni faraja kubwa sana kwao
hata kuliko chochote kile, maneno yenye faraja, na ushauri mzuri kwao ni njia
mojawapo ya kuponya wenzetu wenye mahangaiko katika maisha. Hasa tunaalikwa
kuwa karibu na wale waliopoteza imani kwa Kristu na matumaini kuwafariji ili
wapate kumrudia Mungu muumba wao, hayo yote yanawezekana pindi tukimwachia
Kristu Yesu atawale katika mioyo yetu na atutumie kama vyombo vyake ili kufanya
utawala wake uenee duniani kote.
Maandiko matakatifu leo
yanatupa motisha kuwa tuwe daima watu wa kusikiliza wenzetu walio katika raha
na pia katika unyonge (upweke,utupu wa maisha- waliokosa ajira, walioonewa,
wagonjwa n.k,), tumwombe Mungu awabariki hao wote wenye kusumbuka kupitia
vinywa vyetu na mikono yetu.
Ishara
ya uponyaji wa Mungu
Kuna mjadala ambao
huendelea kwa baadhi ya watu hasa wale walioshikilia msimamo wa kisayansi na
kipagani kuhusu uponyaji wa Yesu kwa watu waliokuwa wagonjwa, mawazo ya watu
kama hawa ni kuwa, je Yesu aliweza kabisa kuponya wagonjwa wa mwili au aliponya
wale waliokuwa na pepo peke yake? Mjadala kama huo haufai na uko nje ya malengo
ya imani ya Kikristu. Ukweli ni kwamba Kristo aliponya mwili na roho. Kristu
anavyofanya uponyaji hafanyi huo uponyaji kama miujiza ili kushangaza watu,
Kristu anafanya miujiza kuonyesha huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake, pia
uponyaji aliofanya Kristu ilikuwa ni ishara kuwa mkono wa Mungu daima upo
unafanya kazi daima duniani.
Ilitokea siku moja
madaktari walikuwa na maongezi juu ya uwezo wa sala kuwasaidia wagonjwa
kupona,waliuliza swali kuwa sala inatenda zuri lolote kwa wagonjwa?kundi moja
la watu waliokuwepo hapo, walisema kuwa “ sala huwa inasaidia wale wanaosali
kujisikia kuwa wanafanya kitu kwa mgonjwa, ila haimsadii mgonjwa kupona kamwe.”
Kundi jingine la watu lililokuwepo lilisema “ sala kimsingi inamsaidia mgonjwa
kupona.” Kundi la kwanza lilipinga kundi la pili kwa kusema hii kisayansi
haiwezekani haiwezi thibitishwa kamwe. Hivyo ilibidi ifanywe jaribio
kuthibitisha kama sala yawezekana ikamfanya mgonjwa akapona. Jaribio hili
lilifanywa kwa wale wagonjwa wa moyo. Hivyo ilichukuliwa shauri kuwa baadhi ya
wagonjwa wa moyo waombewe bila ya wao kujua kuwa wanaombewa na pia kuwafanya
wanaowambea wasijue ni nani wanamwombea. Hivyo waombaji walipewa idadi ya watu
waliopaswa kuombewa bila ya kuwafahamu, na madaktari waliokuwa wanatibu hao
watu hawakuwafahamu kama walikuwa wanaombewa. Nini kilitokea? “ ona waliokuwa
wanaombewa walipona haraka” lilisema lile kundi lilokuwa linadai kuwa sala ina
matokeo mazuri kwa mgonjwa, tukimtanguliza Mungu mbele kuna makubwa
yapatikanayo kuliko kuitanguliza sayansi.
Imani
na msalaba wa Kristu
Kila mmoja wetu kwa
namna moja au nyingine anajua ninini maana ya mateso iwe ni mateso ya kimwili,
kihisia, kiakili au kiroho. Hakuna namna ambayo mateso yaweza kuzuilika maana
ni sehemu ya asili na maisha yetu. Twaweza jiuliza kuwa mateso kadiri ya imani
yetu yanatufundisha nini?? Mateso huja kwa namna nyingi na huja katika hatua
mbalimbali katika maisha ya mwanadamu, mateso yaweza kuja wakati wa utoto,
ujana, au katika uzee. Mateso yako ya namna nyingi ila hatuna kipimo na
hayawezi pimwa kwa kipimo chochote kile. Kilio na machozi ya Ayubu kama
tulivyosikia katika somo la kwanza ni kilio ambacho mateso yake hayana mbele
wala nyuma ila limebaki kama fumbo. Ayubu baada ya kupata hayo majaribu na
mateso yote anaonekana kumsahau Mungu. Ayubu alikuwa akiishi maisha ya kumcha
Mungu, sasa anashangaa kwa nini Mungu analeta hiyo mikasa katika maisha yake na
familia yake. Mungu ambaye alikuwa kama rafiki yake wa karibu sasa anaonekana
kama adui. Kadiri ya mazoea mikasa na matatizo hasa ya kiwemo yale ya kiafya,
kifamilia, na kiuchumi huwa yanawafanywa wengi wamsahau Mungu na kukimbilia
miungu wengine ikiwemo pia kubadili madhehebu. Ayubu ni kielelezo cha kila
mwanadamu. Ni kielelezo kinachoonyesha binadamu akiwa katika mwanga na akiwa
katika giza pia. Hasa ni kielelezo kinacholenga sehemu ya giza(kumweka Mungu
pembeni mbele ya shida) ya mwanadamu duniani.
Imani na msalaba wa
Kristu ni vitu visivyoweza kutenganishwa. Ni chini ya msalaba wa Kristu imani
yaweza kuimarika. Kristu mwenyewe alishiriki kikamilifu mateso ya mwanadamu.
Kristo alikubali kuubeba udhaifu wetu sisi binadamu. Msalabani tunaona Kristu
ndipo Kristu alipoonyesha upendo na unyenyekevu wake. Pale msalabani tunamwona
Yesu akilia “ Mungu mbona umeniacha”( Mt 27:46), kilio hicho ni tendo la
kiimani, ni lugha ya kiimani hasa pale unapohitajika msaada wa Mungu pindi giza
likitawala katika maisha ya kila mmoja wetu. Mungu hakumwacha Yesu ateseke,
bali kuteseka kwake ndo kumeleta uzima kwa watu wote duniani. Hivyo tunavyoadhimisha
jumapili ya tano ya mwaka B mwaka wa Kanisa, hatuna budi kutambua kuwa katika
magumu yetu yote kristu bado hajatuacha bado anatembea nasisi kutufariji.
0 Response to "MAHUBIRI JUMAPILI YA 5 YA MWAKA B"
Chapisha Maoni